29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAGONJWA YASIYO YA KUAMBIKIZA YANAVYOMALIZA WATU

Na LEONARD MANG’OHA,

MAGONJWA yasiyo ya kuambukiza yametajwa kuathiri watu wengi zaidi barani Afrika na mataifa yanayoendelea. Maradhi hayo yamesababisha vifo milioni 36 mwaka 2008 duniani kote.

Asilimia 63 ya vifo vyote vilivyotokea mwaka huo, asilimia 48 vilichangiwa na magonjwa ya moyo.

Magonjwa mengine yanayotajwa kuongezeka kwa kasi na kusababisha vifo ni saratani, magonjwa sugu ya hewa, kisukari, magonjwa ya macho yasiyoambukiza na seli mundu (sickle cell).

Miongoni mwa vyanzo vya magonjwa haya ni pamoja na utumiaji ovyo wa pombe, uvutaji sigara, kutofanya mazoezi, kutokula mbogamboga na matunda na ulaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha mafuta.

Mkurugenzi wa magonjwa yasiyoambukiza wa Wizara ya Afra, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Ayoub Magimba anasema magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi duniani kote hasa katika nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.

Mwaka 2005 magonjwa hayo yalisababisha vifo milioni 35 kati ya vifo milioni 58 vilivyotokea duniani kote kwa mwaka huo.

“Hapa Tanzania, utafiti uliofanyika katika wilaya nne kuanzia 1994 hadi 2002 ulionyesha kuwa asilimia 18 hadi 24 ya vifo vilivyotokea vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema Profesa Magimba.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria kuwa asilimia 20 ya vifo vilivyotokea nchini mwaka 2005 vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ambapo vifo vilivyotokana na magonjwa ya moyo ni asilimia 9; saratani asilimia 4, magonjwa ya mfumo wa hewa asilimia 2,  kisukari asilimia moja na magonjwa mengine sugu asilimia 4.

Muda mrefu sasa Serikali kupitia idara zake imekuwa ikiandeleza tafiti mbalimbali ambapo katika utafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mwaka 2012, ulionyesha kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa mujibu wa Magimba, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta sigara licha ya kuchangia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama mapafu na ini, kutokana na moshi wa sigara.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 29.3 wanakunywa pombe; asilimia 97.2 wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa wiki hali inayochangia ongezeko la magonjwa hayo kutokana na kukosa baadhi ya madini muhimu yanayopatikana katika mboga mboga.

Unene ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuchangia magonjwa hayo hasa shinikizo la damu ambalo limewaathiri zaidi watu wenye umri wa kuanzia miaka 45 na kuendelea.

Utafiti unaonyesha asilimia 26 ya wananchi ni wanene kupita kiasi, 26 wana lehemu (cholesterol) nyingi mwilini, 33.8 wanamafuta mengi, 9.1 wana kisukari na asilimia 25.9 wana shinikizo la damu.

“Utafiti huu pia ulionyesha robo ya wananchi waliohojiwa hawajishughulishi na kazi za nguvu na hawafanyi mazoezi japo hata mara tatu kwa wiki, hivyo kuchangia kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema Profesa Magimba.

Anasema magonjwa ya akili yamekuwa yakiongezeka duniani hali inayotishia uhai wa watu ikiwa hawatazingatia kanuni bora za maisha.

Ugonjwa wa saratani umetajwa kuwa ni miongoni mwa magonjwa saba yanayoongoza kwa kusababisha vifo nchini, ambapo wastani wa wagonjwa saba hugundulika kuwa na ugonjwa huo kila siku.

Profesa Magimba anasema saratani ya shingo ya kizazi kwa akina mama ndiyo inayoongoza katika saratani zote kwa kusababisha vifo wa wanawake wengi nchini.

Serikali imekuwa ikipambana kuhakikisha wanapunguza kasi ya kuongezeka kwa magonjwa haya hususan saratani.

Profesa Magimba anasema wanaendelea na juhudi za kuboresha huduma za kinga kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya pombe, kuvuta sigara na kupima afya mara kwa mara.

“Pia tunaendelea kuimarisha huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na dawa, vifaa tiba na kuweka wataalamu. Pia kuimarisha huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo na saratani kwenye hospitali kama KCMC na Bugando,” anasema.

Hivi karibuni Serikali iliboresha Hospitali ya Ocean Road ya Dar es Salaam ambayo imekuwa tegemeo kubwa kwa wgonjwa wa saratani nchini.

Ni wazi kuwa magonjwa haya yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na wadau wa masuala ya afya sambamba na wananchi kuzingatia taratibu bora za maisha ili kuepuka vifo visivyo vya lazima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles