Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
SHULE za msingi mkoani Morogoro zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni uchakavu wa majengo, uhaba wa nyumba za walimu, ukosefu wa vyoo vya wanafunzi na uhaba wa walimu shuleni.
Changamoto hizo ni miongoni mwa mambo yanayochangia wanafunzi mkoani Morogoro kufanya viabaya katika mitihani yao ya mwisho.
Wilaya za Mvomero, Kilosa na Morogoro Vijijini zinatajwa kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana. Chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya inasemekana kuwa ni mazingira mabovu ya shule nyingi zilizopo wilayani humo.
Wilaya ya Morogoro Vijijini inatajwa kushika mkia katika matokeo hayo ya darasa la saba.
Idadi ya shule zilizofanya vibaya ni 13 ambazo zinatoka katika tarafa za Bungu, Kilole na Kisanga.
Mratibu wa Elimu Tarafa ya Kasanga, Innocent Mloka anasema mazingira ya shule nyingi ni mabaya hivyo wanafunzi wengi hushawishika kutoroka shuleni kabla ya muda wa masomo kuisha.
“Shule nyingi hazina vyoo hivyo walimu hulazimika kuwaruhusu wanafunzi kwenda nyumbani kujisaidia, jambo ambalo huwafanya wengi wao wasirudi darasani pindi wanapokwenda nyumbani,” anasema.
Anasema kuwa mazingira mabaya ya miundombinu kuanzia barabara, madarasa na nyumba za walimu pia umekuwa ukichangia utoro kwa wanafunzi.
“Uhaba wa walimu nalo ni tatizo kubwa kwani kutokana na kuelemewa na masomo, hujikuta wakishindwa kumaliza silabasi kwa wakati na hivyo wanafunzi kujikuta wakikosa maswali mwengi katika mitihani yao ya mwisho.
“Katika shule zetu zote walimu na wanafunzi bado wanajisaidia vichakani, mazingira ya darasani nayo mabaya, nyumbani pia ni shida tupu hivyo walimu wengi hawapendi kufundisha huku,” anasema mratibu huyo.
Naye Mratibu wa Elimu Tarafa ya Kolelo, Salim Timbushe anasema kuwa walimu wengi hukataa kufundisha katika shule za pembezoni kutokana na mazingira ya kufundishia kuwa mabaya.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao wanasema kuwa katika maeneo wanayoishi mwamko wa elimu bado ni mdogo.
Kwamba wazazi wengi wanaona ni vema watoto wao wakatufute riziki mitaani badala ya kwenda shuleni.
“Watoto wengi wakitoka shule wanakimbilia kwenda kuuza bidhaa mitaani na wengine kuendesha bodaboda, kubeba mizigo kwa waachuzi wa mazao, na kwenda migodini badala ya kujisomea,” anasema Khadija Masoud.
Anasema kwa hali hiyo utagundua kuwa wazazi nao ni kikwazo, badala ya kuwahimiza watoto kujisomea, wanawaacha waende mitaani kutafuta fedha… hii yote ni kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
“Shuleni nako ni shida, sijui huwa wanafundishwa nini hawa watoto wetu. Mimi huwa nina desturi ya kuchunguza madaftari ya mwanangu, lakini tangu aanze shule huu mwaka wa tatu sijawahi kuona daftari lake hata moja likiwa limejaa,” anasema mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina Zamoyoni Juhudi.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Wariambora Nkya anakiri kuwapo kwa changamoto hizo na kwamba wanajitahidi kukabiliana nazo.
Anasema kuwa shule nyingi ni chakavu na kwamba utaratibu wa kuzifanyia ukarabati unaendelea kufanyika mwaka hadi mwaka.
Anasema kuwa wanashindwa kumaliza tatizo hilo kwa wakati kutokana na wingi wake.
Kuhusu suala la walimu kukataa kufundisha shule zilizopo katika mazingira magumu, anasema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na halmashauri inaendelea kutafuta njia za kuwashawishi walimu kwenda katika shule hizo.
“Kuhusu suala la vyoo tunawaomba wazazi washirikiane na halmashauri kujenga vyoo bora shuleni ili kuepusha wanafunzi kupata magonjwa ya mlipuko,” anasema.