32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MANUSURA LUCKY VINCENT KUTOA USHAHIDI KORTINI

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

MWANAFUNZI   Wilson Tarimo, aliyenusurika katika ajali ya basi iliyoua wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ni miongoni mwa mashahidi 15 wa upande wa Jamhuri kwenye kesi inayomkabili mmiliki wa shule hiyo, Innocent Moshi.

Moshi anakabiliwa na tuhuma za makosa ya usalama barabarani ikiwamo kusafirisha wanafunzi bila kuwa na vibali muhimu.

Katika kesi hiyo namba 78 ya mwaka huu, Moshi pamoja na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Nkana, jana walisomewa hoja za awali katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Desderi Kamugisha, Wakili wa Jamhuri, Khalili Nuda, alidai Jamhuri inatarajia kuwa na mashahidi 15 katika kesi hiyo, pamoja na vielelezo 12.

Mashahidi wengine ni Ofisa Kazi Mfawidhi wa Idara ya Kazi Mkoa wa Arusha, Wilfred Mdemi, Mohamed Matumula kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar Insurance, Songoyi Jilala (askari wa usalama barabarani Arusha), Koplo Hamad (Karatu), Inspekta Shukrani (askari wa usalama barabarani Arusha), Koplo Saada (trafiki Arusha) na E.4312 PC Mugobe (trafiki Arusha).

Wengine ni Mkuu wa Polisi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO), Nuru Suleiman, G 4130 PC Mwita (askari wa usalama barabarani Karatu), Ignatus Paul(Karatu), Leonidas Gerald (Morombo) na Hamis Omary mkazi wa Sombetini.

Wakili Nuda alitaja vielelezo hivyo kuwa ni kadi ya gari  namba  T 871 BYS, mkataba wa ununuzi wa gari, Barua ya RTO kwenda Sumatra ya Mei 8 mwaka huu, barua ya RTO kwenda Zanzibar Insurance ya Mei 8, mwaka huu na  taarifa ya Zanzibar Insurance ya Mei 9 mwaka huu.

Vingine ni taarifa ya Sumatra ya Mei 9 mwaka huu, taarifa ya idara ya kazi, taarifa ya ukaguzi wa gari, ramani ya eneo la tukio, maelezo ya mshitakiwa wa kwanza na maelezo ya mshitakiwa wa pili.

Wakili huyo aliiomba mahakama hiyo kutoa wito kwa mashahidi hao.

Akiwasomea hoja hizo za awali, Wakili Nuda alidai  katika shitaka la kwanza linalomkabili Moshi, ni kufanya biashara ya usafirishaji abiria bila kuwa na leseni ambapo kati ya Desemba 12 mwaka jana hadi Mei 6 mwaka huu, alitumia gari katika barabara ya umma  aina ya Mitsubishi Rossa T. 871 BYS, kubeba wanafunzi.

Alidai shitaka la pili ni kuruhusu gari hilo kutumika bila kuwa na bima kati ya Desemba 16 mwaka jana na Mei 6 mwaka huu.

Shitaka  la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake kati ya Juni Mosi mwaka jana hadi Mei 6, mwaka huu akiwa mmiliki  wa gari hilo alishindwa kuingia mkataba wa ajira kinyume na sheria za ajira na dereva wake, Dismas  Gasper ambaye kwa sasa ni marehemu.

Katika shitaka  la nne, Moshi anadaiwa kubeba na kuzidisha  abiria  13 ambako Mei 6, mwaka huu akiwa Mmiliki wa Kampuni ya Lucky Vincent, katika maeneo ya Kwa Morombo, aliruhusu gari hilo kubeba abiria 38 badala ya abiria 25.

Katika kesi hiyo, Nkama anakabiliwa na shitaka moja ambalo ni kuzidisha abiria katika chombo cha usafiri  ambako akiwa mwandaaji wa safari hiyo ya wanafunzi aliruhusu abiria zaidi ya 13 kupanda katika gari hilo ambalo lilipaswa kuwa na abiria 25.

Baada ya kusomewa maelezo hayo Moshi alikiri gari hilo kwenda Karatu likiwa halina bima huku Mwalimu Mkuu Msaidizi akikiri kuwa alizidisha abiria katika safari hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles