25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI KUFUNGUKA TENA SAKATA LA DAWA ZA KULEVYA?

Na MWANDISHI WETU-Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli leo anatarajiwa kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na wenzake Kamishna wa Operesheni, Mihayo Msikela na Kamishna wa Intelijensia, Fredrick Kibuta, katika hafla itakayofanyika Ikulu Dar es Salaam.

Kutokana na vita ya sasa ya kuwakamata watu wanaodaiwa kutumia na kuuza dawa hizo inayoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, pengine ni wazi kuwa Rais Magufuli atakuwa na la kuzungumza.

Hoja hiyo inapewa nguvu na wadadisi wa mambo kutokana na namna sakata hilo lilivyotikisa sehemu tofauti, ikiwamo mhimili wa Bunge ulioazimia kuwa Makonda aitwe katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge baada ya kutuhumiwa kuwakashifu wabunge.

Makonda anadaiwa kuwakashifu wabunge wakati alipotaja hadharani majina ya wasanii, wanasiasa na wafanyabiashara aliowataka kufika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam ili wahojiwe kuhusu tuhuma zinazowakabili.

Uteuzi huo wa Sianga umekuja takriban wiki moja baada ya Makonda kuendesha operesheni hiyo na unatarajiwa kupanua wigo wa vita hiyo inayotajwa kuwa itaendeshwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria chini ya mamlaka hiyo.

Baada ya hoja ya dawa za kulevya kuibuka wiki hii na jinsi Makonda anavyolishughulikia suala hilo, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), alikumbusha umuhimu wa kuunda mamlaka hiyo kama sheria mpya ya kupambana na dawa za kulevya inavyoagiza.

Bulaya aliwahi kuwasilisha hoja binafsi bungeni mwaka 2013 akitaka kutungwa kwa sheria na uwapo wa mamlaka hiyo iliyopewa nguvu na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (CCM) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama.

Pia Juni, mwaka jana, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alipozungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya na Usafirishaji Haramu, alisema ametia saini sheria mpya ya dawa za kulevya ya mwaka juzi iliyotarajiwa kwenda sambamba na kuundwa kwa mamlaka itakayoongoza vita hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles