LONDON, ENGLAND
KIUNGO wa timu ya Manchester United, Nemanja Matic, amesema kikosi chao kilikosa kiongozi ndani ya uwanja wakati kikishushiwa kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park.
Lakini Manchester United bado ina matumaini ya kutinga nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, licha ya kipigo hicho cha mabao kutoka kwa Richarlison, Gylfi Sigurdsson, Lucas Digne na Theo Walcott.
Manchester United imepoteza michezo sita kati ya minane kwenye michuano yote tangu ifanye vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG mwezi uliopita.
Matic anakiri kwamba anastahili lawama kutokana na kucheza chini ya kiwango akiwa miongoni mwa wachezaji wachache wenye uzoefu ndani ya kikosi cha timu hiyo.
“Nafikiri mambo hayakwenda kama tulivyotarajia leo (juzi).
“Tulijiandaa na mchezo kama ambavyo tunafanya kila siku. Benchi la ufundi lilituonyesha kila eneo ambalo Everton wangekuwa hatari kwetu lakini nafikiri tatizo kubwa hatukuwa na kiongozi ndani ya uwanja leo.
“Mimi ni mchezaji mzoefu kwenye timu, hivyo kama hatukufanya vizuri eneo la kiungo inakuwa ngumu wachezaji wengine kucheza. Na kama kuna mtu anatakiwa kulaumiwa, basi nitakuwa wa kwanza.
“Nafikiria vitu vingi, lakini ni jambo jema kuwa na utulivu wa akili ya ushindi ndani ya chumba cha kubadili nguo.
“Ni rahisi kusema kwamba ukishinda unakuwa na utulivu wa akili, lakini wakati ukipoteza watu wanataka kufahamu tatizo na nina uhakika watachambua kila kitu na watapata njia sahihi ya kutatua tatizo,” alisema Matic.
Manchester United inakabiliwa na kibarua kingine kigumu dhidi ya Manchester City ambao wapo kwenye mbio za ubingwa msimu huu.
Matic anaamini kuwa Manchester United itacheza kwa jihadi kushinda mchezo huo.
“Aina hii ya mchezo nafikiri tutakuwa na hali ya ushindi. Kwenye mchezo huu si tatizo kwa timu yetu kutafuta hali ya ushindi.
“Tatizo wakati unacheza dhidi ya timu ambayo siwezi sema ndogo lakini haipo kwenye nafasi sita za juu ya msimu wa ligi. Pia msimu uliopita tulikuwa kwenye tatizo kama hili dhidi ya timu iliyokuwa katikati ya msimamo wa ligi ambayo ilikuwa ikitafuta kuepuka kushuka daraja,” alisema Matic.
Baada ya kupoteza mchezo huo, Manchester United imebaki nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, huku ikiwa imepitwa pointi mbili dhidi ya Arsenal ambayo ipo nafasi ya nne.
Michezo mingine iliyobaki kwa Manchester United ni dhidi ya Chelsea, Huddersfield na Cardiff.