MWANDISHI WETU
WANANCHI wa Sogea, Wilaya ya Mjini Unguja wamemkabidhi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, orodha ya watu wanaoshukiwa kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya visiwani Zanzibar.
Wananchi hao walikabidhi orodha hiyo baada ya Naibu Waziri Masauni kuwataka waorodheshe majina ya watu wanaowafahamu wakituhumiwa kujihusisha na biashara hiyo ambayo imekuwa ikiharibu nguvu kazi ya taifa na kusababisha matukio ya uhalifu katika sehemu mbalimbali visiwani humo.
Awali, wakiwasilisha kero zao kwa nyakati tofauti, wananchi hao waliiomba serikali kudhibiti biashara hiyo ya dawa za kulevya kwa vile imekua ikishamiri kwa kasi visiwani humo na wanashangazwa na ukimya wa mamlaka husika kuacha biashara hiyo ikizidi kuleta madhara katika jamii.
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Masauni aliwaahidi wananchi hao kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na wauzaji wa dawa za kulevya huku akitoa maelekezo kwa polisi kuwakamata watu wote waliotuhumiwa na uchunguzi uanze mara moja.
“Hatuwezi kama taifa tukawa na vijana ambao hawana faida katika jamii.
“Vijana ni nguvu kazi ya taifa, tutahakikisha majina yaliyoletwa hapa tunayafanyia kazi na natoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa na nitahitaji ripoti hiyo ndani ya wiki mbili,” alisema Masauni.
Akizungumza katika mkutano huo, Kamishna Msaidizi, Saleh Mohamed Saleh, aliwaomba wananchi kuzifikisha taarifa za uhalifu katika vituo vya Jeshi la Polisi au Serikali ya Mtaa hatua ziwe zinachukuliwa kudhibiti uhalifu katika maeneo yao.