29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mashali awaachia neno wadau wa ngumi

dsc_0344*Mtoto, Baba yake wazungumza, kuzikwa leo Tandale,

NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

WOSIA ulioachwa na aliyekuwa bondia wa uzito wa kati (Super Middle Weight), marehemu Thomas Mashali (36) ‘Simba asiyefugika’, umeamsha  simanzi kwa wadau na tasnia nzima ya ngumi nchini.

Mwili wa marehemu Mashali aliyeuawa jana Kimara Bonyokwa, unatarajiwa kuzikwa leo Tandale, Dare es Salaam.

Kifo cha bondia huyo mahiri nchini kimetokana na kupigwa mapanga kichwani na watu, hali iliyopelekea kutokwa damu nyingi na kusababisha kifo chake.

Rais wa Oganaizesheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBO), Yassin Abdalla ‘Ustadhi’, aliliambia MTANZANIA kuwa tasnia ya ngumi nchini itaendelea kumkumbuka marehemu kutokana na wosia wake wa mwisho aliouacha katika tasnia hiyo.

“Usiku kabla ya tukio la kifo chake, tulikuwa naye marehemu katika kikao cha kujadili agenda nne za maendeleo ya mchezo huu hapa nchini.

“Tukiwa katika kikao hicho kutokana na hoja zilizokuwapo, marehemu alisema mchezo huu hautakuwa na mafanikio na utaendelea kutetereka kama viongozi wake wataendelea kuwa wababaishaji,” alisema Ustadhi.

Ustadhi aliongeza kuwa kifo chake kimeondoa ladha ya mchezo wa ngumi ambayo mashabiki wa mchezo huo waliizoea kutokana na umahiri aliokuwa nao katika kupigana.

“Mashabiki wa mchezo huu watakosa burudani kutoka kwa bondia huyu, kwani akiwa ulingoni alikuwa hachoshi, alikuwa anafurahisha na kuburudisha na alikuwa anapigana kwelikweli.

“Mashali alikuwa tofauti na mabondia wengine katika urushaji wa makonde na manjonjo ulingoni, hakika tutamkumbuka,” alisema Ustadhi.

Rais huyo alisema baada ya kujadiliana na familia ya marehemu, mwili wa Mashali utazikwa leo Tandale na si mkoani Songwe  kama walivyokuwa wamepanga.

“Mwili wa marehemu utazikwa kesho (leo), baada ya kukaa na familia na kufahamu eneo tutakalotumia kwa kuupumzisha mwili huo.

“Tulifika katika uamuzi huo baada ya kutambua  umuhimu wa bondia huyo kuzikwa hapa Dar es Salaam,” alisema Ustadhi.

MTANZANIA lilizungumza na baba mzazi wa bondia huyo, Malifedha Mashali, ambaye alieleza kuwa kifo cha mwanae ni pigo kubwa katika familia yake kutokana na mapenzi yake kwa marehemu.

“Hata kama angekuwaje Mashali bado ni mtoto wangu tu na uchungu uko palepale, kifo chake kimetuhuzunisha sana kwani kilikuwa cha ghafla na tulikuwa hatujaonana kwa zaidi ya miezi mitatu.

“Nilizungumza naye kwa njia ya simu kwa mara ya mwisho saa 2:00, usiku ambao mwanangu alipoteza maisha  kwani ilipofika saa 9:00  usiku, marafiki zake watatu walikuja hapa nyumbani kunitaarifu kuhusu kifo hicho,” alisema na kuongeza kuwa bado hajui ukweli wa tukio hilo na kusisitiza kuwa  ameachia kazi hiyo Jeshi la Polisi ambao wameahidi kutoa taarifa rasmi kesho.

Akizungumzia tabia ya marehemu mtoto wake, alisema alikuwa akisikia tuhuma za wizi ingawa hakuwahi kuthibitisha jambo hilo.

“Kuna vitendo vingine vinafanyika kutokana na makuzi ya watoto, lakini mbali ya kusikia watu wakisema, sijawahi kushuhudia mwanangu akifanya vitendo vya wizi vinavyozungumziwa,” alisema.

Mtoto mkubwa wa marehemu Mashali, Rose Mashali (17), alisema  baba yao amefariki wakiwa bado wanamuhitaji kutokana na umri wao kuwa mdogo.

“Siamini kama kweli baba amefariki, ametuacha tukiwa bado wadogo kwani hatujui hata maisha ya baadaye yatakuwaje, tunamwombea kwa Mungu apumzike kwa amani,” alisema Rose.

Bondia wa Super Middle Weight, Francis Cheka, alisema hakika wamepoteza bondia mahiri na ataendelea kuvikumbuka vituko na changamoto za marehemu wakiwa ulingoni.

“Pambano letu la mwisho Mashali alinipiga, lakini zaidi nitamkumbuka kutokana na changamoto zake ulingoni kwani alikuwa mpinzani wa kweli aliyekuwa ananifanya nifikirie sana tunapokuwa ulingoni,” alisema Cheka.

Cheka alisema alitarajia kupambana na marehemu Novemba 26, mwaka huu katika  pambano la mkanda wa dunia wa  WBF kama pambano lake la Ujerumani likiwa bado.

Naye bondia Abdalah Pazi ‘Dula mbabe’, alisema kuwa tasnia hiyo imepoteza bondia imara na shupavu mwenye kuifahamu kazi yake vema awapo ulingoni.

“Jembe limeondoka, tasnia imezizima kwa huzuni, Mashali alikuwa mfano wa mabondia bora nchini,” alisema Pazi.

MTANZANIA pia lilizungumza na  Mkurugenzi wa  Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Emmanuel Mlundwa, ambaye alisema marehemu ameacha pengo kubwa katika tasnia ya mchezo huo nchini.

“Novemba 19, mwaka huu marehemu alitakiwa kutua nchini Ujerumani kwa ajili ya pambano la kawaida la raundi nne.

“Leo tulitarajia kupokea barua maalumu kwa ajili ya pambano hilo ambalo tulishirikiana naye kwa karibu katika kulifanikisha,” alisema Mlundwa.

Mashali ambaye ameacha watoto watano wote wa kike, katika uhai wake alikuwa akimiliki mkanda wa UBO wa uzito wa Super middleweight wa Afrika na dunia, na  WBF wa Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles