Aziza Masoud na Neema Bariki (TSJ), Dar es Salaam
TAASISI ya Kiislamu ya Hawzat Imam Saadiq, inatarajia kufanya maandamano kesho jijini Dar es Salaam ya kupinga mauaji yanayotokea katika mji wa Gaza nchini Palestina.
Maandamano hayo yatakayoanzia Ilala Boma na kuishia katika uwanja wa mpira wa ‘Peoples’ uliopo Kigogo, yanatarajiwa kupokelewa na viongozi wa kidini, wahadhiri wa vyuo vikuu na Balozi wa Palestina nchini, Nasri Abu Jaish.
Akizungumza jijini jana, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sheikh Abdul Sharif, alisema maandamano hayo yatafanyika kesho kuanzia saa tatu asubuhi ambapo siku hiyo taasisi hiyo itakabidhi tamko linaloelezea machafuko hayo na kupinga tamko lao kwa mgeni rasmi.
“Maandamano haya yana lengo la kuwaamsha Watanzania ili kuangalia matatizo yanayotokea nchi nyingine na kujifunza ili yasije yakatokea na nchini,” alisema Sheikh Sharif.
Alisema wananchi wa Gaza kwa sasa wanaishi kwa kuzudhulumiwa haki zao hivyo basi jitihada zinahitajika katika kuwaokoa na tatizo hilo.
Alisema jumuiya ya kimataifa imekuwa ikishughulikia mambo hayo kidiplomasia hali ambayo haisaidii kutatua matatizo yaliyopo.