28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maoni ya wabunge, wasomi

MAJIBUNA MWANDISHI WETU, DODOMA

Baadhi ya wabunge walitoa maoni tofauti kuhusu bajeti ya serikali iliyowasiliswa jana ambapo pamoja na mambo mengine waliisifu Serikali kwa kuongeza  kodi katika vitu visivyo vya lazima.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema bajeti hiyo ni nzuri kwakuwa katika kodi zilizoongezwa hakuna inayomgusa mwananchi wa kawaida moja kwa moja.

Alisema kodi nyingi zilizoongezwa haziendi kuongeza gharama kubwa kwa wananchi,

“Kama nchi tuna challenge (changamoto) ya kuongeza wigo wa kodi kwa kuibua vyanzo vya mapato, wamesema kurasimisha sekta isiyo rasmi kuingia katika kodi nayo ni mawazo mazuri,”alisema Bashe.

Naye Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi  Mwigulu Nchemba  alisema bajeti imejielekeza katika mambo yanayoleta ufanisi na ni njia mbadala ya ukusanyaji wa mapato.

Mbunge wa Mlalo Rashid Shangazi (CCM) alisema bajeti hiyo inafanana na Mpango wa Maendeleo hivyo serikali inapaswa kuangalia masuala ya msingi hasa mfumuko wa bei za bidhaa.

“Mfumuko wa bei unapaswa udhibitiwe ili kupunguza ugumu wa maisha,bidhaa zinaongezeka bei kwa kasi,”alisema Shangazi.

 

Zitto: Ni bajeti ya deni la taifa

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akiizungumzia bajeti hiyo alisema ni ya deni la Taifa kwakuwa kiasi cha fedha Sh trilioni nane za makusanyo ya mapato zitakwenda kulipa deni hilo.

“Makusanyo ya mwaka mzima ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni takriban Sh trilioni 15 sasa trilioni nane zinakwenda kulipia deni la Taifa na trilioni saba zinalipa mishahara. Ndio maana waziri Mpango alikuwa kila akisema anaeleza ukiondoa deni la Taifa kwa sababu ni kubwa.

“Maana yake ni kwamba fedha zinaporomoka, wasiwasi wangu ni uwezo wa serikali wa kuweza kukusanya fedha hizo inazotarajia inabidi tusubiri kwa mwaka mmoja tupime jambo hilo,” alisema.

Kuhusu msamaha wa kodi, Zitto ambaye ni mmoja wa wajumbe katika ya bajeti alisema walipendekeza isizidi asilimia moja ya pato la taifa.

“Wameondoa msamaha wa kodi kwenye taasisi za dini na jeshi lakini ni kiwango kidogo mno cha msamaha. Kiwango kikubwa cha msamaha wa kodi kipo kwenye sekta ya madini ambayo ni asilimia 75 lakini hakujaguswa,” alisema Zitto.

Kuhusu makato ya kodi katika posho za wabunge suala hilo limewekwa kisiasa na ingekuwa vyema lingefanyika 2020 wakati ambao wabunge wanamaliza muda wao.

“Limetamkwa ili kuwafurahisha tu wananchi, sheria inaeleza wazi posho za wabunge hazitozwi kodi…tunalipwa malipo ya aina tatu, mshahara, posho ya siku (120,000) na ‘sitting allowance’ 220,000 ambayo sijui ilitokea wapi.

Zitto alisema kwa upande wa kodi (VAT) kwa bidhaa zinazotoka Tanzania bara kwenda visiwani au visiwani kwenda bara itazorotesha uchumi wa Zanzibar.

“Sijui mantiki ya makubaliano haya, sheria inasema lazima waziri kabla hajatangaza akubaliane na mwenzake wa visiwani, nategemea mjadala mkubwa katika hili kwa sababu itaumiza uchumi wa Zanzibar, na ile VAT kwenye utalii inaweza kuathiri sekta nzima ya utalii,” alisema.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Binto Binto alisema ana imani kuwa serikali imefanya utafiti wa kutosha juu ya sheria ya manunuzi kabla ya kupeleka hati ya dharura bungeni.

Naye mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jenson Jingo alisema bajeti hiyo imezingatia makundi yote na kwamba ni wakati wa vijana kuamka na kufanya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles