22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AKEMEA MAOFISA MISITU

Na MWANDISHI WETU – TABORA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amekemea maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFC) kwa kutoa vibali vya uvunaji misitu bila kuwashirikisha wenzao wa halmashauri.

Majaliwa alikemea hali hiyo kwenye mkutano wake na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora uliofanyika Kata ya Goweko, wilayani humo jana.

Waziri Mkuu alibaini kuwa maofisa hao hawafanyi kazi kwa kushirikiana baada ya kumhoji Ofisa Misitu wa TFS, Juma Kazimoto na Ofisa Misitu wa Wilaya ya Uyui, Jared Nzilorera.

“Hapa kuna uvunaji mkubwa wa misitu. Je, kuna mtu anafuatilia kama wanavuna kwa usahihi?” alihoji Majaliwa.

Akijibu swali la Waziri Mkuu, Kazimoto alisema Uyui hakuna uvunaji, lakini wanaovuna wanatoka Sikonge na wanakwenda wilayani hapo kuuza mbao.

Alipoulizwa Ofisa Misitu wa Wilaya, Nzilorera, ni kwa kiasi gani wanapeana taarifa na mwenzake wa TFS ambao wote wako chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, alitoa majibu ya kujichanganya hali iliyomfanya Waziri Mkuu aamue kukemea tabia yao ya kutoa vibali bila kuwahusisha wenzao wa halmashauri.

“TFS mmejiingiza kwenye kuvuna misitu, na mnawa-over power DFOs (wale wa halmashauri). Hawa walioko kwenye halmashauri ndio wanaolinda misitu yote ambayo iko ndani ya wilaya husika.

“Tatizo hili liko nchi nzima, ni la ushindani kati ya maofisa misitu wa TFS na wale wa halmashauri. Misitu yetu inakwisha sababu mnaimaliza nyie kwa kutoa vibali bila kuwashirikisha wenzenu,” alisema.

Majaliwa alimwagiza Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Queen Mlozi, asimamie suala hilo.

“DC wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, simamia jambo hili na usisitize utunzaji wa mazingira na upandaji miti,” alisema.

Majaliwa alisema ukataji miti ovyo umechangia kukauka kwa vyanzo vingi vya maji. “Mhandisi wa maji anahangaika kuchimba visima, lakini hakuti maji sababu miti imekatwa ovyo na ardhi tepetevu imekauka. Watumishi wote nendeni vijijini mkahamasishe utunzaji wa mazingira,” alisema.

Kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, kila mkoa una ofisa misitu, kila wilaya imeajiri ofisa misitu wa halmashauri na TFS kupitia wizara pia imeajiri maofisa wa misitu  katika ngazi za mkoa na wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles