UGONJWA wa kisukari ni tatizo la kiafya ambalo hutokea pale ambapo mwili wa binadamu unashindwa kutawala kiwango cha sukari kinachotakiwa katika mzunguko wa damu na mwili kwa ujumla.
Mwili unaposhindwa kutawala kiwango hicho, husababisha sukari kuongezeka katika damu hatimaye kuharibu mifumo ya mwili kufanya kazi inavyopaswa.
Ugonjwa huu ni moja kati ya magonjwa yaliyopo katika kundi la magonjwa yasiyoambukiza – yale ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kutegemeana na staili ya maisha yake mfano, ulaji, vinywaji, pia inawezekana ikawa ni tatizo alilozaliwa nalo.
Kutegemeana na chanzo cha ugonjwa huu wa kisukari, (Diabetes type I, and Diabetes type II), matibabu yake yanahusisha dawa mbalimbali ambazo kwa pamoja husaidia kurekebisha kiwango cha sukari kwa mtu mwenye tatizo hili.
Tatizo la kisukari kutegemeana na ukubwa wake, linaweza kusababisha mtu apate matatizo mengine yakiwamo vidonda vinavyochelewa kupona, kuharibika kwa mishipa ya damu, matatizo ya nguvu za kiume, pamoja na magonjwa ya moyo.
Hali hii husababisha matibabu kwa mgonjwa kuhusisha dawa ambazo zitasaidia kutibu matatizo hayo mengine ambayo chanzo chake kisukari.
Miongoni mwa dawa zinazotumika moja kwa moja katika kutibu tatizo la kisukari ni pamoja na dawa ya sindano (Insulin) na dawa za vidonge (Glibenclamide na Metformin).
Dawa ya sindano aina ya Insulin imetengenezwa kutoka katika chembechebe asilia zinazopatikana kwa wanyama. Ili dawa hii iweze kumsaidia mgonjwa ni lazima itumike kulingana na dozi ambayo mgonjwa ameandikiwa na daktari, pia kwa kuwa mgonjwa anaweza kupatiwa ili aweze kuitumia akiwa mazingira ya nyumbani.
Jambo la kuzingatia ni kwamba inapaswa kuhifadhiwa katika mazingira yenye ubaridi mfano katika friji (haitakiwi kuganda). Aidha, kwa mazingira ambayo hakuna friji, mgonjwa anashauriwa kuihifadhi kwa kuiweka katika chombo/mkebe na kuitumbukiza katika maji yenye ubaridi. Dawa hii haitokuwa na msaada katika matumizi endapo itahifadhiwa katika mazingira yenye joto mfano kabatini, jikoni au dirishani ambako mionzi ya jua inapita muda mwingi.
Katika matumizi ya dawa jamii ya vidonge, mambo ya msingi ya kukumbuka pamoja na usahihi wa dozi ni kuhakikisha dawa uliyopewa na mtaalamu wa afya unaitumia katika ratiba sahihi ya ulaji wa chakula, iwe kabla au baada ya chakula inategemea na ushauri wa daktari. Vyakula vilivyozoeleka siku zote vinachangia kuongeza nguvu/sukari na joto mwilini hasa vile vyenye wanga. Hivyo, dawa inayotumika inatakiwa ikasaidie kupunguza kiwango cha sukari ambacho kitaingia mwilini kutoka katika chakula cha wanga ambacho kimetumika au vinywaji.
Mfano, dawa aina ya Metformin vidonge, hutumika kwa mgonjwa wa kisukari ambaye seli za mwili wake zinashindwa kuhisi (sense) uwapo wa insulin(asilia katika mwili ambayo hurekebisha kiwango cha sukari). Matumizi ya dawa hii ni kuboresha uwezo wa mwili katika kurekebisha kiwango cha sukari katika damu – inashauriwa itumike pamoja na chakula.
Kutegemeana na hali ya mgonjwa, kuna mazingira ambayo dawa zote mbili (vidonge na sindano) hutumika kwa pamoja ili kumsaidia.
Wakati mgonjwa anatumia dawa za kisukari, mfano kwa mgonjwa anayetumia dawa aina ya metformin ni vyema akachukua tahadhari katika matumizi ya dawa hizi: Furosemide (lasix), Nifedipine (dawa ya presha), Cimetidine/Ranitidine(dawa za vidonda vya tumbo na kiungulia) pamoja na Digoxin (dawa ya moyo).
Kwa kuwa ugonjwa wa kisukari pia unaweza kumsababisha mtu kupatwa na vidonda ambavyo havitibiki kwa urahisi, inashauriwa kuwa mwangalifu kujilinda asipatwe na majeraha. Aidha, endapo majeraha yatatokea, huduma ya dawa/matibabu itategemeana na uchunguzi wa kitaalamu. Pia kuna dawa za kupakaa ambazo mgonjwa anaweza kupatiwa ili ziweze kumsaidia katika kutibu vidonda.
Pia, kisukari kinaweza kusababisha matatizo ya nguvu za kiume, endapo mgonjwa wa kisukari atapatwa na hali hii ni vyema akamfahamisha daktari ili aweze kumsaidia kwa kumpatia dawa na ushauri unaofaa hatimaye aondokane na hali hiyo.
Pamoja na matumizi ya dawa katika kutibu kisukari, inashauriwa kufuata kanuni za afya ikiwamo kufanya mazoezi na kuwa na ulaji mzuri/salama wa vyakula na vinywaji ili kuendelea kuilinda afya.