BADI MCHOMOLO NA MITANDAO
HAKUNA kitu kizuri kwenye michuano ya Kombe la Dunia kuwaona nyota wanaofanya vizuri duniani katika klabu zao na kuwaona wakifanya hivyo katika kuyapigania Mataifa yao.
Mwaka 2010 idadi kubwa ya mashabiki nchini Afrika Kusini walisikitishwa sana na kitendo cha kocha wa timu ya Taifa ya Brazil, Carlos Dunga kuita majina ya wachezaji 23 wa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini na kuliacha jina la Ronaldinho Gaucho.
Hakuna ambaye alikuwa hataki kumuona mchezaji huyo akiwa uwanjani akifanya yake hasa katika uwezo wa kuuchezea mpira, kweli aliuteka ulimwengu kwa kiasi kikubwa na alikuwa mchezaji wa pekee ambaye anapendwa na idadi kubwa ya mashabiki duniani.
Walioumia hawakuwa mashabiki wa Afrika Kusini pekee, hata Tanzania ambapo timu hiyo ilipita na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki huku Taifa Stars ikipokea kipigo cha mabao 5-1. Wengi walitamani kumuona mchezaji huyo lakini yalikuwa maamuziki sahihi ya kocha huyo.
Kuelekea michuano hiyo kwa msimu wa 2018 nchini Urusi, kuna hatari kubwa ya kuona baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa wakishindwa kushiriki kutokana na timu zao kuwa katika wakati mgumu wa katika harakati za kufuzu.
SPOTIKIKI leo hii imekufanyia uchambuzi wa baadhi ya wachezaji ambao tunaweza tusiwaone kwenye michuano hiyo nchini Urusi mwakani, lakini wanapambana kuweza kufuzu.
Lionel Messi – Argentina
Kwenye ulimwengu wa soka kwa sasa hawezi kuliacha jina la Lionel Messi. Ni mchezaji pekee ambaye anaongoza kuwa na tuzo nyingi za mchezaji bora duniani Ballon d’Or, huku akiwa amechukua mara tano.
Amekuwa akifanya makubwa sana akiwa na kikosi chake cha klabu ya Barcelona, lakini mchango wake kwenye kikosi cha timu ya Taifa unaonekana kuwa mdogo sana hadi ikafikia hatua ya mashabiki wa nchi hiyo kuanza kumtupia lawama.
Kitendo hicho kilimfanya mchezaji huyo achukizwe na kutangaza kujiuzulu kuitumikia timu hiyo, lakini serikali na baadhi ya wadau wa soka walikaa chini na kumuomba abadili maamuzi hayo, alikubali kufanya hivyo lakini hali ni mbaya kuelekea kufuzu.
Soka la Amerika Kusini linaonekana kuwa ngumu sana, timu nne tu ambazo zinatakiwa kufuzu kati ya 10, wakati huo Brazi na Uruguay zikiwa zimejihakikishia kufuzu, lakini kazi kubwa ipo kwa Argentina ambayo inashika nafasi ya tato na Chile ikishika nafasi ya sita.
Argentina imebakisha michezo miwili, hivyo inahitaji kushinda yote na kuwaombea mabaya wapinzani wao Peru na Colombia ambao wanashika nafasi ya tatu na nne, lakini kama Argentina watapoteza michezo yao miwili basi tunaweza tusiwaone nyota wa timu hiyo kama vile Messi, Sergio Aguero, Di Maria, Paulo Dybala na wengine.
Alexis Sanchez – Chile
Ukiitaja timu ya Taifa ya Chile, hauwezi kuliacha jina la nyota wa timu hiyo Alexis Sanchez pamoja na kiungo wao Arturo Vidal, lakini wachezaji hao tunaweza tusiwaone kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia mwakani kutokana na timu yao kushika nafasi ya sita kwenye msimamo huku timu nne zikitakiwa kufuzu.
Sanchez ni mchezaji ambaye alikuwa anasubiriwa na idadi kubwa ya mashabiki katika kipindi hiki cha majira ya joto kumuona anaelekea wapi, alikuwa anahusishwa kutaka kuondoka kwenye klabu yake ya Arsenal na kujiunga na Man City au PSG, lakini hadi dirisha linafungwa bado yupo kwenye viwanja vya Emirates.
Mchango wa Sanchez na Vidal wa Bayern Munich unaonekana kuwa mdogo na kuifanya timu hiyo kuwa katika wakati mgumu wa kuelekea kufuzu. Wiki iliopita mashabiki wa Chile ambao ni mabingwa wa Kombe la America Kusini waliwatupia maneno wachezaji hao kuwa hawana msaada kwenye timu.
Cristiano Ronaldo – Ureno
Mabingwa wa michuano ya Euro 2016, Ureno wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi lao huku wakiwa na pointi 21, wakati huo Switzerland wakiongoza wakiwa na pointi 24, bado michezo miwili kwa kila timu kwenye kundi hilo, lakini Ureno bado wana nafasi ya kufuzu.
Chochote kina weza kutokea kwenye michezo hiyo miwili iliobaki, lakini kitu ambacho kitashangaza ni kuona Ureno wanapoteza michezo yote miwili iliobaki, ila bado ina nafasi kubwa ya kufuzu.