29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MBAPPE, PAUL POGBA SILAHA ZA MAANGAMIZI UFARANSA

MOSCOW, URUSI


UFARANSA wamefanikiwa kuingia hatua ya fainali kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, baada ya juzi kushinda bao 1-0 dhidi ya Ubelgiji.

Ushindani ulikuwa wa hali ya juu katika mchezo huo kutokana na ubora wa kila timu, lakini Ufaransa imeweza kuwazidi wapinzani kutokana na vitu vifuatavyo.

Mlinda mlango

Hadi kufikia mchezo wa juzi, Ufaransa imeruhusu jumla ya mabao manne tangu kuanza kwa michuano hiyo huku wakiwa wamecheza jumla ya michezo sita.

Walikuwa na mlinda mlango ambaye alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu, Hugo Lloris, anayekipiga katika klabu ya Tottenham.

Safu ya ulinzi

Tangu kuanza kwa michuano hiyo, Ufaransa haijapoteza hata mchezo mmoja kati ya sita waliocheza, walitoka suluhu dhidi ya Denmark katika hatua ya makundi, lakini michezo mingine yote mitano waliibuka na ushindi.

Ubora wa safu ya ulinzi ulikuwa unaundwa na beki wa kati, Samuel Umtiti (Barcelona), Raphael Varane (Real Madrid), Benjamin Pavard (Stuttgart), Lucas Hernandez (Atletico Madrid) na wengine.

Hao waliweza kumuweka sehemu salama mlinda mlango wao, Lloris, ili asiwe kwenye wakati mgumu.

Viungo

Wachezaji ambao walikuwa wanaunda safu ya kiungo walikuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha washambuliaji wake wanalishambulia lango la wapinzani.

Katika safu hiyo kulikuwa na N’Golo Kante (Chelsea), Blaise Matuidi (Juventus), Paul Pogba (Man United) na Corentin Tolisso (Bayern Munich).

Wachezaji hao walikuwa kwenye kiwango bora kuhakikisha wanaleta mawasiliano kati ya safu ya ulinzi na ushambuliaji.

Kila mchezaji alionekana kuvaa jezi kwa ajili ya kulipigania taifa hilo na kutaka kuandika historia mpya baada ya mwaka 1998 kufanya hivyo.

Pogba alikuwa anahakikisha anapiga mipira mirefu ili kuwafikia washambuliaji, kazi hiyo ilikuwa inafanywa na mchezaji mwingine Kante.

Washambuliaji

Uwepo wa Kylian Mbappe mwenye umri wa miaka 19, akitokea klabu ya PSG, Antoine Griezmann wa Atletico Madrid, kulileta changamoto kubwa kwa safu ya ulinzi ya wapinzani wao katika kila mchezo.

Wachezaji hao hadi sasa kila mmoja ana jumla ya mabao matatu. Mbappe alionekana kuwa tishio tangu kwenye mchezo dhidi ya Argentina katika hatua ya 16 bora ambapo Ufaransa ilishinda mabao 4-3, huku mchezaji huyo akifunga mabao mawili na kutoa pasi ya mwisho.

Kwa hali ya kawaida Ufaransa imeonekana kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi vijana wakiwa na kasi kubwa na hadi sasa wamefunga jumla ya mabao 10.

Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Didier Deschamps, amekuwa na lengo la kutaka kuandika historia mpya katika timu hiyo kuwa wa kwanza kutwaa taji hilo mara mbili akiwa mchezaji na kocha.

Alikuwa nahodha mwaka 1998 wakati timu hiyo inatwaa ubingwa kwenye ardhi ya nyumbani na sasa ana ndoto ya kufanya hivyo akiwa kocha.

Timu inayokutana na Ufaransa katika fainali Jumapili lazima iwe makini katika kuwazuia wapinzani wao katika safu ya ushambuliaji na viungo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles