Na JOYCE KASIKI-DODOMA
IMEELEZWA kuwa kufikia mwaka 2030, kutakuwa na ongezeko la magonjwa mapya 30 kwa mwaka kutoka matano hadi nane ambayo hujitokeza hivi sasa kila mwaka duniani.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dodoma na Mjumbe wa Afya Moja, Profesa Japhet Killewo wakati akitoa mada kwenye kikao kazi cha wadau wa Afya Moja.
Kikao hicho kilishirikisha wataalamu kutoka sekta ya afya, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na sekta ya mazingira, lengo likiwa ni kuunganisha nguvu katika kupambana na magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Profesa Killewo alisema ongezeko hilo la magonjwa mapya ni kutokana na kuongezeka kwa watu duniani hasa kwa chi zinazoendelea.
“Mambo yote hayo yanaongeza uwezekano wa binadamu na mnyama au mnyama pori kukaa pamoja maana mambo hayo yote hufanyikia porini. Ugonjwa ukitokea kwa sasa ni rahisi kuenea kwa kasi dunia nzima kutokana na kurahisishwa kwa usafiri tofauti na zamani,”alisema Profesa Killewo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, Profesa Faustine Kamuzora aliwataka wadau hao wa Afya Moja kushirikiana huku kila mmoja akitimiza wajibu wake kikamilifu.