30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Matapeli ‘wamliza’ Mwigulu

NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, ameeleza jinsi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba alivyotapeliwa na vishoka wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Kutokana na hali hiyo, waziri huyo ametoa siku 14 kwa wakala huo kujitathmini na kujisafisha na akatahadharisha kuwa hatosita kuchukua hatua kwa atakayeshindwa kwenda na kasi anayoitaka.

Akizungumza Dares Salaam jana baada ya kutembelea Brela, alisema ndani ya wiki mbili amefanya hivyo mara mbili kwa sababu kuna malala miko mengi kuhusu huduma zinazotolewa huku mengine yakiwasilishwa moja kwa moja kwa Rais Joseph Magufuli.

Alisema miongoni mwa malalamiko hayo ni uwepo wa vishoka ambao wamekuwa wakiwatapeli watu fedha pindi wanapohitaji kupata huduma zinazotolewa na wakala huo.

“Hivi ninyi Brela kwanini hamna wivu wa kulinda taasisi yenu, sasa wale mnaowakamata (akimaanisha vishoka) na kuwaacha inaonekana mnanufaika nao.

“Kuna watuwana ofisi chini (kwenye jengo la Ushirika), wanadai wanawasaidia wananchi wanawatoza hadi Sh milioni tatu,” alisema Kakunda.

Alisema Mwigulu ni miongoni mwa watu waliotapeliwa na vishoka hao na kujikuta akiwatumia fedha mara kadhaa.

“Yuko mmoja amemsumbua Mwigulu Nchemba kila wiki anapata fedha, anamwambia jamaa wa Brela wanataka fedha, hadi jana (juzi) Mwigulu akaamua kunipigia, sasa huyo atafutwe hadi apatikane,” alisema.

Waziri huyo alisema kuna malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara ambayo yanachangiwa na udhaifu mkubwa ulioko kwenye mifumo kuliko uhalisia.

“Malalamiko yanayofika kwa Rais kila siku hayapungui mawili, wafanyabiashara wanamlalamikia na kuna wakati anasema hii Brela tuifute.

“Kati ya simu10 ninazopokea kutoka kwa wafanyabiashara wanane zinalalamikia Brela hili ni tatizo. Brela ingekuwa iko ‘perfect’ nisingekuja, nimekuja kwa sababu kuna matatizo,” alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, ndani ya siku 14 yaani kuanzia jana hadi Desemba 31, mitambo yote ya wakala huo ikaguliwe ili penye udhaifu pajulikane na kushughulikiwa.

“Kama mitambo haina uwezo waiteni walioifunga waibadilishe, mkivumilia mapungufu tutaelewa kwamba mlipata mshiko.

“Sheria ya Manunuzi inaelekeza mitambo isipokelewe kama haijafanyiwa ‘training’ (mafunzo) yakutosha, sasa mnaniambia training bado hii ni hatari, maana yake hamkuzingatia sheria,” alisema.

Kuhusu tovuti, alitoa siku saba kwa wakala huo kuisafisha kwani ina mkanganyiko wa taarifa kwani inaeleza kwa mgeni anatakiwa awe na namba ya hati ya kusafiria na namba ya kitambulisho cha taifa wakati hicho kinatolewa kwa Mtanzania tu.

Waziri huyo pia alimtaka Mtendaji Mkuu wa Brela, Emmanuel Kakwezi, kukunjua makucha kwani wizara kwa asilimia 80 haiwezi kufanya vizuri kama wakala huo haufanyi vizuri.

“Hali ya biashara si nzuri kulingana na changamoto tunazokutana nazo, fanyeni kila njia kurekebisha hali hii. Hatutakuwa na urafiki na mtu anayekimbiza mitaji na ajira za Watanzania.

“Mimi sikuota kama nitateuliwa kuwa waziri, rais aliamini akiniweka nitamsaidia, sasa akiniandikia sms (ujumbe mfupi) kuna tatizo nisiposhughulikia je, ataona nafaa kumsaidia?

“Haiwezekani nakaa ofisini napata malalamiko kutoka kwa mkandarasi aliyeko Kalambo (mkoani Rukwa), hiki si kitu kizuri. Tunaonekana Watanzania tuko nyuma kiviwango. 

“Ni mambo ambayo yanatia hasira naomba Kakwezi (Mtendaji Mkuu Brela) uanze kuwa mkali. Mkichafuka wote tutawashughulikia, msiache mambo yanayochafua ‘image’ (taswira) ya taasisi yaendelee,” alisema Kakunda.

Naye Kakwezi alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa upungufu wa watumishi 51 huku vibali vya ajira vikichukua muda mrefu.

“Mtandao wa ORS ni mzuri unasaidia kuhakikisha tunasajili makampuni na huduma nyingine, lakini kuna changamoto ya mfumo kutokuwa imara.

“Katikati ya kazi unaweza kuzimika, mteja anatuma maombi lakini hayaonekani na sisi tunawezakumjibu lakini haoni,” alisema Kakwezi.

Alisema wameongeza watumishi wa kujitolea na muda wa kufanya kazi hadi saa 12 jioni nakuweka dirisha maalumu katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) zilizopo wilayani ili kurahisisha shughuli za usajili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles