22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

MZIMU WA RAMBIRAMBI ZA GAMBO WAIBUKIA BUNGENI

MAREGESI PAUL-DODOMA Na JANETH MUSHI -ARUSHA


MZIMU wa fedha za rambirambi zilizotokana na msiba wa wanafunzi 33 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya Arusha hatimaye umetua bungeni baada ya kuripotiwa sehemu ya fedha hizo zitatumika kukarabati Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Agizo la baadhi ya fedha hizo kukarabati hospitali linadaiwa lilitolewa na  Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo,     jambo lililowafanya baadhi ya wazazi ambao walikuwa wajumbe wa kamati  ya matumizi ya fedha za rambirambi, kujitoa.

Jana, akizungumza bungeni,  Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alisema haridhishwi na uamuzi wa Serikali ya Mkoa wa Arusha kubadili matumizi ya fedha za rambirambi zilizochangwa na watu mbalimbali kwa ajili ya wafiwa wa wanafunzi, walimu na dereva wa basi la Shule Msingi, Luck Vincent ya   Arusha.

Alisema   taarifa za mabadiliko ya matumizi ya fedha hizo zilizoripotiwa jana na Gazeti la MTANZANIA, zinawakatisha tamaa wanaotoa misaada kwa wanaopatwa na matatizo.

Waitara aliyasema hayo   alipokuwa akiomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa hapo nje na nimeangalia Gazeti la MTANZANIA la leo (jana), linaelezea  mabadiliko ya matumizi yaliyofanywa katika fedha za rambirambi za Shule ya Msingi Lucky Vicent, kwamba fedha zile zimeenda kufanya kazi nyingine.

“Katika gazeti hilo, wanasema fedha z nyingine zimekwenda kuwalipa posho madaktari na nyingine zimeenda kwenye matibabu ya wale watoto. Pili, wanasema fedha nyingine zinaenda kujenga hospitali badala ya kwenda kwa waathirika waliokusudiwa.

“Hizi fedha kwa kweli Bunge linahusika nazo kwa sababu tulikatwa posho kwa maana ya kutoa rambirambi kwa wahusika.

“Pamoja na hilo, imekuwa ni tabia inayojirudiarudia mara kwa mara, yaani fedha zinachangwa kwa ajili ya rambirambi, baadaye Serikali inazipangia matumizi mengine kitu ambacho kinatukwaza sana hasa mimi mwenyewe.

“Kama tutakuwa tunachangishana fedha hapa halafu wanakwenda kufanya matumizi ya kulipana posho ni afadhali kila chama humu ndani au kada fulani iwe inachangia yenyewe kuliko hii tabia inayoendelea.

“Kwa hiyo, naomba mwongozo wako kwa sababu hii si sahihi, fedha zinachangwa kwa ajili ya rambirambi halafu zinabadilishwa juu kwa juu bila kupelekewa wahusika,” alisema Waitara.

Akitoa mwongozo wake, Chenge alisema Bunge haliendeshwi kwa kutumia magazeti na kwamba mtu anapotoa rambirambi hatakiwi kufuatilia matumizi ya rambirambi hizo

“Sisi humu bungeni hatuendeshwi kwa magazeti. Lakini pia kwa mila zetu, ukishatoa mchango wako wa rambirambi, unaiachia familia ile au chombo kile kifanye kinavyoona inafaa.

“Kwa maoni yangu naomba tusiendeleze hayo ingawa hapa bungeni Serikali ipo, Bunge lipo na uongozi wa Bunge upo pia.

“Kwa hiyo tunategemea mrejesho kwa michango ya Bunge ili siku za usoni mtakapokuja kuombwa kuchangia, muwe na uhiyari wa kuitikia.

“Hivyo basi, kuanza kuleta tuhuma kwamba fedha hazijaenda huko, mimi nasema kidogo ni tatizo. Hilo halijatokea bungeni, umesoma huko kwenye magazeti yako naomba liishie huko,” alisema Chenge.

Mwanzoni mwezi huu, wanafunzi 35, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Msingi, Luck Vincent ya  Arusha, walifariki dunia kwa ajali ya basi walipokuwa wakienda wilayani Karatu mkoani humo, kufanya mtihani wa ujirani mwema katika Shule ya Msingi Tumaini.

Pamoja na vifo hivyo, wanafunzi watatu walionusurika, walisafirishwa wiki iliyopita kwenda   Marekani kwa matibabu zaidi baada ya afya zao kuonekana kudorora   walipokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mount Meru,  Arusha.

Kutokana na ajali hiyo, watu na taasisi mbalimbali nchini, walitoa rambirambi za zaidi ya Sh milioni 300 zikiwamo Sh milioni 100 zilizotolewa na wabunge kwa kukatwa posho zao za siku moja, pamoja na ofisi ya Bunge.

Polisi na mil. 18/-

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeendelea kuzishikilia Sh milioni 18 za rambirambi zilizochangwa na Shirikisho la Wenye Shule na Vyuo Binafsi  Tanzania (TAMONGSCO).

Rambirambi hizo zilikuwa zikabidhiwe Alhamisi iliyopita  lakini ilishindikana baada ya polisi kuvamia kikao cha makabidhiano ya rambirambi hizo kwa wazazi na walezi waliopoteza watoto wao katika ajali hiyo ya hivi karibuni Kata ya Rhotia wilayani Karatu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha, Yusufu Ilembo, alithibitisha kuwa amri ya kuwakamata viongozi hao na waandishi wa habari wakitekeleza majukumu yao lilikuwa  ni agizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Viongozi hao walikamatwa Alhamisi iliyopita na kushikiliwa  na polisi kwa siku mbili baada ya kukamatwa katika shule ya Msingi ya Lucky Vincent ambayo katika ajali hiyo ilipoteza wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja.  

Kuendelea kushikiliwa   fedha hizo kulielezwa jana   wakati   viongozi   hao walipoenda kuripoti kituoni hapo kama walivyotakiwa na jeshi hilo Jumamosi walipoachiwa.

Viongozi hao waliripoti kituoni hapo jana   saa 3.00 asubuhi na  wote wanatakiwa kurudi kituoni hapo Ijumaa.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa asingeweza  kulizungumzia suala hilo.

Alisema halifahamu kwa sababu alikuwa nje ya ofisi wakati tukio hilo linatokea lakini aliahidi kulifuatilia.

“Siwezi kuzungumzia kitu ambacho sikifahamu, siwezi kujibu kitu ambacho sijakifahamu bado, sijui kama kuna watu walikamatwa na hela. Ukishtakiwa ukapelelezwa ukagundulika huna kosa unarudishiwa mali yako.

“Hata kama una kosa ukashitakiwa mahakamani lakini mali yako unarudishiwa kama siyo 'part and parcel’ ya kesi unayoshitakiwa nayo.

“Kama hiyo mali ilikamatwa haiwezi tena kuendelea kuwa mikononi mwa polisi kama mwenye nacho ameachiwa anapewa mali anaondoka,”  alisema Mkumbo.

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,   Gambo , alidaiwa kuita wazazi wafiwa akiwataka wakubali Sh milioni 56 zielekezwe katika mambo matatu kuboresha wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), kujenga Kitengo cha magonjwa ya akili au kuboresha chumba cha kuhifadhia maiti, Hospitali ya Mount Meru.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles