26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa, Mbowe wavutana mikutano ya hadhara, tume huru ya uchaguzi

Ramadhan Hassan – Dodoma

HOJA ya tume huru ya uchaguzi na kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara imeibuka bungeni, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema tume ni huru wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akisema majibu hayo ni mepesi.

Mjadala huo uliibuka jana bungeni wakati Mbowe alipouliza swali wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Hoja ya tume huru ya uchaguzi imeibuka siku za hivi karibuni na juma lililopita ilichagizwa na Ubalozi wa Marekani nchini, ambao ulimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa ahadi aliyoitoa kwa mabalozi kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa amani, huru na haki huku ukisema unatarajia pia kutaundwa tume huru ya uchaguzi.

Jana katika swali lake, Mbowe alihoji ni lini Serikali itaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi ili kujiandaa na Uchaguzi Mkuu, huku pia akitaka kujua mpango wa Serikali kuhakikisha kunakuwa na tume huru ya uchaguzi.

 “Ni miaka minne sasa tangu Serikali yenu imeweka zuio kwa vyama vya siasa kufanya wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya nchi na tunavyozungumza leo (jana) ni siku 262 zimebaki kufika Oktoba 25, siku ambayo nchi yetu ifafanya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

“Kwa busara zako binafsi katika Serikali ambayo wewe ni kiongozi mwandamizi, unafikiri ni lini mtaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi kujiandaa na Uchaguzi Mkuu?” aliuliza Mbowe.

MIKUTANO YA HADHARA

Akijibu, Waziri Mkuu alisema vyama vya siasa havijazuiliwa kufanya shughuli zake ila umewekwa utaratibu muhimu kwa viongozi waliopata ridhaa kwenye maeneo yao na ratiba za uchaguzi zitatolewa na kueleza lini shughuli za kampeni zitaanza.

“Lakini pia lini tutajiandaa kwa ajili ya uchaguzi? Ratiba za uchaguzi zitatolewa na ratiba zile zitaeleza kuanzia lini, shughuli za kampeni zitaanza lini ili vyama vikaeleza sera zake kwenye maeneo yote ili sasa wananchi waweze kupata fursa ya kuendelea kufanya maamuzi ya sera ipi, ya chama gani inafaa kutuletea maendeleo nchini.

“Kwa hiyo hilo linaendelea na wote mnajua hata kulipokuwa na chaguzi ndogo, ratiba ilipokuwa inatolewa na kila chama kilikuwa kinaendelea kushiriki na huo ndio utaratibu ambao unaifanya hata nchi kuwa imetulia na watu wote kufanya shughuli zao kama kawaida na tutaendelea kufanya hivyo kwa vyama vyote,” alisema Majaliwa.

TUME HURU YA UCHAGUZI

Kuhusu tume huru ya uchaguzi, Majaliwa alisema jambo hilo pia lilitolewa majibu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama na yeye anarudia kwamba tume ya uchaguzi ni huru.

“Mimi nataka nirudie tu kwamba tume hii imeundwa kwa mujibu wa katiba, na kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi kipengele 78, 74 na kipengele kidogo cha 7, 11 na 12 kinaeleza kwamba hiki ni chombo huru.

“Kimeelezwa pia kwenye katiba pale kinaundwaje na chombo hiki hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote, iwe Rais wa nchi, iwe chama chochote cha kisiasa au mamlaka nyingine yoyote ile haipaswi kuingilia.

“Kama ni chombo huru kwa mujibu wa katiba, ndio tume huru! Sasa kunaweza kuwa kuna tofauti ya neno huru hili tunataka itambulike vipi, chombo kipo, kinajitegemea na kinafanya kazi yake bila kuingiliwa na mtu yeyote kwa mujibu wa katiba yetu ya mwaka 1977,” alisema Majaliwa.

SWALI LA NYONGEZA

Spika wa Bunge, Job Ndugai alipompa Mbowe nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, alidai majibu ya Waziri Mkuu ni mepesi na kuna siku watakuja kujuta kutokana na majibu hayo.

“Unajua vizuri sana, Serikali yako inajua vizuri sana, Watanzania wanajua vizuri sana kwamba vyama vya siasa vya upinzani vimezuiwa kwa miaka minne sasa na unapotupa maelezo ndani ya Bunge ya kuhalalisha kilichofanyika unasema ni utaratibu ambao mmejiwekea, mmejiwekea kwa sheria ipi?

“Unajua yote hayo vizuri sana kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi unayoiita ni huru kwa sababu imeandikwa katika katiba sio huru na watendaji wake vile vile wamekuwa ni ‘part’ (sehemu) na masuala haya yamejitokeza wazi na yanaonekana.

“Haya ni majibu mepesi ambayo kuna siku mtakuja kujuta katika nchi hii kwa majibu haya mepesi, je hamuoni muda mwafaka sasa Serikali ikaona umuhimu wa wadau mbalimbali ambao wanahusika na masuala ya uchaguzi katika nchi hii ya kutafuta njia bora kwenda kwenye uchaguzi kuliko kwenda kibabe kwa namna ambayo mnataka kwenda?” aliuliza Mbowe.

UFAFANUZI WA HOJA

Akimjibu Mbowe, Waziri Mkuu alikanusha kwamba Serikali inaongoza kibabe ambapo alidai kwamba wanalenga kulifanya taifa liwe na usalama.

“Mbowe ni kiongozi, tunazungumza, tunabadilishana mawazo, lakini sote tunabadilishana mawazo, tunalenga kulifanya taifa hili liwe na usalama, liwe tulivu ili shughuli zetu ziweze kwenda, lakini muhimu zaidi Watanzania wanahitaji maendeleo na kwa maana hiyo tunapoweka utaratibu wa namna ya kuwafikia wananchi na kupata maendeleo, jambo hili si la chama kimoja ni la nchi nzima.

“Hakuna mbunge wala diwani kwenye eneo lake amezuiwa asifanye siasa na watu wake, kunaweza kuwa labda kuna tatizo mahali fulani, lakini kwa utaratibu ule tunaozungumza tunakutana, tunazungumza wapi kuna shida, lakini wiki iliyopita Sugu (Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi) alieleza kule Mbeya anazuiwa na OCD, na mimi nilimwita hapa tumezungumza, mkuu wa mkoa ameungana nae.

“Mkuu wa polisi mkoa ameungana nae. Shida kama ziko kwenye ngazi ndogo ndogo huko ni suala la kuzungumza kwenye eneo hilo na pale ambako kuna shida ya namna hiyo tuendeee kuwasiliana,” alisema Majaliwa.

Kuhusu tume kuonwa sio huru, Majaliwa alisema huo ni mtazamo wa mtu na kwamba tume hiyo imekuwa huru na wala hawajawahi kuona mtu yeyote akiingilia wala chama cha siasa.

“Suala la tume hii kuonwa kwamba si huru ni mtizamo wa mtu, lakini katiba na utendaji wake iko huru na pale ambako kunaonekana kuna shida, basi kwa utaratibu ule paelezwe kwamba hapa kuna shida, lakini hatujawahi kuona Rais akiingilia, chama cha siasa kikiingilia, ile tume iko huru na inafanya kazi yake kama ambavyo imetakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ukiwa na jambo lolote lile unao uhuru wa kubadilishana mawazo ili tuone wapi tunaweza kusaidia kufanya jambo hilo liweze kwenda sahihi,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles