Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
SERIKALI imeagiza hadi ifikapo Desemba 30, sura ya upatikanaji wa vazi la taifa iwe imeanza kujionesha.
Agizo hilo limetolewa jijini hapa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipokuwa akifunga Tamasha la Urithi, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza, Majaliwa aliiagiza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuhakikisha wanakamilisha haraka mchakato huo.
“Nikiwa hapa nimeangalia kila kabila na watu wamevaa mavazi yao ya kiutamaduni, tofauti hii ni nzuri. Lakini hadi sasa bado hatujaunganishwa na vazi la taifa letu kama ilivyo kwa mataifa mengine.
“Naagiza hadi Desemba 30, mwaka huu Wizara ya Habari shughulikieni jambo hili haraka, mje na sura halisi ya upatikanaji vazi la taifa. Pia kwa Desemba hiyo hiyo nitakuja kuona tamasha la mfano la vazi la taifa,” alisema.
Kuhusu vazi la kabila la Maasai, alisema tayari limefanikiwa kutambulika duniani na kuingia katika sekta ya utalii.
“Ni vyema kila kabila likaingiza vazi lake la utamaduni kwenye tamasha hili la urithi, lakini ni muhimu zaidi tukawa na vazi letu la taifa linalotuunganisha wote,” alisema.
Akitoa maagizo kwa watendaji wanaohusika na uandaaji wa Tamasha la Urithi, aliwataka waweke utaratibu matamasha kama hayo kufanyika upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
“Wananchi wa Tanzania Bara wanahitaji kuona utamaduni wa wenzao wa Zanzibar kama ilivyo kwa Tanzania Bara, hivyo basi kaangalieni upande gani uhusike kufungua tamasha na mwingine kufunga,” alisema.
Alizitaka wizara zinazohusika kukaa kwa pamoja kuratibu jambo hilo ili wananchi walifahamu na kushiriki kikamilifu mwakani.
Alisema kufanyika kwa tamasha hilo ni moja ya jitihada za Serikali kuutangaza utalii na kuongeza watalii wanaotembelea nchini kila mwaka.
“Mwaka 2015 tulipokea watalii zaidi ya milioni 1.2, lakini malengo yanatutaka kufikia watalii milioni 2 ifikapo mwaka 2020 na lengo hili linatekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Tamasha hili ni moja ya kichocheo cha kudumisha tamaduni, mila, mavazi, vyakula vyetu. Lakini pia litaongeza ajira kwa vijana na kuingiza mapato kwao na Serikali,” alisema Majaliwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Josephat Hasunga, alisema hadi sasa mapato yanayotokana na utalii hayalingani na aina ya vivutio vilivyopo nchini.
“Kwa sasa tumeamua kuvitambua vivutio vipya na kuanzisha mazao mapya ya utalii ukiwamo utalii wa miamba kwa maeneo kama Ngorongoro,” alisema Hasunga.
Alisema kufanyika kwa tamasha hilo kutaendelea kutoa nafasi kwa wananchi wa makabila mbalimbali kutangaza vivutio vyao, pia kutangaza utalii kuongeza mapato na ajira.
“Tumehitimisha hapa Arusha, naamini tamasha lijalo mwakani litaboreshwa zaidi,” alisema Hasunga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alimweleza Majaliwa kuwa mkoa huo unaendelea na jitihada za kuongeza vivutio vya utalii.