31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Matatani kwa kumzuia mtoto wake asifanye mitihani darasa la saba

Gurian Adolf -Nkasi

MKAZI wa Kijiji cha Paramawe kata Wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Luvinza Kasakwa(55) amefikishwa polisi kwa tuhuma za kumzuia binti yake asifanye mitihani ya kumaliza darasa la saba ili amuozeshe apate  mahali.

Mzazi huyo wa mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Paramawe alikamatwa baada ya mtoto wake  huyo kutofika kufanya mitihani kwa madai kuwa amezuiliwa na mzazi wake.

Akizungumza na na mwandishi wa gazeti hili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Missana Kwangula amekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa ni la kusikitisha hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inatoa  elimu bila malipo ili watoto wote wapate elimu bila vikwazo.

Akisimulia undani wa tukio hilo, Mkurugenzi huyo alisema Septemba 12 ambayo ilikuwa siku ya kwanza  ya wanafunzi wa darasa la saba  kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi  nchini,  mwanafunzi huyo hakuonekana katika chumba cha mtihani katika shule ya msingi Paramawe.

“Mtihaniwa kwanza ulikuwa wa somo la Kiingereza  lakini msichana huyo hakuwepo kwenye chumba cha mtihani, msimamzi wa mtihani shuleni hapo alitoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ambaye aliwasiliana na baba wa mwanafunzi huyo ambaye alidai kuwa binti yake alikuwa mgonjwa,”  alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kushawishiwa  kwa simu alikubali kumpeleka binti yake huyo shuleni, lakini alipofika hakuonekana mgonjwa  hivyo aliamriwa kuingia kwenye chumba cha mtihani lakini alikuwa amechelewa na kushindwa kufanya mtihani wa somo la Kiingireza .

Aliongeza kuwa baba mzazi wa mwanafunzi huyo alikamatwa na kushikiliwa katika kituo cha polisi kilichopo katika Kata ya Paramawe  kabla ya kuhamishiwa wilayani ili kusubiri mtoto wake  amalize mitihani yake na kuendelea na upelelezi kujua kilichosababisha mwanafunzi kutofika shuleni kufanya mitihani hadi alipolazimishwa.

“Japo hatuna ushahidi wa moja kwa moja lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa baba mzazi  wa msichana huyo  alikuwa na nia ovu ya kusababisha binti yake asifanye mitihani ili amuozeshe, uzuri ni kwamba katika kijiji cha Paramawe kipo Kituo cha polisi ambapo uchunguzi unaendelea” alisema Kwangula.

Diwani wa Kata ya Paramawe, Wilbroad Kakui akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema kuwa msichana huyo alipohojiwa alikiri kuwa hakuwa mgonjwa bali baba yake alimkataza asiende kufanya mitihani na akienda ahakikishe anafanya vibaya ili asifaulu kwani ana lengo la kumuozesha.

Kakui alisema kuwa hata hivyo  siku ya mtihani alimzuia asiende shule kufanya mitihani hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles