24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Ufuatiliaji na uteketezaji umedhibiti bidhaa zisizotakiwa Kanda ya Ziwa

Na Aveline Kitomary

Maabara ni sehemu muhimu zaidi katika kufanya vipimo,tafiti na majaribio mbalimbali ikiwemo ya dawa.

Ili kuweza kupata bidhaa bora hasa za dawa, chakula, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu kuwa na maabara zenye viwango na uwezo wa kufanya vipimo hivyo kwa ufanisi.

Hapa nchini Mamlaka ya Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi(TMDA) imekuwa na nafasi kuwa katika kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa kabla ya kutumika.

Kaimu mkuu maabara ya TMDA Kanda ya Ziwa, Bugusu Nyamweru(kushoto) akieleza jinsi mashine ya kusafisha vifaa tiba inavyofanya kazi kuliani ni mchunguzi wa maabara, Godfrey Marwa

Mamlaka hii imeendelea kujiimarisha kwa kuwa na maabara ya kisasa na yenye uwezo mkubwa katika upimaji ukanda wa kanda ya ziwa.

Maabara ya TMDA, kanda ya ziwa ilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kutoa huduma katika maeneo makuu mawili , upande wa maicrobiolojia na upande wa kemia.

Maabara hiyo ambayo imesheheni mashine za kisasa inajumla ya watumishi sita ambapo kwa upande wa microbiolojia wapo wawili na upande wa kemia wanne.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa maabara hiyo, Bugusu Nywamweru, Maabara hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa dawa katika kipindi chote hadi sasa.

Anaeleza “Vile vile maabara hii ipo mahususi kwaajili ya uchunguzi wa aina mbalimbali za vipukusi tuna mitambo ya kisasa ambayo inawezesha kufanya uchunguzi wa aina mbalimbali za sampuli kutoka maeneo mengi ya kiutafiti.

“Tuna mitambo ya kisasa kama liquid cromatography mass (LCMSMS),High Performance Liquid Chromatragraphy(HPLC) na pia kuna Microwave Plasma Atomic Emission Spectroscopy (MPAES).

“Mashine hizo zimewekwa kwa gharama ya takribani Sh bilioni tatu ambao ni uwekezaji mkubwa katika maabara hii na taasisi yetu,” anasema Nyamweru.

Kaimu Menja wa TMDA kanda ya ziwa Sophia Mziray akieleza namna wanavyofanya ufuatiliaji na ukaguzi wa bidhaa.

Nyamweru anasema Maabara hiyo imekuwa ikifanya uchunguzi wa dawa hivyo wamefanikiwa kuchunguza na kug’amua baadhi ya dawa ambazo zilikuwa na matatizo katika viwango au kuathirikiwa hivyo kuweza kusaidia viwanda husika kufanya marekebisho.

“Kipindi cha miaka mitatu tumeweza kupima jumla ya sampuli 860,”anabainisha.

TARATIBU ZA UCHUNGUZI

Nywamweru anasema katika uchunguzi kuna wateja wa aina mbili ambao ni wateja wa ndani ikijumuisha wakaguzi wa mamlaka na wateja wa nje ambao ni wenye viwanda au watengenezaji wa bidhaa.

“Sampuli zinavyoletwa zinapokelewa kwa utaratibu katika mfumo wa kielektroni, tuna mfumo unaoitwa ‘lims labatri information management system’, zitapokelewa na wataalama na kisha kuingizwa kwenye mfumo na kutunzwa stoo kama zitakuwa zimekidhi vigezo vinavyotakiwa ili ziweze kufanyiwa uchunguzi.

“Zinapohitaji kuchunguzwa mtaalamu wa uchunguzi atachukua sampuli na kuzipeleka maabara kwaajili ya uchunguzi na zoezi la uchunguzi linapokamilika mtaalamu husika atachukua majibu na kuingiza katika mfumo wa kielektroniki na kisha kuhakikiwa na mchunguzi mwingine mwenye utaalamu sawa au zaidi yake kwaajili ya kujiridhisha kama taratibu zote za kiuchunguzi zimefatwa,” amasena.

Anasema baada ya kukamilika kwa uhakiki endapo hakutakuwa na tatizo katika mfumo wa majibu yatawasilishwa kwa msimamizi wa maabara au Mkurugenzi kwa ajili ya kuhakiki na kutoa kibali cha kuandaliwa cheti cha majibu ya uchunguzi kupelekwa kwa muhusika.

UFUATILIAJI NA UKAGUZI

TMDA hufanya ukaguzi elekezi wa majengo mapya ya kutengenezea, kuhifadhi na kuzuia dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kaimu Meneja wa TMDA kanda ya Ziwa, Sophia Mziray, anasema ukaguzi huo unalenga kutoa ushauri wa kitaalamu wa kuanzisha na kujenga viwanda, maduka na maghala ya kuhifadhia bidhaa ili kuendana na matakwa ya uzalishaji bora, uhifadhi na utunzaji bora na salama wa bidhaa.

“Tumekuwa tukifanya ukaguzi wa kina wa bidhaa katika maeneo yote ya mikoa sita mara mbili kwa kila Mkoa na Halmashauri zake ili kuhakikisha bidhaa zinaendelea kuzalishwa, kuhifadhiwa na kutolewa kwa utaratibu zikiwa bora na salama na zenye ufanisi.

“Vilevile tunahakikisha kuwa bidhaa zilizopo sokoni ni zile ambazo tumezisajili na kupewa kibali cha kutumika na TMDA, endapo tutakuta bidhaa duni au bandia tutaviondoa sokoni na kuchukua hatua stahiki za kisheria,”anasisitiza Mziray.

Mziray anasema kuwa mamlaka hiyo pia inafanya ukaguzi maalum baada ya kupata taarifa ya uvunjifu wa sheria kwa wafanyabiashara wasio waaminifu.

“Tumekuwa tukipokea taarifa za utunzaji na uuzaji wa bidhaa zisizo na usajili au bandia kutoka kwa wananchi na watu wanaofanya biashara hii haramu huchukuliwa hatua stahiki za kisheria na bidhaa hizi huteketezwa.

“Pia tunafanya ukaguzi wa kiuchunguzi kuwa baini wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaingiza au kuuza bidhaa zisizosajiliwa ,tumekuwa tukibaini uvunjaji wa sheria kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wanabadili lebo kwa bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi na kuzirudisha sokoni kwaajili ya matumizi.

“Shughuli za ukaguzi zinafanyika kwa kushirikiana na wakaguzi katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri waliotambuliwa na TMDA kwa kupewa vitambulisho baada ya kupata na kufaulu mafunzo ya ukaguzi yanayotolewa,”anabainisha Mziray.

Anasema ukaguzi unalenga maeneo yanayotengeneza dawa ,vifaa tiba,vitendanishi na vipukusi,maeneo ya kuuza dawa,maeneo ya kuhifadhi(maghala) na maeneo kama hospitali,zahanati,vituo vya afya na maabara.

Mziray anaeleza kuwa mamlaka hiyo inajukumu la kufanya ukaguzi katika vituo vya forodha vya mipakani .

“TMDA imeweka wakaguzi wake ambao hufanya ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuziruhusu kuingia au kutoka nje ya nchi, mkaguzi hukagua bidhaa na nyaraka zote ikiwemo kibali cha TMDA kwa mfumo wa TMDA import and export online portal/scanning QR code, kupitia mfumo huo tumedhibiti matumizi ya vibali vya kughushi kwa wafanyabiashara wasio waaminifu.

“Mkaguzi anaweza kujihakikishia uhalali wa nyaraka zingine zilizoambatana na mzigo wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa mfumo unaoitwa Tanzania Customs Integrated System(TANCIS),”anaeleza Mziray.

Mziray anatoa rai kwa wafanyabishara wanaotaka kuanzisha viwanda na maduka ya dawa kuwasiliana na TMDA ili kupata ushauri .

“Vile vile nawaasa wafanyabishara wasio waaminifu kuacha kufanyabiashara haramu ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi watambue kuwa TMDA iko macho na inaendelea kuweka nguvu kubwa kuwabaini na kuwachukulia hatua stahiki,”anamalizia Mziray.

UTEKETEZAJI DAWA/VIFAA TIBA

Mkaguzi wa Dawa wa TMDA Kanda ya Ziwa, Mtani Njegere, anasema sababu za kuteketeza dawa na vifaa tiba ni kukosa sifa na baadhi ya dawa kubainika kuwa ni dawa bandi au kutokukidhi mahitaji ya magonjwa.

“Lakini pia kuna dawa ambazo zinahifadhiwa vibaya hivyo utakuta imehifadhiwa katika mazingira ambayo karibu dawa zote zina masharti ya kuhifadhi inaweza kushindwa vigezo.

“Uteketezaji wa dawa na vifaa tiba uko wa aina mbili kuna uteketezaji wa hiari kutoka kwa wafanyabiashara lakini pia kuna uteketezaji usio wa hiari, wa hiari ni ile ambayo mfanyabiashara akibaini muda wa matumizi umekwisha watakuja kuomba kwamba wanahitaji kuteketeza bidhaa hizo.

“Lakini kuna bidhaa ambazo zinateketezwa bila hiari tunafanya ukaguzi sehemu mbalimbali na tunaweza kubaini kuwa zipo dawa hazikidhi viwango hizi zinaweza kuwa zimehifadhiwa vibaya au dawa bandi au sababu zozote zinazokosesha sifa hizi tunazikamata na kufanya utaratibu wa kuteketeza,”anafafanua Njegere.

Jengo la TMDA Mwanza

Anaeleza kuwa kila uteketezwaji unazingatia sheria iliyowekwa huku hatua mbalimbali muhimu zikifatwa.

“Kama mfanyabiashara kafanya maombi ya kuhitaji kuteketeza hatua hiyo huambatana na dawa au vifaa tiba vinavyohitaji kuteketezwa na orodha inakuwa na taarifa muhimu kama jina la biashara ya dawa,jina halisi la dawa, nguvu ya dawa.

“Vitu vingine ni toleo la dawa ,tarehe ya kuisha muda wa matumizi,aina ya dozi, kiasi cha dawa, thamani ya dawa na sababu ya kuteketeza.

Anabainisha kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia maombi yanaweza kufanyika kwa njia ya mtandao baada ya kuwasilishwa wakaguzi huandaa kuthibitisha taarifa ya vitu vilivyowasilishwa,wakaguzi pia hupendekeza njia bora ya uteketezaji wa dawa kutokana na aina ya dawa.

“Ukaguzi wa kuridhisha hufanyika na taarifa zote hujazwa katika fomu (verification formu) kwahiyo mfanya biashara akileta taarifa tunajiridhisha kwani kuna wafanyabiashara wasio waamini wanaweza kukisia thamani ya dawa anaweza kukuambnia dawa ni Sh milioni 80 wakati ni Sh milioni 15 na mwisho tunatoa cheti cha uteketezaji kinachtambulika kisheria yenye taarifa sahihi.

“Iwapo bidhaa zitadhibitishwa pamoja na thamani mamlaka huamua mahali ambapo bidhaa zitateketezwa na kumtaarifu mfanyabiasha kwa barua pia taarifa zitatolewa kwa mamlaka ya usimamizi wa eneo ambalo uteketezaji utafanyika ili kukamilisha zoezi,”anaeleza Njegere.

Kwa mujibu wa Njegere Mamlaka huwajibika kuzitaarifu Mamlaka zingine ambazo zinashiriki katika zoezi la uteketezaji wa bidhaa ambazo ni jeshi la polisi, mfamasia wa halmashauari,afisa mazingira, usalama wa taifa na mwakilishi wa mmiliki wa dawa.

“Uteketezaji huzingatia mwongozo wa uteketezaji dawa nchini mamlaka pia huzingatia sheria ya baraza la mazingira nchini (NEMC) kutokana na tabia za dawa mbalimbali mamlaka inawajibu wa kuanisha namana ya uteketezaji wa dawa fulani ili kuhakikisha usalama wa mazingira na viumbe hai hulindwa.

“Mamlaka hujaza fomu maalum ikieleza njia iliyotumika kuteketeza dawa, eneo, uzito na thamani halisi na fomu itasainiwa na maafisa waliosimamaina na mwakilishi wa mmiliki.

“Tunazingatia njia sahii ya uteketezaji ili kuhakikisha uteketeza unakamilika na bidhaa zimeharibika kwa asilimia 100, kuhakikisha kuwa havina tena madhara kwa mazingira na viumbe, kuhakikisha zoezi zima halizalishi kemikali au mazao yanaweza kuathiri mazingira na viumbe.

Anaeleza kuwa kutokana na utofauti wa dawa zipo ambazo zikichomwa kwenye mazingira moshi unaleta madhara kwa watu na viumbe na mazingira.

“Unaweza kutumia joto la juu yenye nyuzi 850 au 1000 au tunaziweka katika mfumo ambao dawa haiwezi kusambaa tunaita ‘mobilization’ mfano unaweza kutuchua vidonge ukaweka kwenye maji ukakoroga halafu utaweka simenti baada ya muda itakuwa kama jiwe hii inaitwa ‘mobilization’ hata mvua ikinyesha hazitatoka,”anafafanua Njegere.

Anasema dawa za kimiminika zinateketezwa kwa kutumia mabomba maalum zinazoitwa ‘sewer’ na pia wanaweza kuzibadilisha dawa kutokuwa na madhara katika mazingira.

“Kama dawa za Kansa hizi zinahitaji kuteketeza kwa nyuzi joto za juu sana hivyo tunazingatia hayo mambo yote.

“Kutokana na dawa zinazoteketezwa zinakidhi sifa katika vinu mara nyingi tunatumia kinu cha hospitali ya Bugando ambacho kinazalisha joto la juu, kutokana na madhara ya dawa katika mazingira hata kama eneo hilo hawakai watu hatupaswi kuteketeza katika mazingira ya wazi kwasababu mvua ikinyesha inaweza kusambaza dawa .

“Na hivyo tunaishi kando ya ziwa kubwa sana na mvua ikinyesha inaweza kupeleka katika ziwa na huko kuna viumbe kama samaki utakuta mtu anatumia samaki kama kitoweo halafu zinadawa madhara yake mengine ni kujenga usugu wa dawa,” anasema.

Anabainisha kuwa mamlaka pia inaelimisha jamii kuhusu mwongozo wa utunzaji salama na utiaji taarifa pindi dawa zinapoharibika.

“Tunajua kuwa kwenye vituo vya afya na zahanati kuna zile dolani za kuteketeza taka za dawa lakini zipo za aina nyingine kuna zingine uchafu tu wa kawaida wa vitu vinavyotumika hospitali lakini zile hata zikiteketezwa katika joto la kawaida haziwezi kuacha madhara lakini dawa lazima ziteketezwe na mamlaka,”anafafanua Njegere.

ONYO KWA WANAOTUPA DAWA OVYO

Zipo dawa ambazo zinabaki majumbani baada ya muhusika kutomaliza dozi kama inayoelekezwa.

Dawa hizi mara nyingi hutupwa hovyo bila kuelewa madhara yake kwa afya na mazingira.

Njegere anatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kutupa dawa hovyo pindi zinapobaki na badala yake wazirejeshe maeneo ya huduma za tiba ili ziweze kuteketezwa kwa njia salama.

“Kuna dawa ambazo ziko majumbani,wengine wakipona wanaziacha afu unakuta baadhi wanazitupa hovyo.

“Natoa rai kwamba wakati wanapokuwa na mabaki ya dawa wawasilishe katika maeneo ambayo yanatoa huduma za tiba lakini pia katika maduka ya dawa wazirudishe ili wao waweze kuwasiliana na sisi wakati wa uteketezaji dawa walizonazo.

“Kutupa dawa kwenye mazingira au kwenye maji au eneo lolote inaathari kubwa kwa sisi wanadamu athari kama usugu wa vimelea ,Mwananchi akipewa dawa tunasisitiza atumie kama alivyoelekezwa na dakari wake kwahiyo zinatakiwa kwisha,”anasisitiza Njegere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles