30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NGOME ZA RAILA ZATIBUKA

NAIROBI, KENYA

MATUKIO ya fujo, uharibifu wa mali na vifo vya watu yameripotiwa kutokea nchini Kenya, katika baadhi ya ngome za aliyekuwa mgombea wa urais kupitia muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga ambaye ameshindwa na Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.

Maeneo ambayo yameathirika na matukio hayo ni Mkoa wa Nyanza na baadhi ya viunga vya Jiji la Nairobi.

Matukio hayo yameripotiwa kutokea muda  mfupi baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza Uhuru kuwa mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumanne iliyopita.

VURUGU

Taarifa iliyochapishwa jana asubuhi na mtandao wa Standard Digital, imesema kwamba Jeshi la Polisi la Kenya limekuwa katika mapambano makali na makundi ya waandamanaji wanaopinga matokeo hayo ya urais katika miji ya Kisumu, Mathare na Kibera.

Katika Kaunti ya Kisumu ambako ni moja ya ngome ya Raila alikopata asilimia 97.9 ya kura zote, polisi wameripotiwa kutumia helikopta kushika doria kutoka angani..

Standard Digital imeripoti kuwa polisi walikusanyika pia kupambana na makundi ya waandamanaji katika miji ya Siaya, Bondo, Homa Bay na Migori.

Inaelezwa kuwa baadhi ya barabara zilifungwa na biashara zimesimama katika maeneo mbalimbali kwa siku nzima ya jana.

Mwandishi mmoja wa Kituo cha Televisheni cha KTN aliyekuwa katika mji wa Kibera, amekaririwa akisema kwamba alikuwa akisikia milio ya bunduki katika eneo alilokuwapo jana asubuhi.

Mwandishi huyo alisema kuwa barabara zote muhimu zinazoingia na kutoka ndani ya Mkoa wa Nyanza zimefungwa na watu wengi wamebaki majumbani mwao.

TAARIFA ZA MAUAJI

Katika hatua nyingine kumeripotiwa taarifa tofauti kuhusu idadi ya vifo vinavyodaiwa kusababishwa na vurugu hizo.

Kutokana na mapambano hayo, Standard Digital imeripoti kuwa watu sita wanahofiwa kupoteza maisha baada ya kujeruhiwa kwa risasi usiku wa kuamkia jana.

Kwa mujibu wa Standard Digital, ilitembelea Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga  na kukuta watu watano wamelazwa kwa kujeruhiwa huku watatu kati yao wakiwa na majeraha ya risasi.

Naye mmoja wa madaktari katika Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga alidai kuona maiti za watu wanne ambao miili yao ilikuwa imejeruhiwa kwa risasi.

Taarifa nyingine zinasema kuwa katika mji wa Siaya mwendesha bodaboda mmoja alikutwa ameuawa karibu na ofisi ya mwakilishi wa wanawake bungeni, Dk. Christine Ombaka.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walidai kuwa mauaji ya kijana huyo yametokana na mapambano baina ya polisi na vijana wa mitaani yaliyotokea usiku wa kuamkia jana.

Taarifa nyingine zilizoripotiwa na BBC jana jioni, zinasema kuwa takriban watu 11 wameripotiwa kuuawa na polisi katika maeneo yanayomuunga mkono Raila Odinga, ingawa waandishi hawajaona ushahidi wa kuthibitisha mauaji hayo.

Kwamba chumba cha kuhifadhi maiti cha kaunti ya Nairobi, kilipokea miili minane.

Watu wengine watatu waliripotiwa kuuawa katika kisa kingine, ikiwemo mtoto wa miaka tisa aliyepigwa risasi kwa bahati mbaya katika Mtaa wa Mabanda wa Mathare jijini Nairobi.

Mtu moja pia ameripotiwa kuuawa mjini Kisumu, ambayo ni ngome ya upinzani na eneo la ghasia za kikabilia wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, zilizosababisha vifo vya takriban watu 1,200 na wengine 600,000 kuachwa bila makazi.

Lakini kwa upande wake, Jeshi la Polisi limepinga taarifa hiyo na kuthibitisha kutokea kwa kifo cha mtu mmoja pekee.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Nyanza, Titus Yoma alisema kuwa taarifa ya uhakika waliyonayo ni ya mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Vincent Ochieng, aliyefariki katika eneo la Dago mjini Kisumu.

Kwa mujibu wa maelezo ya polisi, Ochieng alipigwa risasi na polisi wakati akijaribu kukusanya makundi ya vijana katika soko la Dago.

Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka ndani ya familia ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 19, inadai kuwa ndugu yao alipigwa risasi na polisi wakati akirudi nyumbani baada ya kumaliza kuangalia mechi ya soka ya Ligi Kuu ya England.

WAFARIKI WAKIFURAHIA USHINDI

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini humo, katika mitaa ya Buruburu na maeneo ya Kiambu, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya makundi mawili.

Kundi moja lilikuwa linasherehekea ushindi na jingine likipinga matokeo hayo.

Wakati huo huo, watu wanne wamefariki dunia wakisherehekea ushindi wa Uhuru.

Vifo hivyo vimetokea baada ya kugongwa na magari mawili karibu na mji wa Mahi mahiu.

WAKILI AMSHUTUMU RAILA

Wakili maarufu, Nelson Havi amemshutumu Raila kwa uratibu mbaya wakati wa uchaguzi mkuu kwa kukataa kulinda kura.

Havi alimtaka kiongozi huyo kukubali kushindwa baada ya kushindwa kuwafurahisha wafuasi wake.

Alisema Raila hakuwa na mawakala na nyenzo za kuhakikisha kuwa kura zinalindwa hali ambayo imewaangusha wafuasi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles