Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, jana aliwaweka ndani maofisa ardhi zaidi ya 10 kwa saa sita.
Imeelezwa kuwa Makonda alifanya hivyo kwa kile kilichoelezwa kukaidi agizo lake la kuwataka wawahi katika eneo la mkutano kusikiliza migogoro ya ardhi.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Nakasangawe Kata ya Wazo, Dar es Salaam, baada ya maofisa hao kuchelewa kufika tofauti na walivyotakiwa.
Makonda alisema walikubalina kuwahi katika kikao cha pamoja.
Alisema lakini katika hali ya kushangaza ingawa yeye alifika katika eneo hilo kwa wakati, maofisa hao walifika saa 5.00 asubuhi kitendo ambacho hakiendani na nidhamu ya kazi.
“Hivi sasa wamewekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Wazo na tumelazimika kuahirisha shughuli hii kwa muda,” alisema Makonda.
Alisema hatua aliyoichukua kwa maofisa hao itakuwa fundisho kwa watendaji wengine kuwafanya wawajibike wakati wote kwa ajili ya masilahi ya wananchi na si yao binafsi.