25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAWAGOMEA WABUNGE WALIOFUKUZWA CUF

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imegoma kutoa amri ya muda waliyoiomba wabunge wanane na madiwani wawili waliofukuzwa CUF wakati wa usikilizwaji wa pingamizi dhidi ya maombi yao ya zuio.

Uamuzi huo ulitolewa jana mahakamani hapo na Jaji Lugano Mwandambo, baada ya kusikiliza maombi ya mdomo yaliyowasilishwa na wakili wa wadai, Peter Kibatala.

Kibatala aliomba mahakama itoe amri ya muda kwamba hali iliyopo sasa ibaki kama ilivyo, wabunge wapya wasiapishwe, madiwani wasiteuliwe wala kuapishwa hadi mapingamizi ya Jamhuri yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

“Mahakama haioni tishio la chochote kutokea kati ya jana (leo) na siku ya uamuzi wa mapingamizi ya awali katika maombi ya zuio na hivyo haioni sababu ya kutoa amri za muda wakati wa usikilizaji wa mapingamizi,” alisema Jaji Mwandambo.

Kutokana na uamuzi huo wabunge hao wanasubiri Agosti 25, mwaka huu ambapo mahakama hiyo itatoa uamuzi wa mapingamizi yaliyowasilishwa, huku mkutano ujao wa Bunge ukitarajiwa kuanza Septemba 5, mwaka huu.

Wabunge hao waliovuliwa wanaiomba mahakama itoe zuio la kuapishwa kwa wabunge hao wapya, hadi kesi yao waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama wao itakapotolewa uamuzi.

Katika pingamizi hilo Mwanashera Mkuu wa Serikali ambaye ni miongoni mwa wadaiwa akiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vicent Tango pamoja na mambo mengine aliomba maombi yatupwe kwa sababu hayana msingi kisheria.

Mahakama imepanga kusikiliza pingamizi hilo kwa njia ya maandishi na uamuzi utatolewa Ijumaa wiki hii.

Jaji Mwandambo aliamua kusikiliza kwanza pingamizi hilo la awali kwa njia ya maandishi ambapo Jamhuri watawasilisha hoja zao za maandishi Agosti 18 na wabunge na madiwani watajibu hoja hizo  Agosti 21 na Agosti 22, ambapo upande wa  Jamhuri utajibu kama utaona kuna haja ya kufanya hivyo na uamuzi utatolewa Agosti 25.

Wabunge hao walikuwa wakipinga kuapishwa kwa wabunge nane walioteuliwa na  kutangazwa na Tume ya  Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wabunge  walioteuliwa na NEC katika kikao chake cha Julai 27 mwaka huu  ni pamoja na Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Kiza Mayeye, Zainab Mndolwa, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Magogo, Alfredina Kahigi na Nuru Bafadhili.

Wabunge hao wanane waliovuliwa ubunge walipeleka maombi yao wakiomba mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya wabunge nane wateule kuapishwa.

Katika maombi hayo  madogo  namba 447 ya mwaka huu  ilieleza kuwa mdaiwa wa kwanza ni Katibu wa Bunge, huku mdaiwa wa pili akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na  mdaiwa wa tatu ni Bodi ya Wadhamini wa Chama cha CUF pamoja na wabunge wanane wateule.

Wabunge hao walifungua maombi katika mahakama hiyo  wakiomba mahakama itoe amri ya zuio kwa Bunge ili wabunge walioteuliwa baada ya wao kuvuliwa uanachama wasiapishwe.

Uteuzi huo wa wabunge hao wateule wa CUF umefanyika baada NEC kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge  ambaye kwa mujibu wa Kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 alitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwepo kwa nafasi wazi nane  za wabunge wa viti maalum kupitia chama cha CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles