25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maseneta wanne walivyomnusuru Trump kung’oka urais Marekani

Washington, Marekani

BARAZA  la seneti mjini Washington limemtakasa Rais Donald Trump, katika kesi ambayo alikuwa akishutumiwa na wabunge wa chama cha Democrat kutumia vibaya madaraka yake na kutatiza kazi za Baraza la Wawakilishi.

Katika kura ambazo zimefuata msingi wa vyama, isipokuwa moja tu, maseneta 52 wamemwondolea hatia Trump, dhidi ya 48 waliotaka afukuzwe kazi.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Marekani, John Roberts ndiye aliyeyatangaza matokeo hayo.

”Katika shauri hili la mashtaka, maseneta 48 wamesema Donald John Trump anayo hatia kwa makosa aliyoshtakiwa, maseneta 52 wamesema hana hatia kwa mashtaka hayo.

“Waliomkuta na hatia hawafiki theluthi mbili ya maseneta waliopo kwahiyo Rais Trump hakukutwa na hatia katika shauri hili la mashtaka,” alisema Jaji Roberts.

Rais Trump alikuwa akikabiliwa na shutuma za kutumia vibaya madaraka yake, kwa kumshinikiza rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kumchunguza makamu wa zamani wa Rais Joe Biden, ambaye anaweza kuwa mpinzani wa Trump katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba mwaka huu.

Republican wanaolithibiti baraza la seneti wamepiga kura 52 kumtakasa Trump, huku mmoja tu, Mitt Romney akijiunga na Wademocrat na kufikisha idadi ya kura 48 zilizotaka Trump atimliwe kutoka madarakani.

Shitaka la pili dhidi ya Trump lilikuwa kulitatiza baraza la wawakilishi kutekeleza majukumu yake kwa kuwazuia maafisa wa utawala wake kutoa ushahidi mbele ya baraza hilo.

Kuhusu shitaka hili, Romney amejiunga na Republican wenzake na kuwashinda Democrat kwa kura 53 dhidi ya 47.

Akizungumza baada ya matokeo hayo, kiongozi wa maseneta  wa wanademocrat walio wachache, Chuck Schumer, amesema kura iliyomuondoa hatiani Trump haina thamani yoyote, kwa sababu Wanarepublican walikataa kata kata kusikiliza mashahidi.

Schumer amesema anatumaini Wamarekani watajua kilichotokea.

”Naamini Wamarekani watajua kuwa kilichotokea ni kisa cha kufunika makosa kikubwa zaidi katika historia ya nchi yetu. Naamini kwamba Wamarekani watajua upande gani umesimamia ukweli, na upi uliogopa ukweli na kuufichaficha. Lakini, hatua kwa hatua, ushahidi zaidi utaibuka, na Republican watawajibishwa kwa namna walivyopiga kura.” Amesema Seneta Schumer.

Kiongozi mwingine wa chama cha Democrat, Spika wa baraza la wawakili Nancy Pelosi, amewashutumu Republican kufanya alichokiita; ”kuhalalisha uvunjifu wa sheria, na kuupa kisogo mfumo wa wizani wa mamlaka ya mihimili ya utawala”.

Angekutwa na hatia kwa kosa lolote kati ya hayo, Trump angelazimika kuachia madaraka yake kwa Makamu wa rais Mike Pence.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema Trump, ambaye ni rais wa tatu kufunguliwa mashitaka nchini Marekani, na wa kwanza kugombea muhula wa pili baada ya mchakato huo dhidi yake, atayatumia matokeo ya kumtakasa kama turufu katika kampeni ya kuwania muhula wa pili.

Mchakato huo ambao umemalizika  uliigawanya vikali Marekani na Trump atakuwa rais wa kwanza aliyeghabika kwenda kwenye uchaguzi.

Baraza la Wawakilishi linaloongozwa na Kidemokrasia liliidhinisha nakala za mashtaka Disemba 18.

Hii ni mara ya tatu katika historia ya Marekani kwa rais  kukabiliwa na kesi ya kutumia madaraka vibaya kwa maslahi yake binafsi.

SHUTUMA ZILIZOKUWA ZIKIMKABILI

Kuomba msaada kwa serikali ya Ukraine kumsaidia achaguliwe tena mwezi Novemba.

Kusitisha kutoa misaada ya mamilioni ya fedha pamoja na msaada wa kijeshi kwa Ukraine hadi rais wa nchi hiyo afanye uchunguzi dhidi mpinzani wake.

Ikulu ya Marekani kutoruhusu wafanyakazi wake wote kutoa ushaidi dhidi ya Trump wakati kesi ya rais huyo iliposikilizwa wa mara ya kwanza mwaka jana.

Trump alikanusha kuhusika na makosa yote na kikosi chake cha sheria kudai kuwa madai hayo ni hatari sana na upotoshaji wa katiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles