27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Kesi za uhujumu uchumi zatawala Wiki ya Sheria

Nora Damian Na Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MAADHIMISHO ya Siku ya Sheria yamefanyika huku suala la kuchelewa kwa upelelezi wa kesi likitawala ambapo Rais Dk. John Magufuli, Jaji Mkuu na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamelizungumzia kwa namna yao.

Suala hilo limetajwa kuchangia watu wengi kukaa mahabusu muda mrefu na kusababisha kupokwa haki zao kinyume na ibara ya 14, 15 (i) na 15 (ii) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo jana, aliwanyoshea kidole wapelelezi na kuwataka wabadilike.

“Kila siku wakienda wanasema upelelezi unaendelea, ameshapeleleza, ameshamshika na meno ya tembo huku anazungumza upelelezi unaendelea.

“Ninaomba wapelelezi na wasimamizi wa sheria hili mlifanyie kazi, watu wanateseka, ukienda kwenye magereza watu wanalia na wengine ni kesi za kusingiziwa.

“Wako watu wamewekwa kwa sababu ya matajiri kwamba nakukomesha utakwenda kwanza mahabusu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuwa hadi sasa magereza yana watu 32,208 na kati yao wafungwa ni 13,455, mahabusu 17,632 hali inayodhihirisha kuwa tatizo la ucheleweshaji kesi bado lipo.

Alilitaka Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), kuharakisha upelelezi wa kesi kwani wanawanyima watu haki.

“Ndugu zangu wapelelezi ufalme wa mbinguni utakuwa shida kwenu msipotubu na kumrudia Mungu kwa sababu roho za watu wasio na hatia zinaangamia, na wala msiwasingizie mahakimu, majaji kwa sababu hamuwapelekei.

“Saa nyingine kupelekwa mahakamani lazima uhonge ili kesi yako ikasomwe, mnawapa shida mahakimu, majaji, lakini mnawapa shida watu wanaowekwa kule.

“Nawaambia ukweli badilikeni, ninawaomba viongozi wa dini kaliombeeni suala hili, hao wanaochelewesha kwa makusudi wakapate laana,” alisema Rais Magufuli.

Pia aliagiza mabaraza ya ardhi yaangaliwe kwa umakini kwa sababu yanachafua sura nzuri ya mahakama.

“Mahakama inafanya kazi nzuri sana, lakini kwenye mabaraza ya ardhi kuna kelele nyingi, wanapindua pindua tu.

“Kuna wenyeviti niliwaweka kwenye orodha ya kuwafukuza nikiwa Wizara ya Ardhi, lakini mpaka leo bado wapo, sasa sifahamu kama walibadilika,” alisema Rais Magufuli.

ATOA BILIONI 10/-

Rais Magufuli pia aliahidi kutoa Sh bilioni 10 kwa ujenzi wa Mahakama Kuu Dodoma.

Alisema katika kipindi cha miaka minne wafungwa 38,801 walisamehewa na kwamba majadiliano yanaendelea kuwarejesha kwao raia 1,415 wa Ethiopia waliofungwa kwa makosa ya uhamiaji.

Kuhusu masilahi ya watumishi alisema; “Mishahara ya watumishi wote si wa mahakama tu haitoshi, hata mimi haunitoshi, huo ndiyo ukweli.”

JAJI MKUU

Awali Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, alisema idadi ya maombi ya dhamana ni kiashiria cha wingi wa mashauri ya uhujumu uchumi ambayo hushughulikiwa upelelezi unapokamilika.

 “Takwimu kutoka mahakama za wilaya na mahakama za hakimu mkazi zinaonyesha idadi kubwa ya kesi za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi bado zimekwama katika hatua za awali kusubiri upelelezi kukamilikakabla ya kuwasilishwa katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kwahiyo hili ni eneo ambalo bado kuna changamoto,” alisema Profesa Juma.

Hata hivyo alisema wamejipanga kuhakikisha mashauri yote yanayosajiliwa yanasikilizwa ndani ya miezi tisa kama inavyoelekezwa katika kanuni ya divisheni hiyo.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, tangu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ianzishwe Julai 2016, mashauri 391 ya maombi ya kawaida na dhamana yamesajiliwa na 385 yamemalizika.

Alisema mashauri 119 ya uhujumu uchumi yamesajiliwa na 89 yamemalizika na kwamba faini ya Sh bilioni 13.6 na fidia ya Sh bilioni 30.6 zimetolewa.

Profesa Juma alisema pia matumizi ya Tehama yamewezesha mahakama kudhibiti ukusanyaji wa tozo na ada mbalimbali na kuongeza maduhuli kutoka Sh bilioni 1.6 mwaka 2017 hadi Sh bilioni 2.5 mwaka huu.

Alisema mwaka jana mashauri 2,435 yalifunguliwa kwa njia ya kielektroniki.

Profesa Juma alisema vifaa vya mawasiliano kwa njia ya video vimefungwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bukoba na Mbeya, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gereza la Keko na kwamba hadi sasa mashauri 60 yamesikilizwa kwa mfumo huo.

Alisema kupitia mfumo huo pia walisikiliza mashahidi waliokuwa katika nchi za Uingereza, Marekani, China na Kenya.

“Kwa Januari mwaka huu mashauri 27 yalisikilizwa kati ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gereza la Keko hatua iliyosaidia na kuokoa muda, gharama na changamoto ya ulinzi,” alisema Profesa Juma.

Kuhusu watumishi, alisema mahitaji ni 10,351 lakini waliopo ni 5,947.

Profesa Juma alisema kuanzia Januari hadi Desemba, mwaka jana watumishi 258 waliondoka kazini na kati yao 162 walistaafu, 39 kufariki, 27 waliacha kazi na wawili waliondolewa kwa sababu za kimaadili.

Aliomba wakubaliwe kuajiri watumishi 268 kwa mahakama mpya zinazoanzishwa zikiwamo Mahakama Kuu Kigoma na Musoma.

Kuhusu mashauri, alisema kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana, mashauri 272,326 yalifunguliwa katika ngazi zote za mahakama na kati ya hayo 271,214 yalisikilizwa na 68,648 yalibaki ambapo 3,776 ndiyo yenye umri wa zaidi ya miaka miwili.

MWANASHERIA MKUU

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi,alisema wanapitia mikataba yote ya kuzalisha umeme, hasa mkataba wa Songas ambao una matatizo makubwa.

Alisema pia wamefanya rejea katika mikataba 182 sambamba na mikataba 70 ya misaada ya mikopo ili kuangalia tija na baadhi ya masharti yaliyomo.

CHAMA CHA WANASHERIA

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk. Rugemeleza Nshalla, alisema kuendelea kutumika kwa mfumo wa jinai wa kikoloni kumesababisha watu wengi kupokwa uhuru wao kutokana na kukaa mahabusu muda mrefu.

“Mfumo wa jinai wa kikoloni ulikuwa na lengo la kumshikilia mfungwa au mahabusu kwa muda mrefu kwa lengo la kuwatia hofu wananchi ili watii amri za kikoloni bila kuhoji.

“Mara kadhaa tumekunuu wewe na watangulizi wako mkihoji suala la kutokamilika kwa upelelezi ilihali mtu amekamatwa na ushahidi.

“Ikumbukwe kuwa muda wa mwanadamu hapa duniani una ukomo na hakuna mwenye uwezo wa kuongeza ila ni Mwenyezi Mungu, kila siku ambayo mtu anapokwa uhuru wake kwa kuwekwa ndani siku hiyo haitarudi.

“Bahati mbaya nchi yetu haina mfumo wa kumfidia mtu ambaye alipokwa uhuru wake na baadaye kesi yake kufutwa au kukutwa hana hatia, na jamii haina mfumo wa kuweza kumlipia,” alisema Dk. Nshalla.

Kwa mujibu wa Dk. Nshala ibara ya 14 ya Katiba inatoa haki ya kuishi wakati ibara ya 15 (i) inasema kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.

“Ibara ya 15 (ii) inataka mtu asishikwe na kuwekwa ndani au kuhamishwa kwa nguvu na kupoteza uhuru wake isipokuwa kwa mujibu wa sheria au anapokuwa ametiwa hatiani.

“Ili kukidhi matakwa hayo, inabidi polisi na waendesha mashtaka kujiridhisha kuwa pale wanapotoa amri ya kushikwa na kuwekwa ndani basi upelelezi uwe umekamilika,” alisema Dk. Nshalla.

Alishauri pia haki ya kupata dhamana iheshimike kwani hadi sasa watuhumiwa wengi wanaokabiliwa na kesi za jinai wako ndani licha ya kuwa makosa yao yanadhaminika.

“Suala hili linahitaji utashi wa kisiasa ili kubadilisha mwenendo huu na pengine kuondokana kabisa na hali hii, kuepusha gharama kubwa za uendeshaji mashauri na kushikilia watuhumiwa kwa muda mrefu.

“Tutafakari kwa makini na kuweka mfumo mzuri wa kushikilia mahabusu na wafungwa kwa muda mfupi zaidi ili nchi yetu isikae na watuhumiwa wengi mahabusu kwa muda mrefu,” alisema Dk. Nshalla.

Kuhusu utungwaji wa sheria alisema kunahitajika mabadiliko makubwa kwani watu wengi bado hawajafahamu adhabu zinazopendekezwa na baadaye kufanywa kuwa sheria.

“Kwa kiasi kikubwa dhana iliyojengeka ni kutoa adhabu kali badala ya kutoa mafunzo kwa mkosaji na wengine ili kuzuia zaidi.

“Sheria iliyojikita kutoa adhabu kali haitoi fundisho, haifaidishi nchi na hutekelezeka kwa upande mmoja ambao ni kumshikilia mtuhumiwa, lakini haitekelezeki upande wa pili ambao ni faini kwa sababu zilizowekwa hazilipiki na kujikuta tunajaza watu gerezani kwa wakosaji kushindwa kulipa faini,” alisema Dk. Nshalla.

Pia alipendekeza zuio la mawakili kufanya kazi katika mahakama za mwanzo liondolewe kwani mahakama hizo hivi sasa zinaongozwa na mahakimu wakazi wenye shahada ya kwanza ya sheria.

“Katazo hili linazuia wananchi wengi kupata huduma ya uwakilishi, mahakama za mwanzo ndizo zinapokea kesi nyingi, hivyo mawakili kufanya kazi katika mahakama hizo kutawezesha wananchi kupata huduma na haki,” alisema Dk. Nshalla.

Pia alitoa wito kwa Serikali jitihada za makusudi zifanyike ili kesi zote ziwe zinarekodiwa kuwezeshwa kusikilizwa kwa kesi nyingi sambamba na mashauri kurushwa moja kwa moja.

“Hivi sasa inasikitisha mahakimu na majaji wanaandika hoja na ushahidi kwa mikono na hii inarefusha muda wa kusikilizwa kwa kesi.

“Katika nchi za wenzetu si hivyo, kwani majaji na mahakimu husikiliza na kuandika hoja kwa uchache, yote yanayofanywa hurekodiwa,” alisema Dk. Nshalla.

Kwa mujibu wa rais huyo, hadi Machi mwaka huu TLS imefikisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwake ikiwa na mawakili 9,372 na kati yao wanaofanya kazi mahakamani ni 8,667 na wanaogonga mihuri ni 14.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,554FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles