29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MASWALI MSAMAHA WA MBUNGE SUGU

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) na Katibu wa Kanda ya Nyasa wa chama hicho, Emmanuel Masonga wameachiwa huru.

Mbilinyi ambaye ni maarufu kwa jina la Sugu, aliachiwa na mwenzake huyo jana baada ya kukaa gerezani kwa siku 73 katika Gereza la Mkoa wa Mbeya, Ruanda.

Februari 26 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Mbeya, iliwahukumu Sugu na Masonga kwenda jela kutumikia kifungo cha miezi mitano kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wanasiasa hao walikata rufaa, lakini hadi wanaachiwa huru jana, rufaa yao ilikuwa haijasikilizwa.

Akizungumzia kuachiwa kwa viongozi hao, Mkuu wa Magereza la Ruanda na Songwe, Paul Kijida, alisema wanasiasa hao waliachiwa kutokana na msamaha wa Rais Dk. John Magufuli, alioutoa April 26, mwaka huu, wakati wa maadhimisho ya sherehe za muungano.

Kwa mujibu wa Kijida, mfungwa ambaye anatumikia kifungo ambacho hakihusiani na jinai, gereza humuondolea moja ya tatu ya adhabu anayotumikia.

Kutokana na hali hiyo, Kijida alisema Sugu na Masonga, wanahusika na msamaha huo kwa kuwa walitakiwa kumaliza adhabu zao Juni 5, mwaka huu.

“Wakati wafungwa hao wakitumikia kifungo hicho, Aprili 26, mwaka huu, Rais alitoa msamaha kwa wafungwa nchini na wanaofaidika ni wale wote ambao wamebakiza muda mchache gerezani.

“Kwa hiyo, ukiangalia mbunge huyo pamoja na mwenzake, walikuwa wamebakiza muda mchache na hivyo kuguswa moja kwa moja na msamaha huo.

“Pamoja na hayo, baadhi ya watu wameanza kuhoji ni kwanini watuhumiwa hao wamechelewa kutoka gerezani baada ya msamaha wa Rais wa Aprili 26.

“Ieleweke kwamba, msamaha wa Rais hubeba robo tatu ya adhabu ya mfungwa na hesabu hupigwa siku ile ya tarehe husika ambayo Rais ametoa msamaha.

“Kwa hiyo, baada ya ofisi kupiga hesabu za kifungo cha mbunge na mwenzake, tarehe ya kuachiwa huru iliangukia Mei 5, mwaka huu na ndiyo leo tumewaachia. Lakini pia, wananchi waelewe kwamba walioachiwa siyo hao tu bali wengine wataendelea kutoka.

“Kwa ujumla, msamaha unapotolewa, kuna taratibu na sheria za gereza lazima zifanyike na hufanywa kwa wafungwa wote ambao majina yao yamebahatika kuingia kwenye orodha ya kusamehewa.

“Eleweni pia kwamba mfungwa anapoachiwa huru, magereza yanagharamia nauli, lakini kwa kuwa mbunge na mwenzake walitueleza nyumbani kwao, basi badala ya kuwapa nauli, ofisi ikaona ni vema ikawasafirisha kwa kutumia usafiri wetu na hili si kosa,”alisema mkuu huyo wa magereza.

Wakati mkuu huyo wa magereza akisema hayo, Sugu alisema hajui ni kwanini wameachiwa huru.

“Tuliingia gerezani kwa utata na leo tunatoka kwa utata. Lakini, naomba kuueleza umma, kwamba mateso na manyanyaso haya tuliyoyapata yatalipwa mwaka 2020, kwa sasa tunyamaze tu.

“Pamoja na hayo, nampa pole mama yangu mzazi ambaye anaumwa na amepitia katika kipindi kigumu wakati nilipokuwa gerezani.

“Pia, nawashukuru wananchi, baraza la madiwani, ndugu na marafiki zangu waliokuwa bega kwa bega na sisi wakati wote tulipokuwa gerezani.

“Huko gerezani wafungwa wenzagu walitupatia ushirikiano wa kutosha kiasi kwamba siasa zilikuwa zikiendelea kwani mimi nilikuwa mfungwa wa kisiasa.

“Mule ndani kulikuwa kama kajimbo kadogo, tulikaa vizuri na wenzetu, wana mengi sana, lakini kubwa lililopo ni ukosefu wa sare kwani wapo wafungwa wanaotembea nusu uchi kutokana na uchakavu wa mavazi wanayoyatumia.

“Mengine nitayazungumza bungeni, ila nawashukuru askari magereza kwa sababu waliniheshimu na walinipa ushirikiano kwa asilimia 97 tofauti na wafitini walivyodhani, kwamba ningedhalilika zaidi.

“Kwa ujumla, sijutii kukaa jela na wala sitajutia kwani imekuwa ni sehemu ya ushahidi wa matatizo yanaoendelea gerezani na nchi inavyoendeshwa kwa udikteta.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles