AVELINE KITOMARY NA NEEMA SIGALIYE (TUDARCO) -DAR ES SALAAM
MTAFITI Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Gelagista Gwarasa, amesema hakuna utafiti unaoonyesha maziwa ya mama yanaongeza nguvu za kiume na kuwataka wanaume waachane na imani hizo potofu.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana katika mwendelezo wa Wiki ya Unyonyeshaji, Gwarasa alisema wanaume wanaonyonya maziwa ya kinamama wanaamini yataongeza nguvu za kiume kitu ambacho si kweli.
“Tafiti hazionyeshi, lakini kwa sababu maziwa ya mama yana virutubisho, yanaweza kuongeza nguvu.
“Kuna baadhi ya wanaume wamekuwa na imani wakinyonya maziwa ya mama huongeza nguvu za kiume, hii si kweli, waachane na tabia hizo,” alisema Gwarasa.
Aliwashauri kula vyakula vyenye virutubisho mbalimbali vitakavyoweza kuongeza nguvu za kiume, kwa kuwa ndiyo njia sahihi.
Alisema wanaume wengi walioko maeneo ya vijijini hawana tatizo la kuishiwa nguvu za kiume kutokana na kula vyakula vinavyoweza kuwasaidia kulingana na jinsi wataalamu wanavyowashauri.
“Wataalamu wanashauri kula vyakula mchanganyiko wa nafaka, mizizi na mboga mboga, na kwa kina baba wale mara tano kwa siku milo mikuu mitatu.
“Mfano kina baba wa vijijini wengi wana nguvu na huwezi kusikia wana tatizo la upungufu wa nguvu za kiume, lakini wanaume wa mijini wanapenda kula vyakula laini,” alisema Gwarasa.
Aliwataka wanaume kuacha kula vyakula vyepesi vyepesi kama tambi, chipsi na mayai na badala yake wale vyakula vyenye mchanganyiko wa nafaka na mbogamboga.