26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maofisa wanne wavuliwa madaraka

profesaNA CHRISTINA GAULANGA, DAR ES SALAAM

WATENDAJI wanne wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, wamevuliwa madaraka, wakidaiwa kukiuka taratibu za kusajili wanafunzi wanaojiunga na elimu ya watu wazima nchini.

Watendaji hao, wanadaiwa kuchagua wanafunzi kama chaguo la pili katika shule za sekondari za Serikali wakati hawajafikia viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa alisema hatua hiyo imefikiwa, baada ya wazazi na walezi kulalamikia muundo wa udanganyifu wa upatikanaji wanafunzi wanaojiunga na elimu hiyo.

Aliwataja wakufunzi  hao na mikoa yao kwenye mabano, kuwa ni  Wotugu Muganda (Dar es Salaam), Senorina Kateule (Dodoma) na Steward Ndandu (Mwanza na Geita).

Alisema baadhi ya wakufunzi wakazi wa taasisi hiyo,walikuwa wakishirikiana na halmashauri na mikoa kufanya usajili wa wanafunzi kinyume na sheria jambo ambalo limeleta malalamiko kwa wazazi nchini.

Alisema watendaji wa taasisi hao, wamekuwa wakifuatilia matokeo ya darasa la saba katika halmashauri na mikoa, kisha kuchukua majina ya wanafunzi ambao wamefeli mitihano yao na kupata alama chini ya 100 na kuwaita kwa madai kuwa wameteuliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Alisema kutokana na kushindwa kutoa ufafanuzi vizuri kwa wazazi ambao hutumia kama mtaji wa kupata wanafunzi wengi, wamejikuta wakigonga mwamba baada ya kutolewa agizo la elimu bure.

“Ilikuwa kawaida yao kuchukua majina ya wanafunzi waliofeli na kudai wamechaguliwa chaguo la pili la Serikali ambapo ada yake huwa ni kulingana na eneo husika…kwakuwa kila kituo kina gharama zake.

“Kwa sababu mpango huo haukuwa wa wazi na wenye kificho, uliwachanganya wazazi ambao wengi wamekuja kulalamika baada ya kufikiri watoto wao wamefaulu kwenda shule za Serikali…walileta malalamiko baada ya kudaiwa ada wakati Serikali imeagiza elimu itolewe bure,”alisema Profesa Eustella.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi, ilibainika  mbinu walizokuwa wakizitumia ni kwa ajili ya kuwavuta wanafunzi wawe wengi katika vituo hivyo.

Pia kamishna huyo amesitisha utaratibu wa kuchagua wanafunzi kupitia ofisi za halmashauri na mikoa bila ridhaa ya wazazi na walezi.

“ Kuanzia sasa wanafunzi katika vituo hivi wanapaswa kujiunga kwa hiari kama ilivyo shule nyingine zisizo za Serikali…wakufunzi wakazi watengeneze nafasi hizi kwa wale wanaohitaji kwa hiari na si vinginevyo,”alisema Profesa Eustella.

Alisema Serikali imekuwa ikichukua wanafunzi wa darasa la saba waliopata alama 100 hadi 250 na wale wanaopata chini ya hapo hukosa sifa za kujiunga na shule za serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles