24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyetaka kuwalipua polisi kwa bomu auawa  

Kamanda-wa-Polisi-Mkoa-wa-TangaNA OSCAR ASSENGA, TANGA

MTU mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30, ameuawa baada kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali.

Mtu huyo, ameuawa baada ya kutoa vitisho vya kuwalipua kwa bomu askari polisi waliokuwa wakitaka kumkamata.

Mtu huyo ambaye jina lake halikufahamika, alikuwa anasakwa na polisi kwa madai ya kuhusika na tukio la mauaji ya watu watano katika duka la Central Bakery Aprili 20, mwaka huu.

Akizungumzia na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul, alisema tukio hilo lilitokea Mei 9, mwaka huu saa 2 usiku katika eneo la Makorora jijini hapa.

Alisema wakati polisi wakimfuatilia, alishtuka na kuwatolea bomu la kurusha kwa mkono ambalo

lina uwezo wa kusababisha mlipuko na kuleta athari kwa zaidi ya umbali wa mita 50.

Kamanda Paul alisema katika purukushani hizo, mtuhumiwa alishindwa kulilipua na kujikuta akiliangusha chini.

Alisema baada kuliangusha, mtuhumiwa alianza kukimbia, ndipo wananchi walipoanza kumtupia vitu vizito, yakiwamo mawe na vyuma eneo la kisogoni.

“Wakati anakimbia wananchi walianza kumtupia vitu vyenye ncha kali, matokeo yake alianza kuvuja damu na kuishiwa nguvu, polisi

wakamkamata, lakini wakati akiwa njiani anapelekwa hospitali alifariki dunia,” alisema Kamanda Paulo.

Wakati huo huo, mwanafunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) Kikosi cha Anga kilichopo eneo la Kange, MT 81627 Koplo Freddy Philip (28) amefariki dunia, baada ya kujipiga risasi kichwani akiwa lindo.

Kamanda Paul alisema tukio hilo limetokea Mei 9, mwaka huu saa 1.15 usiku.

Alisema wakati Koplo Philip akiwa lindo, alichukua uamuzi huo, bila kushirikisha wenzake.

“Kijana huyu alijipiga risasi kichwani wakati akiwa lindo, chanzo cha mauaji hayo hakijafamika, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Kamanda Paul.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles