27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

LOWASSA, SUMAYE WAMFUTA MACHOZI LEMA MAHABUSU

Na JANETH MUSHI – ARUSHA


lowassa-picMAWAZIRI wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, jana wamemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema katika Gereza Kuu la Kisongo mjini hapa.

Lowassa akiongozana na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye pia ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika katika gereza hilo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Calist alisema Lowassa alifika gerezani hapo saa tano asubuhi huku Sumaye aliyeongozana na Naibu Meya wa Arusha, Viola Lazaro akifika baadaye saa saba mchana.

Calist alisema Lowassa akizungumza na Lema, alimwambia kuwa mahakama ndiyo chombo pekee kinachoaminiwa na wananchi, hivyo kinapaswa kutenda haki kwa watu wote.

Alisema Lowassa aliridhishwa na afya ya Lema na kumtaka awe mvumilivu, hasa katika kipindi hiki anachokabiliwa na kesi na aliwataka wananchi wa Arusha Mjini kumwombea kiongozi huyo.

“Watanzania wana matumaini makubwa sana na mahakama, wanaamini chombo hiki pekee ndicho kitakachowapa haki yao, hivyo kwa mwaka 2017 mahakama itoe haki na kuendesha kesi bila upendeleo kwa sababu ndiyo sauti ya wanyonge, nakutakia amani na mwaka mpya mwema,” Calist alimnukuu Lowassa.

Kwa upande wake, Sumaye alisema kuwa alimtaka mbunge huyo kuwa jasiri katika kipindi hiki kwa sababu suala linalomkabili litafika mwisho.

“Mimi nilikuja tu kumsalimia, kumjulia hali ya afya yake kwa sababu Lema tangu amekaa huku gerezani nilikuwa sijapata nafasi ya kuja kumtembelea, kwa vile wakati huu niko katika maeneo haya ya Kaskazini, nikasema nije kumsalimia, afya yake nzuri na nimemuona hana wasiwasi, naona kabisa amekaa vizuri, ameelewa hiyo hali na amepokea, hana uso wa kusononeka na hilo limenipa moyo.

“Nimemwachia ujumbe ‘just be strong’ (awe jasiri), haya yote yatapita muda wake ukifika, suala lake liko mahakamani sio la kisiasa, hata kama lililomleta huku linahusiana na siasa, suala la dhamana tunatarajia litafika mwisho wake, lakini nimemwambia hata kama dhamana ikikosekana, bado kesi ya msingi itafika mwisho wake, asiwe na wasiwasi wala hamaki, awe jasiri asikate tamaa,” alisema.

Desemba 11, mwaka jana, Katibu wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, alimtembelea Lema katika gereza hilo na alimtia moyo aendelee na mapambano na kumtaka asikate tamaa ya kupigania haki za Watanzania.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana akiwa nje ya Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa mahakamani Novemba 11, mwaka jana akikabiliwa na kesi za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli na hadi wakati huo bado anashikikiwa mahabusu katika gereza hilo.

Januari 4, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Arusha inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa namba 135 ya mawakili wa Serikali waliyokata kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliompa Lema dhamana, hata hivyo uamuzi huo haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles