Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM
MEYA wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amesema manispaa hiyo italipa fidia kwa watu watakaoachia maeneo ya huduma za jamii kupisha mradi wa upimaji, upangaji na urasimishaji wa maeneo ya makazi.
Mradi hiyo unatekelezwa na Kampuni ya Upimaji na Upangaji Makazi (HUSEA) katika Mtaa wa Kunguru Kata ya Goba, Dar ea Salaam.
Alikuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano ulohusisha wakazi wa mtaa huo na Kampuni ya HUSEA.
Kampuni hiyo ilikuwa ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia hatua ya upimaji baada ya kukamilisha upitiaji wa mipaka.
“Ili miradi ya urasimishaji makazi iweze kufanyika vizuri bila usumbufu ni lazima halmashauri tusaidie kulipa fidia itakapoonekana kuna uhitaji wa maeneo ya huduma za jamii kama shule, zahanati, viwanja vya michezo na barabara ili upangaji ufanyike kisasa,” alisema Jacob.
Hata hivyo, alisema fidia haitalipwa kwa watu ambao wanatakiwa kupisha upanuzi wa barabara kwa kusogeza hatua chache na badala yake watalipwa wale ambao barabara italazimika kukatiza kwenye viwanja vyao kwa mujibu wa wataalamu wa upangaji.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Mwenyekiti wa HUSEA, Renny Chiwa, alisema mtaa huo una uhaba wa maeneo ya huduma za jamii yatakayoendana na wingi wa watu waliopo.
“Katika hatua za awali za kupitia mipaka tumeona kuna changamoto ya uhaba wa maeneo ya kutosha ya huduma za jamii huku baadhi ya maeneo yakiwa hayapitiki kutokana na kukosekana barabara,” alisema Chiwa.
Alisema mradi huo ni shirikishi yamekuwa yakifanyika mazungumzo na baadhi ya watu ambao viwanja vyao vinazuia barabara na kuingilia maeneo ya wazi waweze kuachia kwa ridhaa yao.
Mkurugenzi wa Upangaji wa Vijiji na Miji kutoka Wizara ya Ardhi na Makazi, John Lupala, alisema ili kufanikisha mradi huo kwa haraka atapangwa Ofisa Ufuatiliaji kutoka wizarani ashirikiane na HUSEA katika mradi huo wa Mtaa wa Kunguru.
“Kama mtaenda kwa umoja huu itakuwa rahisi kwa Kamishna wa Ardhi kuja kutolea hati hapa mtaani kwenu kuondoa usumbufu wa kwenda wizarani kufuatilia hati zenu,” alisema Lupala.