25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGAZETI KUSAJILIWA USAJILI UPYA

ELIZABETH HOMBO Na MAMII MSHANA (TURDACO) – dar es salaam

SERIKALI imetaka magazeti, majarida na machapisho mbalimbali kuomba upya leseni za kuendesha shughuli zake, jambo ambalo kwa sasa litakuwa likifanyika kila mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa habari wamekosoa hatua hiyo, wakisema inaonyesha dhana ya ukandamizaji wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

Novemba 16 mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alitia saini sheria hiyo baada ya kupitishwa na Bunge, huku kukiwa na mvutano mkubwa kati ya wadau wa habari na Serikali kwa upande mmoja na Bunge kwa upande mwingine.

                                                                                      

ALICHOSEMA DK. ABBASI

Jana Dk. Abbasi alisema wamiliki wa magazeti na majarida ambao wana usajili kwa sasa, wanatakiwa kuomba usajili mpya kuanzia jana hadi Oktoba 15.

Alisema utaratibu huo mpya utawahusu wamiliki wote wa magazeti (Newspaper), majarida (journals, magazines na newsletters).

Dk. Abbasi alisema baada ya muda huo, magazeti na majarida ambayo hayatasajili upya, hayataruhusiwa kuchapishwa kwani yatakuwa yametenda kosa kisheria.

Alisema utoaji huo wa leseni ni kwa matakwa ya kifungu cha 5 (e) cha sheria hiyo na kwa kanuni ya 7 ya kanuni za sheria za habari za mwaka 2017, zilizochapishwa kwenye tangazo la Serikali Na 18 la Februari 3.

“Sheria na utaratibu wa sasa unafuta mfumo wa awali wa utoaji wa hati za usajili wa magazeti na majarida, uliokuwa ukitumika kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo kwa sasa imefutwa.

“Aidha leseni hizi zitahuishwa kila mwaka kwa mujibu wa kanuni za 8(3) na 12(1)(2) za kanuni za sheria ya huduma za habari mwaka 2017,” alisema Dk. Abbasi.

Akizungumzia taasisi za Serikali, alisema zenyewe kigezo cha cheti cha usajili wa kampuni hakitazihusu, badala yake watatakiwa kuwasilisha barua kutoka kwa mtendaji mkuu wa taasisi.

“Mfumo wa utoaji leseni za machapisho umerahisishwa, hivyo ndani ya siku tatu leseni itakuwa tayari imeshatoka. Leseni hizo zitahuishwa kila mwaka kwa mujibu wa kanuni zilizopo katika sheria ya huduma za habari.

 TAKWIMU MUHIMU

Kwa mujibu wa takwimu zilizo kwenye tovuti ya Idara ya Habari – Maelezo, idadi ya magazeti na majarida yaliyopo ni 433.

Mwaka jana, Serikali ilifuta usajili wa magazeti 473 kupitia tangazo lake lililochapishwa katika Gazeti la Serikali lenye namba 195 (Supplement No. 23) la Juni 10, 2016 kutokana na kile ilichosema magazeti hayo hayakuchapishwa kwa miaka mitatu mfululizo.

 MASHARTI LESENI MPYA

Tovuti ya Idara ya Habari – Maelezo, ilitaja masharti ya kupata leseni mpya kuwa ni pamoja na kupeleka cheti cha usajili wa kampuni, taasisi au aina nyingine ya usajili wa kisheria, huku taasisi za Serikali zikitakiwa kuwasilisha barua kutoka kwa mtendaji mkuu.

Sharti jingine ni kupeleka andiko la mradi wa gazeti au jarida linalojumuisha dira, dhima, sera ya gazeti ama jarida husika.

Maelezo ya mahali au eneo la kufanyia biashara, wasifu binafsi (CV) na vyeti vya taaluma vya mhariri na waandishi, ni vitu vingine vitakavyotakiwa kupelekwa na mwombaji wa leseni.

Pia mfano wa muundo au mwonekano wa gazeti ama jarida na malipo ya ada ya Sh milioni moja, vitatakiwa kupelekwa na mwombaji.

 MAONI YA WADAU

Kutokana na taarifa hiyo ya serikali, wadau mbalimbali walitoa maoni yao, huku wakikosoa kilichotangazwa na Dk. Abbasi.

 JENERALI ULIMWENGU

Mwanahabari mkongwe ambaye pia ni mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, alisema: “Tangazo la leo (jana) ni kuendeleza sheria mbovu ambayo ni kandamizi na kumaliza kabisa uhuru wa habari na mawasiliano.

“Tulipinga mahakamani… hata wale walioona sheria hii ni nzuri watakuja kuona ni mbaya, uhuru wa habari katika nchi hii haupo tena.

“Tujiandae kuwa na jamii ambayo haitakuwa na vyombo vya habari, isipokuwa vipaza sauti vya Serikali na chama tawala,” alisema Ulimwengu.

 TEF

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema sheria hiyo ilipitishwa hivyo hakuna namna, pamoja na kwamba ina makandokando mengi, wanalazimika kuitekeleza.

Alisema kitendo cha kusajili gazeti kwa Sh milioni moja kila mwaka ni maumivu na kwamba kuna uwezekano baadhi ya magazeti yakafa kwa sababu ya gharama hiyo.

Balile alisema kwa sasa gazeti moja litakuwa na leseni mbili, moja ya jiji au halmashauri na hiyo mpya iliyotangazwa jana.

“Hapa hawakutoa maelezo ya kutosha kwamba leo unasema lisajili upya sasa ukipata hiyo leseni ya Maelezo ile ya jiji inafutika? Inakuwaje biashara moja kuwa na leseni mbili?” alihoji Balile.

 UTPC

Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakari Karsan, alisema hivi sasa ukandamizaji wa vyombo vya habari umeanza kwa kuwataka watu waseme vile Serikali inavyotaka.

“Ukandamizaji umeanza kwa kutumia ‘system’ (mfumo)… sasa mnasajiliwa ili watu waseme Serikali inavyotaka. Sheria hiyo tumeipinga sana na bado pingamizi liko mahakamani,” alisema Karsan.

 LHRC

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema lengo la sheria hiyo ni kuminya uhuru wa habari kwa sababu vyombo hivyo vina vipato kidogo, hivyo ni vigumu kupata Sh milioni moja kila mwaka.

“Kuna vyombo haviko kibiashara, vipo kwa ajili ya kuhabarisha umma, itakuwa ngumu kwao kupata hiyo fedha, hili tulilipinga sana na bado tunapinga,” alisema Bisimba.

 JUKATA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema sheria hiyo haikupaswa kufanya kazi peke yake bali ilitakiwa kuwa pamoja na ile ya haki ya kupata taarifa.

“Sheria hii haikupaswa kufanya kazi peke yake bali na ile sheria mama ya haki ya kupata taarifa, lakini kumbe hawa ni danganya toto, wanataka hii ya kudhibiti vyombo vya habari.

“Kuna mambo yanakosekana katika sheria hii, kwanza haki ya waandishi na wananchi kupata na kutafuta taarifa.

“Sheria hii imeanza kufanya kazi kinyume na taratibu na sheria pacha, kama pacha mmoja anapelekwa shule halafu mwenzake anaachwa inakuwa ni ajabu.

“Sheria hii imekuja, sasa imegeuka nyundo ya Serikali kudhibiti vyombo vya habari,” alisema Kibamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles