Na Damian Masyenene, Shinyanga
Toka mwaka 2015/16 hadi 2020 Tanzania imeendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya hususani afya ya uzazi na mtoto kwa kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma, ambapo taifa limejiwekea malengo kuwa ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe ni miongoni mwa nchi chache duniani kufikia malengo endelevu ya maendeleo kama ilivyofikia malengo ya millennia kwenye kushusha vifo vya watoto.
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka wazi mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita juu ya kuboresha sekta hiyo na kupunguza tatizo la vifo vya akina mama wakati wa kujifungua na watoto wachanga.
Hata hivyo taarifa za mapitio ya vifo vingi vya akina mama na watoto zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya vifo vitokanavyo na uzazi vinazuilika, hivyo Rais Samia alisema juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto zitaendelezwa kwani anasikitishwa kusikia mwanamke anapoteza Maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ambazo zingeweza kuzuilika.
“Nilipokuwa Makamu wa Rais nilizindua Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ili kutilia mkazo uwajibikiaji wa wadau wote katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Hivyo, huu ni mradi wangu wa moyoni kabisa. Binafsi, huwa nasikitishwa sana kusikia mwanamke anapoteza maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ambazo zingeweza kuzuilika,” alisisitiza.
Kufuatia mwelekeo huo chanya wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, baadhi ya wadau wa masuala ya wanawake na Watoto mkoani Shinyanga wameonyesha matumaini makubwa, huku wakipendekeza baadhi ya changamoto zinazopelekea vifo hivyo ikiwemo urasimu wa wahudumu wa afya, mazingira mabovu ya vituo vya afya kurekebishwa ili kutimiza azma hiyo.
Mmoja wa wadau hao, Glory Mbia ambaye ni Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mkoa wa Shinyanga, ameiambia www.mtanzania.co.tz kuwa ni jambo lenye matumaini kwa serikali kuweka kipaumbele katika suala la kutokomeza vifo vya kina mama na Watoto, kwani hiyo inaonyesha wazi kuwa inalenga kuimarisha upatikanaji haki za wanawake na watoto kwani suala la afya ni haki ya msingi ya binadamu.
“WFT tukiwa miongoni mwa mashirika yanayotetea haki za wanawake na watoto tumefarijika sana na mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, tunamuahidi kiongozi wetu na serikali yote ushirikiano wa dhati kabisa.
“Mwelekeo wake katika kuhakikisha usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi. Hilo ni suala ambalo kwa miaka mingi tumekua tukilipigania sasa tumeona mwelekeo wa serikali yake ni kuhakikisha kuwa wanalizingatia kwa kuhakikisha linatokea kwa kufuatana vigezo vinavyohitajika,” alisisitiza.
Naye mjasiriamali na Mkurugenzi wa Lulekia Company, Ansila Benedict ameshauri mifumo ya afya kuimarishwa na kuboreshwa ili kuleta ufanisi, pia vifaa tiba vitosheleze mahitaji na wahudumu wa afya waongezwe ili wajawazito waweze kupata huduma sahihi kwa wakati muafaka.
“Kuna changamoto kadhaa mfano mama mjamzito anaweza kujifungua salama mara akaanza kutokwa damu ghafla lakini hadi daktarin apatikane inachukua saa moja, akitakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji unakuta umeme hakuna, kwahiyo miundombinu yetu katika huduma ya afya bado ni dhaifu inapaswa kuboreshwa ili ikidhi mahitaji,” alieleza.
Katika taarifa ya utekelezaji katika sekta ya afya mkoa wa Shinyanga iliyotolewa Februari 10, mwaka huu na Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. Nuru Mpuya kwenye kikao cha ushauri cha mkoa, ilieleza kuwa vifo vya akina mama wanaoenda kujifungua vimepungua kutoka 74 mwaka 2015 hadi 46 mwaka 2020, huku vifo vya watoto wachanga vikipungua kutoka 1,340 mwaka 2015 hadi vifo 586 mwaka 2020.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Agosti 19, 2020 ilieleza kuwa kiwango cha wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka kutoka akinamama 1,226,707 (asilimia 64) mwaka 2015 mpaka akinamama 1,801,603 (asilimia 83) Juni 2020, ambapo Serikali imevuka lengo la asilimia 80 ililojiwekea katika Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto (2016-2020).
Taarifa hiyo imebainisha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa zaidi ya asilimia 71 ukilinganisha na vifo vilivyotolewa taarifa kupitia utafiti mwaka 2015/2016 (TDHS), huku vifo hivyo vikitarajiwa kupungua zaidi mwaka huu na kuwa chini ya vifo 190 kwa vizazi hai 100,000 ukilinganisha na vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 kama ilivyotolewa taarifa kwenye utafiti wa mwaka 2015/16.
Pia imeonyesha kuwa vifo vya watoto wa umri chini ya mwaka mmoja vilikuwa vifo 9 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2019/20, huku vifo vya watoto wachanga vikiwa 7 kati ya vizazi hai 1,000, ambapo takwimu za utafiti wa mwaka 2015/16 ilikuwa vifo 25 kati ya vizazi hai 1,000.