Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Posta Tanzania linakabiliwa na wingi wa wafanyakazi na uongozi duni kwa zaidi ya miaka 24 sasa, hali inayohitaji kubadilishwa kwa sasa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, anasema ametembelea posta zote nchini na kuzungumza na wafanyakazi lakini moja ya mambo anbayo amejifunza kwa wafanyakazi wa shirika hilo ni kwamba lina mali nyingi lakini wanakufa njaa.
Prof Mbarawa anasema mali wamezikalia wenyewe na wameshindwa kuzitumia na kubaki kulalamika bila kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.
Anasema shirika linakabiliwa na changamoto ya uwingi wa wafanyakazi huku kazi wanazozifanya zikiwa ni chache, kwani hazilingani na idadi yao na hivyo kipato kutokidhi haja.
Pia anasena shirika limekosa uongozi bora na hivyo kukosa maendeleo endelevu na kuwa duni zaidi kwani tangu amelijua shirika hilo ni zaidi ya miaka 24 sasa lakini bado halina maendeleo ya maana.
“Mahusiano ya utendaji wa kazi baina ya wafanyakazi na uongozi mzima ni duni na hivyo kudai mabadiliko.“Nitafanya mabadiliko,” anasema na kuongeza huku akitolea mfano wa Shirika la Reli: “Mfano mzuri nilipotembelea Shirika la Reli Tanzania, nako pia kulikuwa na tatizo kama hilo lakini baada ya kuuliza kiundani nikaambiwa tatizo ni uongozi na si fedha, kwa hiyo tangu nilipotengua uongozi hadi leo, shirika hilo lina maendeleo mazuri na linafanya vizuri katika utendaji wa kazi,” anasema Mbarawa.
Vilevile anasema katika hilo nalo lilikuwa na tatizo la kulipwa kwa mishahara yao wafanyakazi na alipozungumza Mkurugenzi wa shirika hilo hakuwa na jibu la kumpatia.
Pia anasema kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi hawafanyi kazi ipasavyo kwa kigezo cha kutokulipwa mishahara.
Anasema: “Nitawanyoosha wafanyakazi wote wanaozembea kufanya kazi kama nilivyofanya katika makampuni mengine.
“ Nitaleta kiongozi ambaye haijui posta kabisa, nafikiri huyo anaweza kuiongoza vizuri kuliko akipewa madaraka mtu ambaye anaifahamu,” anasema Mbarawa.
“Kwani baada ya matembezi ya ofisi zote za posta nimejua kuwa wafanyakazi ni wengi sana lakini nimewakuta wateja 20 tu, je, wafanyakazi wengine mnafanya nini?” anaongeza.
Anasema katika shirika hili kuna viongozi wengi na wafanyakazi lakini bado hawafanyi kazi ipasavyo.
“Hapa tulipofikia hatuwezi kufanya kazi kwa kujuana na kubebana kimadaraka wakati watu hawafanyi kazi ipasavyo,” anasema Mbarawa.
Anasema kama Shirika lina wafanyakazi lukuki na rasilimali nyingi za kutosha lakini tatizo linakuja katika uongozi, kwanini hao wasioweza kazi hawaondolewi katika shirika? Kwanini wanaangaliwa kila siku kwa mambo wanayoyafanya?
“Shirika la Posta lina miradi mingi ya maendeleo mojawapo ni mradi wa nyumba zaidi ya tatu zilizopo katika Mkoa wa Mwanza na rasilimali nyingine nyingi, kwanini shirika lina miradi kama hiyo lakini linashindwa kuitumia na kuiendeleza endapo kama ina faida ifanyieni kazi,” anasema Mbarawa.
“Nawasihi wafanyakazi wa kampuni hii msikimbilie kudai mishahara yenu wakati kazi mliyofanya haionekani, hilo halitawezekana kwangu pia hata kwa Serikali kwani haiwezi kuwaelewa kabisa, hata vitabu vya dini vimeandikwa kuwa asiyefanya kazi na asile, sasa basi kama kazi mnazofanya hazionekani iweje mnadai mishahara.
Mmoja kati ya wafanyakazi wa Shirika hilo, David Ang’o, anasema kama shirika lina magari mengi ambayo ni mabovu lakini wanashindwa kuyatumia kwa matumizi ya kuyaendesha kutokana na ubovu huo kwani hata walipoyapeleka gereji imeshindikana kutengenezwa kutokana na Serikali kukosa fedha.
“Tunaamini kuwa taasisi haina fedha ya kutosha lakini inatutaka tutumie magari mabovu, ona ni mabovu ambapo yamekaa zaidi ya mwaka mmoja sasa kiasi kwamba ukizingatia hata shirika lenyewe kwa kipindi kirefu sasa haitupatii mafao yetu kwa wakati mwafaka, inatuwia vigumu sisi wafanyakazi.
“Huwezi kuendesha shirika bila kuwa na mahusiano mazuri na yalio bora baina ya wafanyakazi na uongozi na ndio maana tunashindwa kuendelea kimaendeleo katika shirika hili kutokana na ushindani usio na mafanikio baina yetu,” anasema Ang’o.
Anasema: “Tunaomba Waziri kwa dhamana yako uturuhusu tufanye kikao tukiwa na mweyekiti wa bodi ili tuweze kulizungumzia jambo hili kiundani zaidi.”
Mwenyekiti wa Shirika hilo, Dr. Harun Kondo, anasema kama shirika pamoja na wingi wetu tujitahidi kutekeleza mipango mikakati ambayo tuliiweka kwa mwaka jana ingawa kuna baadhi haijakamilika.
Anasema lengo kuu ni kuimarisha shirika hili ili liwe katika ubora wa hali ya juu dhidi ya utoaji wa huduma nzuri na bora zaidi.