32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAKILI WAMPIGANIA SHIKUBA

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


WAKILI wa anayedaiwa kuwa Kiongozi wa Taasisi ya Kusambaza Dawa za Kulevya nchini, Ally Haji, maarufu Shikuba na wenzake wawili, Hudson Ndusyepo amesema wanaendelea na rufaa ya kupinga wateja wao kuondolewa nchini hata kama walishaondolewa.

Wakili Ndusyepo alisema hayo jana baada ya wateja wao kuondolewa nchini juzi usiku kwenda Marekani wakati tayari walishakata rufaa kupinga uamuzi wa kuwaondoa nchini uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

“Tunaendelea na rufaa tuliyokata Mahakama Kuu hata kama walishaondolewa, rufaa imepangwa kutajwa Juni 28 mwaka huu, tutakwenda mahakamani,”alisema.

Shikuba na wenzake walishaondolewa nchini kimya kimya kuelekea huko pamoja na kuwepo kwa rufaa iliyokatwa Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa kuwaondoa nchini.

Taarifa za kupelekwa Marekani Shikuba na wenzake, Iddy Mfuru na Tiko Adam zilipatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika akiwemo mkewe na mawakili wa watuhumiwa hao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani, watuhumiwa hao walisafirishwa Mei  2 mwaka huu kwenda Marekani, kujibu mashtaka kuhusiana na biashara ya dawa za kulevya katika Mahakama Kuu ya Huston, Texas.

“Watuhumiwa hao watatu waliwasili nchini Marekani Mei 2, 2017,  kusafirishwa kwao ni matokeo ya ushirikiano mkubwa wa karibu na wa muda mrefu baina ya Serikali za Marekani na Tanzania katika sekta za usalama, usimamizi wa sheria na haki,”ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser.

Taarifa hiyo inadai Machi 2016, jopo la maafisa mashtaka la Huston, Texas, lilipitisha mashtaka dhidi ya Shikuba na washirika wake kwa tuhuma za kula njama kusambaza dawa za kulevya aina ya heroin nchini Marekani katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015.

Aprili 12 mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha ilikubali maombi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe ya kutaka Watanzania hao washikiliwe na kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.

Baada ya uamuzi huo, Aprili 13 mwaka huu Wakili wa Shikuba na wenzake, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu na Adinani Chitale waliwasilisha nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Kisutu na tayari waliwasilisha rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kama sheria inavyowataka endapo hawakuridhika.

Awali Aprili 10 mwaka huu Serikali iliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Kisutu pamoja na vielelezo mbalimbali wakiomba watuhumiwa wazuiliwe na kusafirishwa kwenda Marekani kujibu tuhuma za kujihushisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mahakama ilisikiliza maombi hayo Aprili 11 na kutoa uamuzi Aprili 12 mwaka huu ambapo mahakama ilibariki watuhumiwa hao kwenda nchini humo baada ya kujiridha kwa ushahidi uliotolewa mahakamani.

Mwakyembe aliwasilisha maombi Februari 15 mwaka huu, akiomba mahakama hiyo kuamuru   Shikuba, Mfuru na Tiko washikiliwe wakati wakisubiri kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani kujibu tuhuma za kula njama kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini Marekani.

Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki katika kuiridhisha mahakama waliwasilisha maombi pamoja na ushahidi dhidi ya wajibu maombi wa kuonyesha kujihusisha kwao katika matukio hayo.

Kakolaki alidai maombi yaliambatana na kiapo kilichoapwa na Richard Magnes ambaye katika kiapo chake anadai wajibu maombi wanatuhumiwa kuingiza dawa za kulevya zaidi ya kilo 1.78 Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles