Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Majaji wapya 14 wamepigwa msasa katika semina ya mafunzo elekezi huku wakitakiwa kujipa muda wa kusoma majalada ya kesi hususan za madai ambayo wakati mwingine hayahitaji kukaa muda mrefu na yanahitaji uamuzi mdogo yaishe
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo Mei 7, katika ufunguzi wa mafunzo hayo na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma na kuongeza kuwa Mahakama ya Tanzania inafanya kazi kwa mujibu wa sheria ya nchi hivyo lazima wajue malengo yao na kuelewa majukumu yao mahali popote wanapokuwa.
Amesema mafunzo hayo ni hatua ya kwanza kuelewa kwamba kazi ya ujaji inahitaji mafunzo endelevu kwa kuwa kuna waliokuwa mawakili wa kujitegemea, wasajili na kwamba kazi ya ujaji ni ya kipekee na si kazi rahisi.
“Natoa onyo kwa majaji wapya kujua kwamba hukumu zinapopatikana katika mitandao kosa moja litajulikana duniani kote.
“Zamani kulikuwa na dhana majaji wanajua sheria, lakini kuna mambo mengi ambayo hawakuweza kuyafanya wakati wanafundishwa sheria kuna matumizi ya Tehama, Sheria ya Mitandao hivyo elimu endelevu kwa majaji ina umuhimu sana,” amesema.