27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

HII NDIYO HOTELI ALIYOFIKIA OBAMA AKIWA SERENGETI

Mwandishi Wetu


HOTELI za Singita Grumeti iliyo kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo imempokea Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama, ni moja ya hoteli zenye hadhi kubwa duniani ambayo imekuwa ikipokea ugeni wa watu mashahuru duniani.

Kabla ya ujio wa Obama na familia yake, Marais wengine wastaafu wa Marekani Bill Clinton aliyewahi kuwa Rais wa 42 wa Marekani na George W Bush nao waliwahi kufikia katika hoteli hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa mmiliki wa kampuni za Microsoft duniani bilionea Bill Gates naye ni miongoni mwa mabilionea waliowahi kufikia katika hoteli hiyo.

Pia bilionea wa Kirusi anayemiliki Klabu ya Chelsea ya Uingereza, Roman Abramovich, alipotembelea nchini Septemba 2009 alilala katika hoteli hiyo.

Mwingine ni bilionea wa kihindi, Mukesh Ambani ambaye kwa sasa anaingia katika orodha ya matajiri 20 duniani aliwahi kufika nchini na kufikia kwenye hoteli hiyo.

Uongozi wa hoteli hiyo haukuweza kupatikana haraka kwa ajili ya kutoa mwelekeo wa gharama zake kwa sasa, lakini baadhi ya vyanzo vyetu ambavyo vimewahi kufika hotelini hapo, vinadai kwa usiku mmoja gharama hapo ni mamilioni ya shilingi mbali na huduma atakazotaka mteja.

Katika eneo hilo kuna malazi ya kwenye mahema na nyumba za kisasa zilizojengwa katika hali ya kuendelea kulinda uoto wa asili.

Katika malazi hayo, mteja anaweza kuendelea kuangalia wanyama akiwa ndani ya chumba chake na mandhari ya kuvutia iliyozunguka eneo hilo.

Kutokana na mazingira ya asili kuendelea kutunzwa kwenye eneo hilo, wanyama hufika mpaka karibu kabisa na zilipo nyumba ama mahema jambo linaloongeza umaarufu na ubora wa hoteli hiyo.

Katika eneo la hema namba 10 lililoko ukanda wa kaskazini wa hifadhi hiyo, jirani kabisa na eneo la wazi la Kijiji cha Makundusi, Pori la Akiba la Grumeti na Hifadhi ya Wanyamapori ya Ikona, limejengwa vyema kwenye kilima cha Sasakwa eneo ambalo linatoa fursa ya kujionea hifadhi hiyo kwa ukubwa wake.

Kampuni ya Singita inayomiliki hoteli hiyo imekuwa ikijihusisha na uhifadhi wa wanyama katika maeneo kadhaa duniani kwa karibu miaka 25 iliyopita ikimiliki hoteli 12 za kifahari ambazo zimekuwa zikiongoza kwa tuzo za ubora katika maeneo matano ya Afrika.

Taarifa za mitandaoni zinaeleza kuwa wasafiri wengi wenye uwezo kifedha, wamekuwa wakipendelea  kutumia hoteli hizo kutokana na namna zilivyo na maeneo mapana ya kutosha na uzuri wa maeneo yanayozizunguka, ukomo wa idadi ya wageni na magari yanayoingia na upekee wa kuwaona wanyama uwapo kwenye mahema ama ndani ya nyumba.

Inaelezwa kuwa huduma ambazo zimekua zikitolewa zimewafanya wateja wengi kuona mabadiliko katika vipindi vyote vya maisha yao mara wanapoondoka katika maeneo hayo, hivyo kuzifanya kuwa sehemu za kukumbukwa.

Kutokana na ubora wake, Hoteli ya Singita Grumeti Reserves inatajwa kuwa kithibitisho cha utajiri wa vivutio vilivyopo Tanzania, ikitajwa kuwa ni hoteli namba moja duniani, baada ya kuchukua tuzo mara mbili mfululizo.

Tuzo hizo hutolewa kila mwaka na taasisi maarufu ya Marekani ijulikanayo kama US Travel and  Leisure ambayo hujishughulisha na viwango vya biashara ya utalii duniani.

Mmiliki wa hoteli hiyo ni Mmarekani Paul Tudor ambaye ameshawahi kuwekwa kwenye orodha ya mabilionea katika jarida la Forbes ambaye anashirikiana na Luke Bailes wa Afrika Kusini.

Sasakwa Lodge

Hii ni moja ya sehemu ya hoteli iliyopo kwenye kilima kinachoitwa Sasakwa Hill, ambayo imejengwa kwa mawe na matofali, huku paa lake likijengwa kwa bati kisha kuwekewa mawe ya nakshi wanayoyaita ‘slates’ ambayo hupatikana maeneo hayo.

Inaelezwa kuwa ndiyo lodge kubwa kuliko zote hotelini hapo ina vyumba vilivyojengwa kwa mtindo wa “cottages” vipatavyo 15.

Sabora Plains Tented Camp ipo katika eneo tambarare ambalo wageni wengi wanaofika mbugani hapo hupenda kupumzika na kuota jua.

Nyingine ni Singita Explore, Singita Mara River Tented Camp, Faru Lodge, Serengeti House  ambazo zote zimekuwa zikihudumia wateja wake kwa gharama tofauti kutokana na chaguo lao wawapo kwenye hifadhi hizo za Serengeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles