23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AAGIZA WALIMU KUHAMIA SHULENI

NA MWANDISHI WETU – RUANGWA


kassim-majaliwaWAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza walimu wanaoishi mbali na shule zao wahame na warudi kupanga katika nyumba za jirani.

Agizo hilo alilitoa wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chingumbwa, Kata ya Mbekenyera wilayani Ruangwa juzi.

Alisema haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwa sababu hali hiyo inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.

“Nimeambiwa kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo (jana), walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo.

“Uamuzi wa walimu kuishi jirani na shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na kuwasimamia wanafunzi wakati wakifanya usafi na wakati mwingine aweze kutoa msaada kwa wanafunzi wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au ufafanuzi,” alisema Majaliwa.

Pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue, asimamie mpango huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.

Alisema ili kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila kijiji kikaweka utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza ujenzi wa nyumba za walimu.

Akiwa katika Kijiji cha Mkutingome, Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100 kutoka kila kaya ili yapatikane 40,000 yatakayotumika kujenga zahanati ya kijiji hicho, huku yeye aliahidi kuwachangia mabati 150 ambayo kati yake, 100 yatatumika kuezekea zahanati hiyo na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba ya mwalimu iliyokaa kwa muda mrefu bila kumaliziwa.

Katika kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unaanza, Mkurugenzi wa Kampuni ya Wanyumbani Construction, Fakihi Bakili, alichangia mifuko 100 ya saruji kwa ujenzi wa zahanati hiyo na Umoja wa Wachimbaji Wadogo Mgodi wa Namungo ambao uko jirani na kijiji hicho, waliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles