24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

UNYAMA…

gazeti la Mtanzania
gazeti la Mtanzania

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu cha Kimataifa Matibabu na Teknolojia (IMTU) kilichopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam ndicho kinahusika na tukio la kinyama la kuichuna, kuikatakata, kuikausha na kisha kuitupa miili ya binadamu kwenye Bonde la Mbweni Mpiji, lililopo Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo awali gazeti hili lilizipata na kuthibitishwa na polisi pamoja na uongozi wa chuo hicho ni kwamba, chuo hicho ndicho kinahusika na sakata hilo na kwamba tayari baadhi ya viongozi wa chuo wameshakamatwa na Jeshi la Polisi.

Jana gazeti hili liliandika taarifa iliyoelezea tukio hilo kubainika baada ya akina mama wanaofanya kazi ya kuponda kokoto kwenye eneo hilo kufungua baadhi ya mifuko hiyo iliyokuwa imetupwa na watu wasiojulikana.

Mashuhuda wa tukio hilo walilieleza gazeti hili kwamba, viungo hivyo vya binadamu vilitupwa Julai 20, mwaka huu, lakini hakuna aliyegundua kutokana na kukaushwa na kupulizwa dawa iliyovizuia kutoa harufu.

UONGOZI WA CHUO WAKIRI

Ofisa Rasilimali watu wa Chuo hicho, Michael Lazaro, alikiri chuo chao kuhusika kwenye tukio hilo, lakini alishindwa kufafanua kwa kina ni kwanini walifanya hivyo, ambapo alisema kitengo cha maabara kinachohusika na uchunguzi na utafiti wa viungo vya binadamu ndicho kinahusika moja kwa moja na tukio hilo.

Lazaro alisema kwa mujibu wa taratibu za chuo, mabaki ya tafiti na chunguzi hizo huwa yanachomwa kwenye tanuru maalumu la kuchomea kemikali, lililopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo anashindwa kufahamu ni kwanini kitengo hicho kilikwenda kutupa taka hizo porini bila kutoa taarifa za kwanini hawakupeleka mabaki hayo Muhimbili.

Alipoulizwa ni wapi wanatoa miili hiyo, Lazaro alisema mtu pekee ambaye angeweza kutoa ufafanuzi wa kina wa wapi inatoka miili hiyo ni Mkuu wa kitengo hicho, anayefahamika kwa jina la Dimesh Kumaar, ambaye anashikiliwa na polisi.

Alipotakiwa kutupeleka kwa Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Prabhakar Rao ili kuelezea sakata hilo, Lazaro alisema bosi wake huyo ni mgeni nchini, lakini pia naye ni mmoja wa viongozi wa chuo waliokamatwa na Jeshi la Polisi.

MADUDU YA CHUO YAIBULIWA

Baada ya tukio hilo, kumeibuka madudu mengi yanayokihusisha chuo hicho na sakata la kutupa viungo vya binadamu, ambapo mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho alisema uongozi wa chuo hicho umekuwa na matatizo na kwamba sakata kama hilo liliwahi kutokea miaka ya nyuma, ambapo kuna mwanafunzi wa chuo hicho alionekana akiwa na mkono wa binadamu mtaani kitendo ambacho hakiruhusiwi.

Mtoa habari wetu alisema kuwa muhula wa kwanza wa masomo ulimaliza kutumia miili hiyo mwezi Machi mwaka huu na uongozi ulitakiwa kuiteketeza, lakini walishindwa kutokana na kifaa cha kuteketeza mabaki hayo kuharibika, ambapo waliomba msaada Muhimbili, huko nako waliambiwa kifaa kimeharibika.

Katika kuhakikisha wanaviteketeza inadaiwa waliomba msaada kwenye maeneo mbalimbali, ambapo walitakiwa kutoa fedha ili kazi hiyo ikamilike, lakini walishindwa kutoa fedha badala yake wakaamua kwenda kuitupa bondeni.

Alisema kuwa hatua hiyo ilifikiwa ili kuwahadaa wajumbe waliokuwa kwenye msafara wa Umoja wa Vyuo vya Madaktari Afrika, ambao kama wangekutana na mabaki hayo ni wazi wangepoteza sifa.

MUHIMBILI WAZUNGUMZA

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminieli Eligaesha, alikiri kuharibika kwa mtambo wa kuteketeza mabaki hayo hata hivyo alikanusha uvumi wa kwamba viungo hivyo vimetoka hospitalini hapo.

Eligaesha alisema kifaa hicho kimeharibika tangu mwezi Februari mwaka huu na kwamba waliagiza kifaa kingine kutoka nje ya nchi ambacho baada ya kuunganishwa kifaa kingine kiliharibika.

“Kawaida huwa tunaagiza vifaa vya mitambo yetu kutoka nje ya nchi, lakini tulipounganisha kuna kifaa kingine kiliharibika na ndiyo maana hadi sasa ndugu waandishi mmeshuhudia mafundi wakiendelea kuutengeneza mtambo huo na kwa mujibu wao utakuwa tayari hivi karibuni,” alifafanua Eligaesha.

JESHI LA POLISI LAUNDA JOPO LA UCHUNGUZI

Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeunda jopo la upelelezi la watu saba linaloongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Japhari Mohamed.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema jopo hilo limeshaanza uchunguzi mara baada ya kupata taarifa hizo kwa kushirikiana na Daktari wa Jeshi la Polisi ambaye anahusika na uchunguzi wa miili ya binadamu pamoja na madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Kova alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kwa mara ya mwisho viungo hivyo vilikuwa katika maabara ya Chuo Kikuu cha Madaktari cha International Medical and Technological University (IMTU) kilichopo jijini Dar es Salaam ambacho pia hufanya mafunzo ya udaktari kwa vitendo.

Alisema jeshi hilo tayari linawashikilia watu wanane kwa mahojiano kutokana na utupwaji wa viungo hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema viungo hivyo vilipatikana jana katika eneo hilo vikiwa katika mifuko mieusi ya plastiki ipatayo 85.

Alisema kati ya watu wanane waliokamatwa wengine ni madaktari pamoja na wale waliohusika katika utekelezaji wa tukio hilo na wamewahoji na kukiri kuhusika.

“Miongoni mwa maswali tutakayoendelea kuwahoji ni pamoja na sababu ya wingi wa viungo hivyo na kwanini walienda kuvitupa katika eneo lile la wazi ambalo watu wengi hupita.

“Ili kufanikisha upelelezi wetu, tutamshirikisha Mkemia Mkuu wa Serikali ili aweze kufanya uchunguzi wa kina ikiwamo kubaini viungo hivyo ni vya muda gani kwa kutumia vinasaba (DNA), pia itabainika kuwa ni vya watu wangapi.

“Baada ya uchunguzi kukamilika jalada hilo litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua za kisheria zaidi zichukuliwe dhidi ya wahusika pamoja na kujua kuwa ni sheria gani  zimevunjwa katika kulinda viungo vya binadamu,” alisema Kova.

MAITI ZINAVYOPATIKANA

Wataalamu wa afya wameeleza namna miili hiyo inavyopatikana na kutunzwa kwa ajili ya mafunzo.

Wamesema kuwa miili hiyo hupatikana kutokana na maiti ambazo zimekaa kwa kati ya miezi sita mpaka mwaka bila kutambuliwa na ndugu zao.

Walisema miili hiyo hutoka katika nchi mbalimbali na kwamba nchi moja ikiwa na shehena ya maiti hutafuta nchi nyingine iliyo mbali ili kubadilishana miili hiyo.

“Kwa mfano Tanzania inaweza kubadilishana miili hii na nchi nyingine iliyo Afrika Magharibi, vinapofika vyuoni huwekwa kwenye maabara maalumu, jambo hili hufanyika kwa umakini sana, haijawahi kutokea mtu aliyeenda kusomea fani ya tiba akakutana na mwili wa ndugu yake ama rafiki yake,” alisema Dk. Samwel Shita.

Dk. Shita ambaye ni mtaalamu wa tiba, anasema miili hiyo hujulikana kitaalamu kama cadaver na hutumiwa na wanafunzi wa vyuo vya tiba, lengo likiwa ni kuifanyia upasuaji ili kujifunza maumbile ya mwili mzima wa binadamu.

Anasema kuwa miili hiyo inaweza kuwa ni ile iliyokosa ndugu wa kuizika na pia baadhi ya watu hujitolea na kuandika kimaandishi kuwa pindi wakifariki miili yao itumike kwa ajili ya mafunzo.

Anasema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo hupendekeza namna ya kuhifadhiwa kwake, maiti hizo huhifadhiwa kwa kipindi cha miezi sita mpaka mwaka mmoja kisha kukabidhiwa kwa wataalamu wa afya ambao huzitunza na kuziwekea dawa maalumu ili zisiharibike wala kuguswa na bakteria wa aina yoyote.

Dawa hiyo inajulikana kama 2-phenoxethanol maarufu kama fomulani. Anasema kuwa dawa hii huingizwa katika mshipa mkubwa wa paja na kisha huenea sehemu yote ya mwili kupitia mfumo wa mishipa ya damu.

Anasema kuwa dawa hiyo huweza kuutunza mwili huo kwa muda mrefu na kuwa hakuna vijidudu vinavyoweza kuugusa na hata ukiwekwa sehemu ya wazi hakuna ndege wala mnyama atakayeweza kuugusa.

“Si kunguru, bakteria au fangasi au kiumbe chochote kinachoweza kuugusa au kuishi kwenye mwili uliowekwa dawa hii,” alisema Dk. Shita.

Alisema kuwa dawa hiyo inatambulika kama moja ya kemikali zinazoweza kusababisha saratani kama mtu atakumbana nayo kwa muda mrefu.

Dawa hii huweza kuwa na harufu kali na inayokera, ina ukakasi na pia huwa rahisi kuwa kama mvuke ambao mtu akiuvuta hupata shida kupumua.

Baada ya mwili huu kutengenezwa, huifadhiwa katika vyombo maalumu vilivyojaa dawa ya maji ya fomulani mpaka pale itakapohitajika.

Dk. Shita anaeleza kuwa mwili wa binadamu umefunikwa kwa ngozi ambayo huwa ni ngumu, hivyo hulazimu watu wanaojifunzia miili hiyo kutenganisha ngozi kwa kuichuna ili kuweza kuona sehemu za mwanzo ambazo huwa na tishu laini kama kitambaa na sehemu hizo huitwa farcia.

Pia huweza kuonyesha mishipa ya damu kwa juu, mishipa ya fahamu ilivyogawanyika katika tishu, misuli ya mwili pamoja na viungo vingine.

Anasema kuwa ni vigumu kuzifikia sehemu hizo bila kuchuna ngozi.

Anasema kuwa dawa ya fomulani husababisha athari mbalimbali katika mfumo wa hewa, mfumo wa fahamu na ngozi.

Alisema kuwa dawa hiyo ndiyo inayonyima kiumbe chochote kuweza kuishi.

Wakati Dk. Shita akieleza namna miili hiyo inavyopatikana na kutunzwa, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Tiba cha Bugando, Dk. Rodrick Kabangila, anasema hata kama miili hiyo ilitumika kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa tiba, kuitupa porini kunaonyesha namna mamlaka zinazosimamia fani hiyo zilivyoshindwa kufanya kazi.

“Mimi nilivyoona hiyo shehena nilikuwa na mambo mawili ya kujiuliza, kwanza niliona yawezekana yametoka hospitali ama kwenye vyuo vya tiba ambapo wanafunzi hutumia kujifunzia.

Lakini ukiangalia hata kama imetoka kwenye vyuo huwa kuna namna ya kuihifadhi kazi yake ikiisha. Nilivyoona zile ngozi zilivyokuwa nyingi nikasema ni vigumu zikawa zimetoka hospitali kwa sababu kule huwa wanachukua ngozi kidogo tu kwa sababu ya kuziweka kwenye sehemu nyingine ya mwili,” alisema Dk. Kabangila.

Alisema kuwa tangu miaka ya 1970 madaktari wamekuwa wakifundishwa na hakuna tukio kama hili, hivyo yawezekana kilichofanyika ni hujuma ama waliopewa kuteketeza mzigo huo walitaka kwenda kuuza.

“Yawezekana watu walikula hela ama ni mtu alikuwa amepatana na mtu mwingine ampelekee huo mzigo wakashindwa kuelewana bei ndiyo wakaenda kuutupa huko,” alisema.

Alisema kuwa katika kufundisha wanafunzi wa udaktari, ni suala la kawaida kuchuna ngozi ya sehemu moja ili kujua mishipa ya damu imepita wapi, ikoje, misuli imepita wapi na ikoje.

Habari hii imeandaliwa na Asifiwe George, Veronica Romwald, Deonidas Mukebezi na Jonas Mushi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles