Na NORA DAMIAN
MAUAJI ya viongozi wa kisiasa na Serikali yanayoendelea Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, yanaonekana kuumiza vichwa vya wengi kutokana na polisi kuyahusisha na vitendo vya ujambazi, huku Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kikisema yana harufu ya kigaidi na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, akikinzana na mitazamo hiyo.
Hadi sasa zaidi ya watu 30 wakiwamo askari polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wameuawa mkoani humo.
Askari polisi wanane waliuawa kwa kufyatuliwa risasi mapema Aprili wakitoka kwenye doria katika Kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti na Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC CID), Peter Kubezya na wenzake watatu nao pia waliuawa kwa risasi Februari, mwaka huu.
HOJA ZA WAZIRI
Juzi Waziri Mwigulu alipotembelea polisi wanaoendelea na operesheni wilayani kibiti, aliibua maswali kadhaa yaliyoonyesha wasiwasi kama mauaji hayo yanasukumwa na wafanyabiashara wa mkaa, vitendo vya ujambazi, udini ama ugaidi.
“Kila nikitafakari naona kuna kamchezo kanachezwa, tusipoangalia kamchezo kanakochezwa tutatafuta adui ambaye hakuwapo na tutaacha adui ambaye anahusika.
“Mwanzoni watu tofauti tofauti kila mmoja alitoa tafsiri yake na wengine wakasema eti ni mkaa, tukawa tunatafuta uhusiano wa mkaa na viongozi wa CCM, yaani ugomvi wa mkaa na CCM wapi na wapi!
“Haya ni maswali yaliyoacha maswali mengi kuliko majibu; wengine wakasema misimamo mikali ya dini, tukahoji na CCM ni wapi na wapi kwa sababu CCM si dini hata viongozi wake wauawe?
“Likaja la ujambazi, hii nayo na CCM tofauti yake iko wapi hata watafute viongozi wa CCM waliostaafu miaka mitano iliyopita?
“Wengine wakasema tena ni ugaidi, sasa ugaidi na CCM ni wapi na wapi na yule anayeonyesha viongozi wa CCM ni nani na yuko wapi mpaka awaonyeshe waliostaafu,” alisema.
LHRC
Wakati maswali hayo yakiendelea kuumiza vichwa vya wengi, LHRC imesema kuna dalili za kuwapo kwa vitendo vinavyoshabihiana na ugaidi katika mauaji hayo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, Ana Henga, alisema walipeleka timu kwenda kufanya uchunguzi mkoani humo na kubaini kuwapo kwa dalili hizo.
“Matukio ya ukiukwaji wa haki ya kuishi yanaongezeka na tukitazama mwenendo wa matukio haya, tunaona yanaashiria dalili za uwepo wa vitendo vinavyoshabihiana kama ugaidi.
“Wanauawa watu wanaofanana, wanauawa viongozi wa Serikali, chama fulani na askari polisi… ni kama vile kuna namna fulani ya kutaka kuondoa kundi fulani la watu,” alisema Henga.
Kituo hicho kimependekeza Serikali kufanya utafiti wa kijamii usiokuwa na vitisho ili kubaini chanzo cha mauaji yanayoendelea katika Mkoa wa Pwani.
“Kupeleka askari wenye mitutu ya bunduki hakutasaidia na pengine kutazidi kujenga hofu kwa wananchi, kama watu wabaya wana mipango yao hawashindwi kuitekeleza.
“Ufanyike utafiti wa kina kujua tatizo ni nini na usiwe wa vitisho bali uwe wa kirafiki,” alisema.
Kituo hicho pia kimelishauri Jeshi la Polisi litumie mbinu mbadala kubaini viashiria vya uhalifu katika maeneo hayo na kuboresha mafunzo ya askari polisi.
“Serikali iimarishe dhana ya polisi jamii, iwekeze katika kutoa elimu ya uraia kwa wananchi na iboreshe mazingira ya kazi kwa askari wake,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Ufuatiliaji Ukiukwaji wa Haki za Binadamu, Felista Mauya, alitahadharisha kuwa haki ya kuishi ni ya msingi na kama ikikosekana ni vigumu kuweza kupata haki nyingine.
“Siamini kama Kibiti kulikuwa na mambo ambayo hayajulikani na kuweka kambi inawezekana ukawa ni mpango wa muda mfupi au muda mrefu. Lakini je, kuna mikakati madhubuti ya kumaliza suala hili na hofu inawatoka Watanzania?” alihoji Mauya.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na kituo hicho, inaonyesha kwa mwaka 2016 kulitokea mauaji ya watu 705 ambayo ni yale ya kujichukulia sheria mkononi wakati yaliyofanywa chini ya vyombo vya dola ni manne.
Pia kati ya mwaka 2014 hadi sasa, askari polisi 36 wameuawa na zaidi ya silaha 60 ziliibwa katika vituo vya polisi Newala, Ikwiriri, Kimanzichana, Ushirombo, Tanga, Mgeta, Pugu na Stakishari.
MSIMAMO WA POLISI
Mara baada ya askari wanane kuuawa, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Nsato Marijani Msanzya, alisema askari hao wameuawa wakiwa njiani kuelekea kambini wakitokea lindoni eneo la Jaribu Mpakani, mara baada ya kuwekewa mtego na wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Kamishna huyo alikataa kulihusisha tukio hilo na ugaidi, huku akisema hakuna haja ya kuanzisha kanda maalumu ya kipolisi katika Mkoa wa Pwani licha ya kutokea mashambulio ya kuwaua maofisa wa Jeshi la Polisi mara kwa mara katika eneo hilo.
“Hili si tukio la mara ya kwanza kwa mauaji ya aina hiyo yanayowalenga askari polisi kutokea katika maeneo ya Mkoa wa Pwani, wakiwemo viongozi wa Serikai na watendaji mbalimbali hali inayozidisha hofu kwa wananchi wa maeneo hayo kuhusu usalama wao na mali zao,” ameeleza Kamanda Msanzya.
Aliongeza kuwa uonevu huo unaofanywa dhidi ya askari sasa umefika mwisho na kusema kuwa jeshi hilo linaingia katika operesheni maalumu ya kuwasaka wahalifu hao kwa lengo la kukomesha vitendo vya kikatili vya mauaji vinavyofanywa na makundi ya wahalifu.