SAN FRANCISCO, MAREKANI
MAJAJI wa Mahakama ya Rufaa ya San Francisco nchini Marekani, inachunguza sababu iliyomfanya Rais Donald Trump kutangaza amri ya kuzuia wahamiaji kutoka nchi saba za Kiislamu.
Uamuzi huo umetokana na Serikali ya Marekani kutuma hoja zake mahakamani, ikitetea amri hiyo ya Rais Trump, ambayo imeshutumiwa vikali ndani na nje ya taifa hilo.
Majimbo ya Marekani yenye shaka na amri hiyo, nayo pia yametakiwa kujieleza.
Mahakama hiyo itaamua kabla ya wiki hii kupita iwapo amri hiyo ya rais ibatilishwe au iendelezwe.
Januari 27, mwaka huu, Trump alitoa amri ya kuzuia raia kutoka mataifa saba ya Kiislamu kuingia Marekani kwa kile alichoeleza kuwalinda raia wake dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.
Hata hivyo, mahakama ilizuia utekelezaji wa amri hiyo hadi kesi iliyowasilishwa kuipinga itakapotolewa uamuzi.