27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

MBARAWA KUUNG’OA UONGOZI MBOVU POSTA

Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM


SHIRIKA la Posta Tanzania linakabiliwa na wingi wa wafanyakazi na uongozi duni kwa zaidi ya miaka 24 sasa, hali inayohitaji kubadilishwa kwa sasa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, anasema ametembelea posta zote nchini na kuzungumza na wafanyakazi  lakini moja ya mambo anbayo amejifunza kwa wafanyakazi wa  shirika hilo ni kwamba lina mali nyingi lakini wanakufa njaa.

Prof Mbarawa anasema mali wamezikalia wenyewe  na wameshindwa kuzitumia na kubaki kulalamika bila kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.

Anasema shirika linakabiliwa na changamoto ya uwingi wa wafanyakazi  huku kazi  wanazozifanya  zikiwa ni chache, kwani  hazilingani na idadi yao na hivyo kipato kutokidhi haja.

Pia anasena shirika limekosa uongozi  bora na hivyo  kukosa maendeleo endelevu na kuwa duni zaidi kwani tangu amelijua shirika hilo  ni zaidi ya miaka 24 sasa  lakini bado halina maendeleo  ya maana.

“Mahusiano ya utendaji wa kazi baina ya wafanyakazi na uongozi mzima ni duni na hivyo kudai mabadiliko.“Nitafanya mabadiliko,” anasema na kuongeza huku akitolea mfano wa Shirika la Reli: “Mfano mzuri  nilipotembelea  Shirika la Reli Tanzania, nako pia kulikuwa na tatizo kama  hilo lakini baada ya kuuliza kiundani  nikaambiwa tatizo ni  uongozi  na si fedha, kwa hiyo tangu nilipotengua uongozi  hadi leo, shirika hilo lina maendeleo mazuri na linafanya vizuri katika utendaji wa kazi,” anasema Mbarawa.

Vilevile anasema katika  hilo nalo lilikuwa na tatizo la kulipwa kwa  mishahara  yao wafanyakazi  na alipozungumza  Mkurugenzi  wa shirika hilo hakuwa na  jibu la kumpatia.

Pia anasema kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi  hawafanyi  kazi  ipasavyo kwa kigezo cha kutokulipwa mishahara.

Anasema:  “Nitawanyoosha wafanyakazi  wote wanaozembea kufanya kazi  kama nilivyofanya  katika makampuni mengine.

“ Nitaleta kiongozi ambaye haijui posta kabisa, nafikiri huyo anaweza kuiongoza vizuri kuliko akipewa madaraka mtu ambaye anaifahamu,” anasema Mbarawa.

“Kwani baada ya matembezi ya ofisi zote za posta nimejua kuwa wafanyakazi ni wengi sana lakini nimewakuta wateja 20 tu, je, wafanyakazi wengine mnafanya nini?” anaongeza.

Anasema katika shirika hili kuna viongozi wengi na wafanyakazi lakini bado hawafanyi kazi ipasavyo.

“Hapa tulipofikia hatuwezi kufanya kazi kwa kujuana na kubebana kimadaraka  wakati watu hawafanyi kazi ipasavyo,” anasema Mbarawa.

Anasema kama  Shirika lina wafanyakazi  lukuki na rasilimali nyingi  za kutosha  lakini tatizo linakuja  katika uongozi,  kwanini hao wasioweza  kazi hawaondolewi katika shirika? Kwanini  wanaangaliwa kila siku kwa mambo wanayoyafanya?

“Shirika la Posta lina miradi  mingi  ya maendeleo mojawapo ni mradi wa nyumba  zaidi ya tatu  zilizopo katika  Mkoa wa  Mwanza na rasilimali nyingine nyingi, kwanini shirika lina miradi kama hiyo lakini linashindwa kuitumia  na kuiendeleza  endapo kama ina faida ifanyieni kazi,” anasema Mbarawa.

“Nawasihi wafanyakazi wa kampuni hii msikimbilie kudai mishahara  yenu wakati   kazi mliyofanya  haionekani,  hilo halitawezekana  kwangu  pia hata kwa Serikali kwani haiwezi kuwaelewa kabisa, hata vitabu vya dini vimeandikwa kuwa  asiyefanya kazi na  asile, sasa  basi  kama kazi mnazofanya hazionekani  iweje  mnadai mishahara.

Mmoja  kati ya wafanyakazi wa Shirika hilo, David  Ang’o, anasema kama shirika lina magari mengi ambayo ni mabovu  lakini wanashindwa kuyatumia kwa matumizi ya kuyaendesha kutokana na ubovu huo kwani hata walipoyapeleka  gereji imeshindikana kutengenezwa kutokana na Serikali  kukosa  fedha.

“Tunaamini  kuwa taasisi haina fedha ya kutosha  lakini inatutaka tutumie magari mabovu, ona  ni mabovu ambapo yamekaa zaidi ya mwaka mmoja sasa  kiasi kwamba ukizingatia hata shirika lenyewe  kwa kipindi kirefu sasa  haitupatii  mafao yetu kwa wakati mwafaka, inatuwia vigumu sisi wafanyakazi.

“Huwezi kuendesha  shirika  bila kuwa na mahusiano mazuri na yalio bora  baina ya wafanyakazi  na uongozi na ndio maana  tunashindwa kuendelea kimaendeleo katika shirika hili  kutokana na ushindani usio na mafanikio baina yetu,” anasema Ang’o.

Anasema: “Tunaomba Waziri  kwa dhamana yako uturuhusu tufanye kikao tukiwa na mweyekiti wa bodi  ili tuweze kulizungumzia  jambo hili kiundani zaidi.”

Mwenyekiti wa Shirika hilo, Dr. Harun  Kondo, anasema  kama shirika pamoja na wingi  wetu tujitahidi kutekeleza  mipango mikakati ambayo tuliiweka kwa mwaka jana  ingawa kuna baadhi haijakamilika.

Anasema lengo kuu ni kuimarisha shirika hili  ili liwe katika ubora wa hali ya juu dhidi ya utoaji wa huduma nzuri na bora zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles