RAMADHAN HASSAN– DODOMA
BAADA ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kukamilisha mchakato wa kuchuja na kuteua majina matatu ya makada waliotia nia ya kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa urais Zanzibar, hatimaye leo Halmashauri Kuu (NEC) itakamilisha mchakato.
Mchakato huo utahitimishwa kwa kupiga kura na kupata jina moja ambalo litakwenda kuthibitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa utakaofanya vikao vyake Julai 11-12 jijini Dodoma.
Katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, wajumbe walichambua mapendekezo ya majina hayo matatu yaliyofika kwao.
Hadi tunakwenda mitamboni bado majina hayo yalikuwa hayajajulikana kutokana na chama hicho tawala kubadili mfumo wake wa ndani ikiwamo kulinda na kuenzi siri ya vikao.
Mchakato huo ulianza kwa kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kujadili majina ya makada wake 31 walioomba na kurudisha fomu za kuomba kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Majina hayo yalifikishwa mbele ya Kamati Kuu na kisha NEC kwa uamuzi wa mwisho kabla ya jina moja kufikishwa mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Julai 11 kuthibitishwa na Mkutano Mkuu
Julai 4, mwaka huu viunga vya mji wa Zanzibar vilikuwa na ukimya na shauku ya kujua nani wametinga tano bora ya CCM kwa urais wa Zanzibar mwaka huu.
Saa chache baada ya kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, baadhi ya majina yalianza kusambaa, wakitajwa Dk. Khalid Salum Mohamed, Khamis Mussa Omar, Dk. Hussein Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha na Profesa Makame Mbarawa kuwa wamepenya kwenye tano bora na sasa wanasonga mbele kwenye vikao vya maamuzi kuamua nani awe mgombea wa urais.
Pamoja na hali hiyo, baadhi ya wahafidhina ndani ya CCM, hasa upande wa Zanzibar, wamekuwa wakihoji hatua ya chama hicho kwenda na majina hayo na kuacha makada wengine ambao kwa namna moja au nyingine nao walistahili kuingia tano bora.
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ulianza Juni 15 hadi 30, mwaka huu ambapo jumla ya makada 32 walijitokeza kuchukua fomu ambao ni Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Jafar Jumanne Mohamed Hijja Mohamed, Issa Suleiman Nassor.
Wengine ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohamed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk. Khalid Salum Mohamed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni Mohamed Aboud Mohamed, Bakari Rashid Bakar.
Pia wapo Mgeni Hassan Juma, Ayoub Mohamed Mahmoud, Hashim Salum Hashim, Fatma Kombo Masoud, Hasna Attai Masoud, Maalim Hamad Idd Hamad Idd, Pereira Ame Silima, Shaame Mcha, Mussa Aboud Jumbe na Moudline Cyrus Castico.
KAULI YA POLEPOLE
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, iliketi jana kupokea taarifa kutoka Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu Zanzibar.
“Ni kweli kabisa kimeketi kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa chini ya Rais na Mwenyekiti wetu, John Magufuli na ninachoweza kuwaambia kwa sasa mazingatio yote ya kikatiba na kikanuni yamefanyiwa kazi kwa maana imepokelewa taarifa kutoka Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu kule Zanzibar.
“Na pia imepokelewa Sekretarieti kutoka Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na kwa pamoja imepokelewa Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM Taifa.
“Na kikao kimefikia uamuzi ambao utawasilishwa kesho (leo) kwenye kikao cha Halmashauri Kuu Taifa ambacho ndiyo yenye dhamana ya kupiga kura kwa mapendekezo ambayo yametafakariwa,” alisema Polepole.
Alisema pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, imezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweza kusimamia vizuri masuala ya uchumi hadi kufikia uchumi wa kipato cha kati.
“Lakini pamoja na mambo ya kiuchaguzi, kamati imetoa pongezi kubwa kwa Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania kwa kuuweka vizuri uchumi, bado nchi yetu imepiga hatua na kuingia katika uchumi wa kati, kwa kauli moja imepongeza sana Serikali zake mbili,” alisema Polepole.
MSISITIZO WA DK. BASHIRU
Juzi Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema kuwa mchakato unaoendelea wa kumteua mgombea urais jijini Dodoma ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Uhai Tv, kuhusu malalamiko ya mgombea urais wa Zanziabar kuchaguliwa na wajumbe wa Bara.
Alisema mgombea urais wa Zanzibar huchaguliwa na wanachama wa CCM visiwani humo, kisha huthibitishwa na vikao vya chama hicho, bila kujali wajumbe wake wanatoka Bara ama Zanzibar.
“Mchakato wa kupata mgombea urais wa Zanzibar huanzia uchukuaji fomu na wanaohusika ni wanachama wa CCM Zanzibar kwa mujibu wa sheria, baada ya hapo hatua ya uteuzi huanza, kuanzia vikao vya Halmashauri Kuu.
“Mchakato upo kwa mujibu wa katiba na unakidhi matakwa ya kikataiba ya CCM na ya nchi,” alisema Dk. Bashiru.
Alifafanua kuwa wenye mamlaka ya kumchagua Rais wa Zanzibar ni Wazanzibari wenyewe, ambao huchagua mtu wanayemtaka katika Uchaguzi Mkuu wa Rais.
“Vyama vya siasa vinateua wagombea, vyama havichagui rais, Rais wa Tanzania huchaguliwa na Watanzania na wa Zanzibar huchaguliwa na Wazanzibari wenyewe, kinachofanyika CCM ni mchakato wa uteuzi, si uchaguzi,” alisema Dk. Bashiru.
Aidha katika hatua nyingine, alisema kuwa hana sababu za kujadili zaidi mjadala huo kwa kuwa hautokani na wanachama wa CCM, bali unavumishwa na watu ambao sio wanachama wa chama hicho.
“Hao sio wana-CCM, CCM wanaamini katika utaifa na umoja, ndani ya CCM kuna wanachama na si Wazanzibari au Bara, kila mwanachama ana haki na wajibu sawa na kila wanapokaa ni kikao baina ya wana CCM.
“Na kama si wana CCM wanaotoa malalamiko hayo, sina sababu ya kujadili mawazo yao na hayawezi kuwepo. Siyo tu katiba hairushusu ubaguzi, lakini pia ndani ya CCM tunakuwa kama wanachama na mambo yetu yanaendeshwa kama wanaCCM, wanaoamini katika utaifa hawawezi wakasema hivyo,” alisema Dk. Bashiru.