NA LULU RINGO
BONDIA ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo, ametamba kumchapa mpinzani wake Charles Misanjo kutoka Malawi kwa K.O, katika pambano litakalofanyika kesho kwenye Ukumbi wa PTA, Sabasaba, Dar es Salaam.
Pambano hilo la raundi 12, ni kwa ajili ya la kuchangia taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za sekondari za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo lengo ni kupata taulo 40,000.
Akizungumza leo wakati wa kupima uzito, katika viwanja vya Las Vegas, jijini Dar es Salaam, Maugo, alisema amejiandaa kumaliza pambano hilo mapema kwa kumpiga mpinzani wake kwa K.O.
Maugo aliwataka mashabiki wa mchezo wa ngumi kufika kwa wingi ili kufanikisha mchakato huo wa kusaidia wasichana kupata taulo hizi wanazotumia wakiwa katika siku za hedhi.
“Misanjo sio bondia wakunitisha mimi, nishakutana na mabondia wengi nchi tofauti na nimewapiga, naomba tu mashabiki wajitokeze kuona wenyewe, pia waweze kutoa mchango wao kuanikisha zoezi hili,” alisema Maugo.
Tofauti na Maugo, mabondia wengine watakaopanda ulingoni ni Ibrahim Class dhidi ya Maina Mazora na litakuwa la raundi nane.
Wengine ni wanawake, Asha Ngedere dhidi Happy Daudi na Frola Machele atazipiga na Sarafina Julius, mapambano yote yatakuwa ya raundi sita.
Kwa upande wake Mratibu wa mapambano hayo, Mbunge wa viti Maalum Mbeya, Sophia Mwakagenda, alisema wanahitaji sapoti ya Watanzania, kufanikisha mchakato huo.
Alisema njia pekee ya kuchangia ni kufika ukumbini siku ya mchezo huo kwa sababu viingilio vyao ndio vitatumika kununulia taulo hizo.
“Hata kwa wale ambao hawatafika, wanaweza kuchangia, tunapokea hata boksi moja la taulo hizo, lengo zifike 40,000, ikiwezekana ziwe zaidi kwa sababu mahitaji ni makubwa,” amesema Mwakagenda.