NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM
MATIBABU kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi yapo shakani kutokana na kupungua kwa vifaa vya kusaidia matibabu yao.
Kwa sababu hiyo, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) inaomba wahisani kujitokeza kuisadia vifaa hivyo vijulikanavyo kama shanty, kwa ajili ya kutolea maji yaliyomo kichwani hadi tumboni kwa njia ya kawaida.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Taasisi hiyo, Almas Jumaa alisema mahitaji ya shanti ni makubwa kwa watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.
“Vifaa hivi vina bei sana kwa wazazi wanaotoka mikoani hawawezi kuvinunua kwa vile shanti moja inauzwa kati ya Sh 150,000 hadi Sh 120,000 ambayo hutegemea duka la dawa ambalo huenda kununua,”alisema Jumaa.
Wodi ya watoto wenye vichwa vikubwa hulaza watoto 50 ambao kama watafanyiwa upasuaji, shanti zilizopo haziwezi kutosheleza.
Jumaa alisema shanti moja inaokoa maisha ya mtoto mmoja hivyo kama jamii itajitokeza kusaidia shanti 10 na kuendelea maisha ya watoto wengi yanaweza kuokolewa.
Wakati huohuo, Jumaa alisema kwa sasa taasisi hiyo, haijaelemewa na wagonjwa kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita.
Alisema hadi jana wagonjwa waliokuwa wamelazwa ni 304 ambako kuna vitanda 340 huku kukiwa na upungufu mkubwa wa wagonjwa.