WASHINGTON, MAREKANI
MAREKANI imewawekea mabilionea saba washirika wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hali inayozidi kufufua kile kinachoitwa Vita Baridi mpya.
Waliolengwa ni pamoja na mfanyabiashara wa vyuma Oleg Deripaska, anayeelezwa kufanya kazi kwa niaba ya Serikali ya Urusi pamoja na Alexei Miller, mkurugenzi wa kampuni kubwa ya nishati inayomilikiwa na serikali ya Gazprom.
Mali zao zozote zilizo katika maeneo yaliyo chini ya umiliki wa Marekani zitataifishwa.
Pia walio katika orodha hiyo ni Suleiman Kerimov, anayechunguzwa na Ufaransa kwa tuhuma za kuingiza mabilioni ya euro katika masanduku yaliyojaa fedha taslimu, na Kirill Shamalov, bilionea anayeripotiwa kuwa mkwe wa Putin.
Zaidi ya hayo, utawala wa Rais Donald Trump umelenga kampuni 12, zinazomilikiwa au kudhibitiwa na mabilionea hao pamoja na maofisa waandamizi 17 wa Urusi na kampuni ya taifa ya mauzo ya silaha, Rosoboronexport.
‘Marekani inachukua hatua hizi kutokana na vitendo vichafu vya serikali ya Urusi vinavyoendelea na kuongezeka kote duniani,” ofisa mmoja mwandamizi aliwaambia wanahabari.
“Hii ni pamoja na uvamizi wa Crimea, kuchochea machafuko mashariki mwa Ukraine, kuusaidia utawala wa Assad nchini Syria na uhalifu wa mitandaoni,” alidai.
‘Lakini muhimu zaidi ni kuitikia mwendelezo wa Urusi wa kushambulia demokrasia za magharibi.”
Hata hivyo, msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House, Sarah Sanders alisema vikwazo vipya havina maana kwamba ofa ya Rais Trump kukaa meza moja na Putin mjini hapa imefutwa.
“Rais ameshaeleza wazi anataka uhusiano mzuri na Urusi lakini pia itategemeana na vitendo vya Warussia,” alisema.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imeahidi kujibu vikali na imesema Marekani imeungana na maaadui wa soko la dunia, wakitumia njia za kiuatawala kuwaondoa washindani kama vile Rosoboronexport.