25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI, WAZIRI MKUU ETHIOPIA WATOA TAMKO ZITO MTO NILE

AZIZA MASOUD NA LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, wamekubaliana juu ya matumizi ya Mto Nile kwa kubainisha kuwa mto huo unapaswa kunufaisha nchi zote zinazozunguka na si kufanywa hati miliki ya nchi moja.

Pamoja na hilo, viongozi hao wamekubaliana mambo mengine 15, ikiwamo ushirikiano katika sekta ya anga, kilimo, viwanda na madini.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kumpokea na kufanya mazungumzo ya faragha na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Desalegn, aliyewasili nchini jana kwa ziara ya siku mbili.

Kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile, ambayo katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakiibua maneno na hata kutishia baadhi ya nchi kuingia vitani, Rais Dk. Magufuli alisema matumizi ya Mto Nile yanapaswa kuwanufaisha wananchi wote wanaoishi pembezoni mwa mto huo.

“Moja ya mambo tuliyokubaliana ni pamoja na matumizi ya Mto Nile, lazima yanufaishe nchi zote zinazopita kandokando ya mto huo, kusiwe na mtu mmoja anayetawala kufikiri kuwa mto huo ni wa kwao,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Kwa muda mrefu sasa baadhi ya nchi ambazo mto huo umepita zimekuwa katika mgogoro, msingi wake ukiwa ni mikataba ya kikoloni iliyotiwa saini mwaka 1929 na 1959, ambayo inaelekeza asilimia 90 ya maji ya Mto Nile yametengwa kwa ajili ya nchi ya Misri.

Nchi zilizo katika njia ya mto huo kama Uganda, Kenya na Ethiopia zinasema hali hiyo ni dhuluma kwao na zimekuwa zikitaka yafanywe makubaliano mapya, ingawa kwa kipindi cha miaka 13 ya majadiliano hakuna kilichofikiwa.

 

 

Itakumbukwa nchi ya Ethiopia iliwahi kuingia katika mgogoro na Misri kiasi cha nchi hiyo kusogeza majeshi yake mpakani, baada ya kuamua kutumia maji ya mto huo kwa ajili ya kuzalisha nguvu za umeme.

Kabla ya hapo, wakati huo akiwa Waziri wa Maji, Edward Lowassa, alitaka kuingiza nchi katika mgogoro mkubwa na Misri baada ya kuruhusu maji ya Ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikuu cha Mto Nile kutumika katika mikoa ambayo ilikuwa inakosa maji.

Katika kile kinachorandana na uamuzi wa ama Ethiopia au ule uliopatwa kufanywa na Lowassa, ambaye pia amepata kuwa Waziri Mkuu, jana Rais Dk. Magufuli alionekana kuunga mkono kile kilichopata kufanywa na Ethiopia kwa kutumia mto huo kuzalisha umeme.

Alisema hadi sasa Ethiopia ndiyo nchi pekee iliyoweza kutumia maji ya mto huo kutokana na uamuzi wake wa kujenga bwawa la umeme lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 6,000, licha ya mpango wa ujenzi huo kupingwa na Misri.

Rais Dk. Magufuli alisema kutokana na nchi ya Ethiopia kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango cha juu kwa kutumia mto huo, Waziri Mkuu huyo amemuahidi kumpa Megawati 400 baada ya kumuomba.

Pamoja na hilo, alisema Desalegn ameahidi kuleta wataalamu walioshiriki kujenga mradi huo wa umeme ujulikanao kama “Great Ethiopian Renaissance Dam-GERD” kushirikiana na wataalamu wa hapa nchini ili kuongeza uzalishaji.

Alisema kwa sasa Tanzania ina umeme unaofikia Megawati 1,500 nchi nzima, kiasi alichoeleza kuwa ni kidogo kwa nchi inayoingia katika uchumi wa viwanda.

“Ukitaka kujenga uchumi wa viwanda ni lazima uwe na umeme wa kutosha, sasa hapa kwetu umeme unaotumika nchi nzima ni Megawati 1,500 tu.

“Nilimuuliza kwao umeme wanauzaje akaniambia kuwa ni kati ya senti sita hadi saba, sasa kwa kutuletea umeme ule Tanesco (Shirika la Umeme Nchini) watajifunza na kuona kuwa wapo wenzao wanazalisha umeme wa bei nafuu na kujua wenzao wanazalishaje na kuuza kwa bei nafuu,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Mbali na hilo, nchi hizo pia zimekubaliana kushirikiana katika eneo la usafiri wa anga ambapo Ethiopia itajenga kituo cha mizigo kitachokuwa kikubwa zaidi barani Afrika.

Kwa mujibu wa Rais Dk. Magufuli, nchi hiyo pia kupitia watendaji wa Shirika lake la Ndege (Ethiopia Airlines) itabadilishana uzoefu na Shirika la Ndege Nchini (Air Tanzania) kuhusu kuendesha biashara hiyo ambayo wamekuwa wakiifanya kwa miaka mingi.

“Ethiopia ina ndege nyingi kubwa, wana ndege kubwa zaidi ya 96 na wameagiza nyingine 42, ndege za kimataifa zinazofanya kazi zinatua katika viwanja zaidi ya 92 na viwanja vya ndani zaidi ya 20, kwa uzoefu walionao tukidumisha uhusiano katika sekta hii na sisi tutafika mbali,” alisema.

Alisema Ethiopia pia imekubali kuwasaidia Watanzania kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ya anga pamoja na kutoa matengenezo kwa ndege zitakazokuwa zinapata hitilafu.

 

 

 

Ziara ya Desalegn inatarajiwa kumalizika leo kwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam, ambayo wamekubaliana kuitumia kwa ajili ya kupitisha mizigo ambayo baadaye itasafirishwa kwa kutumia ndege zao.

Katika eneo la viwanda, nchi hizo zimekubaliana biashara ambayo inahusisha viwanda vya ngozi, nyama na maziwa kwakuwa nchi hiyo imebahatika kuwa na mifugo mingi.

Mbali na viwanda, maeneo mengine waliyokubaliana ni utalii, kilimo, ulinzi, nishati, viwanda, mawasiliano pamoja na viza ambapo asilimia kubwa ya wawekezaji wanaotoka Ethiopia wanashindwa kuweka mitaji mikubwa nchini kwa kuwekewa kikomo cha wafanyakazi.

 Pia alisema kuwa, nchi hizo zimekubaliana kukuza lugha ya Kiswahili, ambapo Waziri Mkuu huyo ameahidi kuteua Chuo Kikuu kimoja nchini Ethiopia kitakachofundisha lugha hiyo, huku Rais Dk. Magufuli akiahidi  kutoa wataalamu kwenda kufundisha nchini humo.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli amesema nchi hiyo pia imeonyesha nia ya kufungua ubalozi wake wa kwanza hapa nchini, ambao utajengwa mkoani Dodoma.

“Tumekubaliana pia watafungua Ubalozi Dodoma, nitampa eneo la kujenga ubalozi bure pamoja na makazi ya balozi,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Naye Waziri Mkuu Desalegn akizungumza wakati wa hafla hiyo, alisema nchi hizo zimekuwa na vitu vingi ambavyo wamekuwa wakishirikiana, pia kama Taifa wana mambo mengi ya kujifunza kwa Tanzania, hasa kwenye maendeleo.

Hakuna haja ya kwenda mbali, hatuhitaji kwenda mbali, dira ya maendeleo sasa inabadilika, hatuhitaji kwenda Ulaya wala Marekani, sasa ni Afrika, hivyo tunahitaji kuwa na ushirikiano ambao unaweza kupatikana hapa kwa sababu Ethiopia na Tanzania si washindani.

“Naamini tutatumia makubaliano tuliyofikia kuleta mabadiliko katika maeneo mbalimbali, tusiangalie tu miji mikubwa, tuangalie pia watu wa chini kama vile wakulima kwa kuzingatia Tanzania imekuwa na maendeleo mazuri katika sekta hii,” alisema Desalegn

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles