AKIWA ameegemea sofani mwake mama Sophie Mei Lan (29) anamnyonyesha binti yake mwenye njaa, licha ya kuwa kwa sasa tayari ana umri wa miaka mitano, akiwa hana dalili za lini ataacha ziwa la mama yake huyo.
Sophie anaamini kitendo hiki kinaimarisha uhusiano baina yake na bintiye huyo Jasmine – ijapokuwa anafahamu hakifurahiwi na mumewe.
Sophie pia mama wa binti mwingine Arianna (2) anasema: “Sidhani kama kuna kitu cha ajabu kuhusu kunyonyesha watoto wako mwenyewe katika umri huo.
“Maziwa ya mama ni mazuri kwa afya, ni chakula bora na ni bure. Kwa hiyo, mbali ya faida ya kiafya kwa binti zangu pia yameokoa maelfu ya pauni, ambazo ningezipoteza kwa miaka mingi kwa kununua maziwa au vyakula mbadala,” anasema.
Wengi wa kina mama husitisha unyonyeshaji baada ya miezi sita lakini utafiti mpya uliofanywa na Chama cha Saikolojia cha Marekani umebainisha kuwa kunyonyesha kwa muda mrefu zaidi kuna faida za kudumu kwa miaka mingi ikiwamo kuimarisha afya ya akili kwa kina mama.
Unyonyeshaji kwa miaka mingi ulifahamika kuwa na matokeo mazuri kwa watoto, akili, afya nzuri na mifumo yenye nguvu ya kinga mwilini.
Sophie kutoka Wakefield, nchini Uingereza pia analala kila usiku na mabinti zake ili waweze kupata chakula chao hicho kisha kulala.
Anasema humnyonyesha Ariana hadi mara 10 ndani ya saa 24 huku Jasmine akimnyonyesha zaidi nyakati za usiku na kwamba ratiba yake hiyo si rahisi kwa sababu haikuwa sehemu ya mpango wake.
“Mara nilipoelekea kumpata Ariana, nilidhani nitaacha kumnyonyesha Jasmine, lakini nilipomzaa Ariana, Jasmine hakuwa tayari kuacha bali kuendelea na nyonyo!
“Hivyo daima nawajibika kuwapatia mabinti zangu wanachohitaji,” mwanablogu huyo wa masuala ya uzazi anasema.
Mama huyo wa watoto wawili anasema unyonyeshaji huo umeokoa maelfu ya pauni kwa kipindi cha miaka mingi kwani hahitaji kununua maziwa mara kwa mara.
Hata hivyo, hilo limesababisha ugomvi na mumewe mpishi Chris Hale, 30.
Anakiri: “Husababisha mzozo kidogo katika uhusiano wetu. Chris angependa kuniona nikiacha kunyonyesha kwa sababu ni kazi yenye kuchosha.
“Huwa hatugombani kuhusu hilo, lakini tunajua maziwa ya mama ni moja ya vitu vyenye afya zaidi unavyoweza kuwapatia watoto wetu.”
Hata hivyo, katika mahojiano mengine ya hivi karibuni katika televisheni, mumewe alionekana kukubali matokeo kwa uamuzi wa mkewe huyo.
Sophie anasema pia huvuta macho ya watu kila anapomnyonyesha Jasmine hadharani. anasema: “Watu huniangalia. Najisikia vibaya kidogo.”
Awali mapema mwaka huu, Mwanamitindo Tamara Ecclestone (32), aliwahi kukaririwa akisema hupokea kauli chafu kwa kumnyonyesha bintiye Sophia mara tatu au nne kwa siku.
Sophie anakiri kuwa angependa kuacha kumnyonyonyesha msichana wake huyo mkubwa kwa sababu wakati mwingine inakera mno.” Lakini binti zake hawaoneshi dalili za kutaka kuacha kunyonya maziwa yake.
Mwanablogu huyo anasema: “Jasmine alianza shule mwaka jana na nilimwambia si watoto wengi katika darasa lake wanaonyonya maziwa ya mama, lakini hakujali hilo.
“Wakati watakapopata meno ya maana itakuwa ngumu kwao kuendelea na kamchezo haka, pengine wataamua kuacha watakapofikisha umri wa miaka saba.