22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

BoT yaonya wanaofanya ushirikina wa noti

*Yataka wanaojihusisha vitendo hivyo na wanaoshuhudia kupewa adhabu kali

BENJAMIN MASESE-MWANZA

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), Kanda ya Ziwa, imevitaka vyombo vinavyosimamia na kutunga sheria kuchukua hatua kwa watu wanaoendekeza imani za ushirikina na kusababisha uhalifu au uchakavu wa noti halali za Sh 10,000, Sh 5,000, Sh 2,000 na Sh 1,000 kwani ni gharama kuchapisha mpya.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Idara ya Uchumi wa Benki Kuu Kanda ya Ziwa, Dk. James Machemba na Mkuu wa Idara ya Huduma za Mabenki, Gloria Mwaikambo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza katika maonyesho ya wakulima – Nanenane.

Akizungumzia uharibifu wa noti, Mwaikambo alisema kama BoT kazi yao ni kuchapisha noti mpya, kusambaza na kupokea zilizochakaa, shughuli hiyo hugharimu fedha nyingi, hivyo kitendo chochote cha makusudi ya kuharibu kwa kuchana kipande cha noti, kuikunja ovyo au kuiwekea alama yoyote kwa imani ya ushirikiana ni kosa.

Mwaikambo alisema hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa kuanzia kwa mtu anayeshuhudia tukio hilo.

Alisema pia vyombo vinavyotunga na kusimamia sheria vikiwamo Bunge, Mahakama na Polisi, navyo vinapaswa kulichukulia jambo hilo kwa uzito kwa kutoa adhabu kali ili kupunguza gharama za kutengeneza noti mpya.

“Kuna watu wanaendekeza imani za kishirikina na kusababisha noti halali kuchakaa kwa uharaka.

“Wapo wafanyabiashara wa makundi mbalimbali na makondakta ambao wakipokea fedha wanaikata kipande kidogo kwenye kona, imani yao ni kwamba wasiibiwe bila kujua.

“Kitendo hicho ni kosa kisheria, wito wetu ni kuviomba vyombo vya kutunga sheria, wasimamizi wa sheria na watumiaji wa sheria kila mmoja alione jambo hilo lina uzito wake.

“Uchakavu mwingine unatokana na shughuli za wafanyabiashara ndogo ndogo, hasa kinamama wa mboga mboga, mama lishe, bucha, wauza mkaa na wengine ambao hupokea noti ikiwa safi, lakini wanazipokea mikono yao ikiwa na mafuta au uchafu fulani, pia utunzaji wao si salama na inafikia hatua hadi panya wanatafuna kutokana na harufu ya mafuta au nyama,” alisema.

Mwaka 2016, BoT ilitangaza mkakati wa kuondoa noti zote za Sh 500 ndani ya kipindi cha miezi minne kutokana na uchakavu.

Machi mwaka huu, wakazi wa Mkoa wa Kigoma walitajwa kuongoza kwa uchafuzi wa fedha, hususan noti kuliko mikoa yote nchini, wakifuatiwa na Kagera.

Hayo yalibainishwa na Meneja Msaidizi wa Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Victoria Msina, alipozungumza na viongozi  wa Serikali, madiwani, wafanyabiashara na wananchi mjini Kigoma.

“Utafiti tuliofanya tumebaini Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuchafua noti, fedha zinachakaa mno ukilinganisha na mikoa mingine, ndiyo maana tumeamua kutoa elimu kwa umma tukianza na mikoa hii miwili (Kigoma na Kagera),” alisema Msina.

BoT imekuwa kwenye mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali ili wajue umuhimu wa kutunza fedha na kuepuka uchakavu wa noti na sarafu, sambamba na alama muhimu ili kutofautisha noti halali na bandia.

Imebainika kuwa suala la kuhifadhi fedha, hasa noti katika mazingira nadhifu, bado ni changamoto kubwa kwa Watanzania wengi, hasa maeneo ya pembezoni ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, BoT imelazimika kuziondoa katika mzunguko noti nyingi zilizochoka, hasa zile ambazo zimekuwa kwenye mzunguko wa fedha wa kawaida.

Hivi karibuni, Meneja Msaidizi Idara ya Sarafu kutoka BoT, Abdul Dolla, akiwa kwenye mafunzo kwa wanahabari za uchumi Dodoma, alisema noti ya Sh 500 ndiyo inayochakaa zaidi.

Alisema hali hiyo inatokana na kuwa noti hiyo imechukua nafasi kubwa katika mzunguko wa fedha, jambo liloifanya BoT kutoa sarafu ya Sh 500.

“Lakini kwa sasa noti ya Sh 1,000 ndiyo iliyochukua nafasi katika mzunguko kutokana kuwa ni noti ya chenji,” alisema.

Dolla alisema sababu ya fedha hizo kuchakaa haraka inatokana na kutumika zaidi katika mzunguko wa fedha hasa kwa kuzingatia kundi kubwa la wananchi ndio watumiaji wakubwa.

“Noti ya Sh 500 na 1,000 zinatumika zaidi ukilinganisha na noti ya Sh 10,000 au 5,000. Ni fedha ambazo zipo katika mzunguko zaidi.

 “Pia utunzaji wa fedha bado changamoto kubwa katika jamii na ndiyo maana zinachakaa mapema. Ukifuatilia zaidi utabaini hizi noti za Sh 500 wengi ambao wanazitumia hawazitunzi vizuri na wala hawazipeleki benki,” alisema Dolla.

BOT YATOA FEDHA UNUNUZI PAMBA

Katika hatua nyingine, Meneja wa Idara ya Uchumi wa Benki Kuu Kanda ya Ziwa, Dk. Machemba, alisema tayari BoT imekutana na benki kadhaa pamoja na wanunuzi wa pamba na wamekubaliana kutoa fedha kununulia zao hilo msimu huu na kilo moja itanunuliwa kwa Sh 1,200.

Alisema wanatoa fedha kwa benki nyingine, wametimiza wajibu wao, hivyo aliwataka wakulima baada ya kupata fedha hizo kutoka kwa wanunuzi, ni vema wakawekeza BoT ili kupata faida zaidi kila baada ya miezi sita.

Aliongeza kuwa tayari ununuzi umeanza katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita na Simiyu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles