Na MWANDISHI WETU
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemzuia Msajili wa Vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi asitoe fedha za ruzuku kwa Chama Cha Wananchi (CUF).
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, CUF, Mbarala Maharagande imeeleza kwamba uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Wilfred Dyansobela.
Akitoa uamuzi huo Jaji Dyansobela amemtaka Msajili wa vyama vya siasa asitoe fedha za ruzuku mpaka hapo shauri namba 21/2017 dhidi ya msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) litakaposikilizwa.
Shauri hilo linahusu fedha za ruzuku Sh.milioni 369 ambazo zinadaiwa kutolewa kwa njia ya udanganyifu kwa chama hicho kwa upande wa Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba.
Katika shauri hilo Wakili Juma Nassor aliyekuwa anakitetea CUF aliwasilisha maombi hayo kwa kusisitiza kuwa kwa mazingira yaliyopo ndani ya chama hicho ni vyema na busara kwa fedha za umma zilizopaswa kutolewa kwa ruzuku kwenye chama hicho ziendelee kubaki serikalini
Mawakili Nassor aliiomba Mahakama Kuu kwamba uamuzi huo pia ufungamane na Kesi ya Msingi namba 23/2016 ya kuhoji maamuzi ya Msajili kumtambua Profesa Lipumba kwa nafasi ya Uenyekiti ambayo ipo mbele mbele ya Jaji Kihijo ambayo kwa sasa imekatiwa Rufa kwa maombi ya kufanyiwa marejeo mbele ya Mahakama ya Rufaa-Tanzania.